Kwa Pacome, Chama na Ngoma watasubiri sana

Muktasari:

  • Chama alijiunga tena na Simba, Januari 2022 akitokea RS Berkane wakati Pacome alisajiliwa na Yanga, Julai 2023 akitokea Asec Mimosas.

WAKATI mtandao wa Transfermrkt ukionyesha kuwa Pacome Zouzoua ana thamani ndogo kuliko Clatous Chama na Mzamiru Yassin, kiungo huyo wa Yanga ameonekana kuwakimbiza wawili hao wa Simba katika takwimu za uwanjani msimu huu hadi sasa.

Kwa mujibu wa mtandao huo ambao umekuwa ukitoa tathmini ya thamani za wachezaji sokoni, Fabrice Ngoma, Chama na Mzamiru  wameonekana kuwa na thamani kubwa kulinganisha na Pacome hadi kufikia jana.

Mtandao huo umebainisha kuwa thamani ya Ngoma kufikia Oktoba 25, 2023 ilikuwa ni Euro 300,000 (Sh820 milioni), Mzamiru Yassin akiwa na thamani ya Euro 175,000 (Sh477.9 milioni), Chama ana thamani ya Euro 150,000 (Sh409.7 milioni) huku mtandao huo ukiwa haujabaini thamani halisi ya Pacome kwa sasa na umeendelea kuweka ile ambayo ulitoa mara ya mwisho Februari 4, 2017 ambayo ilikuwa Euro 50,000 (Sh136.5 milioni).

Pamoja na Transfermarkt kuweka thamani ya chini kwa Pacome, kiungo huyo amekuwa chachu kwa Yanga kufanya vizuri katika mashindano tofauti inayoshiriki jambo ambalo limempatia takwimu bora hadi sasa mbele ya Chama, Ngoma na Mzamiru.

Ligi Kuu
Shindano la kwanza ambalo Pacome kaonyesha makali yake ni Ligi Kuu ambapo hadi sasa amehusika na mabao mengi kuliko watatu hao ambao wanachezea Simba.

Wakati Pacome akihusika na mabao tisa, Chama hadi sasa amehusika na mabao sita, Mzamiru bao moja na Ngoma bao moja.

Pacome amehusika na mabao tisa akifunga mabao sita na kupiga pasi za mwisho tatu, Chama akifunga mabao matatu na kupiga pasi za mwisho tatu, Ngoma akifunga bao moja na Mzamiru akiwa na pasi moja ya mwisho.

Makundi Ligi ya Mabingwa
Katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Ngoma, Chama na Mzamiru wameshindwa tena kufua dafu mbele ya Pacome.

Pacome amefunga mabao matatu yanayomfanya ashike nafasi ya pili katika chati ya kuwania ufungaji bora nyuma ya Sankara Karamoko mwenye mabao manne huku Chama, Mzamiru na Ngoma wakitoka patupu.

Hata hivyo Chama alifunga mabao mawili katika mechi ya raundi ya kwanza ya mashindano hayo wakati Pacome alifunga bao moja.

Cheki Transfermarkt
VIUNGO kwa sasa ndio wanatawala chati za Ligi Kuu Bara. Ukiangalia orodha ya wafungaji unakuta kinara ni Aziz Ki mwenye mabao 10 wakimfuatia Feisal Salum 'Fei Toto' na Maxi Nzengeli kila mmoja akiwa nayo manane. Ukichungulia kwenye asisti yupo Kipre Junior wa Azam mwenye sita. Wote hao ni viungo.

Hawapo hapo kwa bahati mbaya, bali ni kutokana na namna soka la kisasa linavyochezwa, lakini pia ubora wao kwenye timu wanazocheza.

Hali iko hivyo hadi kwenye mkwanja. Wachezaji wengi wanaovuta pesa nyingi katika Ligi Kuu msimu huu ni viungo hapo utawapata kina Aziz Ki, Chama, Khalid Aucho, Ngoma na Luis Miquissone. Hao ni baadhi tu kwenye timu zinazoshika nafasi za juu kwenye msimamo.

Ubora wa wakali hao katika eneo la kiungo umekuwa ukizua mijadala mbalimbali na leo tutagusia viungo watano wenye thamani zaidi katika klabu kongwe za Simba na Yanga kutokana na takwimu za mtandao wa soko la uhamisho wa wachezaji duniani 'Transfer Markt'. Ripoti hii inahusisha viungo walioanza msimu na timu hizo zinazowakilisha Taifa kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

NGOMA (SIMBA)
Kwa mujibu wa takwimu za Transfermarkt yenye maskani yake Ujerumani, Ngoma wa Simba ndiye kiungo ghali kuliko wote walioanza msimu huu wakiwa Simba na Yanga.

Mtandao huo umebainisha kuwa thamani ya Ngoma kufikia Oktoba 25, 2023 ilikuwa ni Euro 300,000 (takriban Sh820 milioni). Kiasi hicho kimemfanya kuwa kinara mbele ya viungo wengi wakiwemo Chama, Aziz Ki, Aucho na Mzamiru Yassin.

