Kwa Phiri Simba imeula

Sunday June 13 2021
phiri pic
By Eliya Solomon

MABOSI wa Simba bado wanakuna vichwa juu mashine zipi kali mpya zitue Msimbazi kwa lengo la kuimarisha kikosi chao kwa msimu ujao wa ligi ya ndani na ile ya kimataifa, lakini ujio wa washambuliaji Justin Shonga na Moses Phiri umemshtua nyota mmoja wa kimataifa wa Tanzania.

Eliuter Mpepo aliyewahi kukipiga Zambia, Eliuter Mpepo, ndiye aliyefichua hayo alipozuingumza na Mwanaspoti na kusema kama kweli Simba itawavuta wakali hao, itakuwa imepiga bao kutokana na ukweli jamaa hao ni washambuliaji wanaojua kazi zao wawapo uwanjani na Msimbazi hawajutia.

Mpepo aliwahi kucheza na Phiri katika klabu ya Buildcon alisema kwa Mzambia huyo, Msimbazi watakuwa wamelamba dube kwani jamaa ni fundi sana.

Phiri ni kati ya majina mawili akiwamo Justin Shonga anayekipiga Cape Town ya Afrika Kusini, walio kwenye rada za Simba ili kuwabeba kuziba nafasi ya Luis Miquissone kama dili lake la kwenda Afrika Kaskazini litafanikiwa .

Mpepo, aliyewahi kukipiga Tanzania Prisons na Singida United, alisema kama nyota huyo atakuwa kwenye kiwango kile kile ambacho alimwacha nacho nchini humo, basi anaweza kuziba vilivyo nafasi ya Luis kwenye kikosi cha Simba.

“Namjua vizuri Phiri ni mshambuliaji mzuri, anaweza kushambulia kwenye maeneo yote, nyuma ya namba tisa au kucheza kama namba tisa na hata kutokea pembeni, anauwezo wa kupunguza mabeki kama Luis ambavyo amekuwa akicheza, ni msumbufu jamaa,” alisema Mpepo anayekipiga kwa sasa Cape Umoya Unuited iliyopo Ligi Daraja la Kwanza Afrika Kusini na kuongeza;

Advertisement

“Shida ambayo yupo nayo ni kwamba huwa anachemka kwenye viwanja vibovu hivyo hilo itabidi alizoee akiwa Tanzania, ila ni miaka mingi imepita pengine atakuwa amebadilika ila kwa mtazamo wangu anaweza kufanya vizuri,” alisema.

Kuhusu Shonga alisema ; “Ukiniuliza yupi ni bora kati yao ni swali gumu, nadhani anayeweza kuwa na majibu mazuri ya hilo ni kocha maana anajua kwa mifumo yake ni yupi ambaye moja kwa moja anaweza kuendana na mbinu zake lakini kwangu wote ni bora,” alisema Mpepo ambaye kwa sasa yupo nyumbani Tanzania kwa mapumziko baada ya msimu wa Ligi kumalizika.

Advertisement