Eneo la kwanza analomudu kucheza Ngoma ni kiungo wa kati, lakini pia anacheza kiungo wa ulinzi na kiungo mshambuliaji, na Simba imekuwa ikimtumia kwa nyakati tofauti maeneo hayo.

Mkongomani huyo ameweza kupenya katika kikosi cha kwanza cha Simba na kuaminiwa na makocha wote wawili akianza Mbrazili Roberto Oliveira aliyeondoka na sasa Mualgeira Abdelhak Benchikha.

Miongoni mwa vitu vinavyofanya thamani ya Ngoma kuwa juu ni ubora sambamba na uhamisho wake ulivyofanyika ambapo amewahi kuzichezea MK Etancheite ya DR Congo, Ifeanyi Ubah ya Nigeria, AS Vita ya DR Congo, Raja Casablanca ya Morocco, Al Faheheel ya Kuwait na Al Hilal ya Sudan.

AZIZ KI (YANGA)
Anayemfuata ni Aziz Ki. Huyu kufikia Januari 11, mwaka huu thamani yake ilikuwa ni Euro 250,000 (sawa na Sh682 milioni).
Aziz Ki eneo lake la asili ni kiungo mshambuliaji, lakini anamudu pia kucheza winga zote sambamba na kiungo wa kati.

Staa huyo raia wa Burkina Faso ndiye kinara wa upachikaji mabao kwenye ligi akifunga 10 na kutoa pasi za mwisho (asisti) mbili. Aziz Kii kwa sasa ni miongoni mwa wachezaji tegemeo zaidi ndani ya kikosi cha Yanga sambamba na timu ya taifa ya Burkina Faso kutokana na ubora wake wa kutengeneza mashambulizi na kufunga.

MZAMIRU (SIMBA)
Kulingana na Transfer Markt, nafasi ya tatu ni ya kiungo wa Simba, Mzamiru Yassin anayefuata ambapo hadi Januari 14, mwaka huu thamani yake ilikuwa Euro 175,000 (sawa na Sh477.9 milioni).

Eneo asili la Mzamiru ni kiungo wa kati na pia anaweza kucheza kama kiungo mshambuliaji. Nyota huyo alianza msimu akiwa kwenye ubora mkubwa chini ya kocha Robertinho, lakini ujio wa Benchikha ni kama umemuweka mtegoni kwani amekuwa akisota kupata muda mwingi kucheza kikosini.

Nafasi anazoweza kucheza kwa sasa Simba mara nyingi huwatumia Ngoma, Sadio Kanoute na Babacar Sarr.

CHAMA (SIMBA)
Chama wa Simba ndiye anashika nafasi ya nne ambaye kufika Januari 11, mwaka huu thamani yake ilitajwa kuwa Euro 150,000 sawa na (Sh409.7 milioni).

Chama eneo lake la asili ni kiungo mshambuliaji, lakini anamudu pia kucheza winga zote sambamba na kiungo wa kati.
Staa huyo kutoka Zambia kwa sasa amekuwa na kiwango bora akiisaidia Simba kujenga mashambulizi na kufunga. Hadi sasa Chama amepachika mabao manne kwenye ligi na kutoa asisti tatu.

AUCHO (YANGA)
Mganda Khalid Aucho wa Yanga anafuatia ambapo kufika Januari 14, mwaka huu thamani yake ilikuwa ni Euro 125,000 (sawa na Sh341.4 milioni). Aucho eneo lake asilia uwanjani ni kiungo mzuiaji akiwa na sifa za kucheza kiungo wa kati sambamba na kiungo mshambuliaji.

Kiungo huyo ambaye ni mhimili wa eneo la kati Yanga amekuwa akionyesha tofauti na viungo wengine akiwa uwanjani na pia wakati anajiunga na Wananchi, akitokea El Makasa ya Misri thamani yake ilikuwa Euro 250,000 (sawa na Sh682.8 milioni).

PACOME JE?
Kama ulimuwaza Pacome hadi Januari 30, mwaka huu, mtandao wa Transfer Markt ulikuwa haujabaini thamani yake halisi na mara ya mwisho Februari 4, 2017 ilikuwa Euro 50,000 (sawa na Sh136.5 milioni).
Staa huyo wa Yanga hadi sasa amefunga mabao sita na kutoa asisti tatu kwenye ligi. Pacome asilia uwanjani ni kiungo wa kati akimudu kucheza winga zote na kiungo mshambuliaji.

ISHI HUMU
Thamani ya mchezaji katika mtandao huo hutokana na sababu mbalimbali ikiwemo gharama ya uhamisho, ubora, umri, timu alizocheza, michuano anayoshiriki na ushiriki wake katika timu za taifa.

Pia thamani hiyo inaweza kupanda au kushuka kutokana na uamuzi wa timu inayommiliki mchezaji husika pale inapotaka kumuuza na vilevile mchezaji na timu inayomhitaji wanaweza kuongeza au kupunguza thamani.

TRANSFER MARKT NI NINI?
Huo ni mtandao wa Kijerumani ulioanzishwa miaka 23 iliyopita kukusanya na kuchakata taarifa mbalimbali za soka na wanasoka duniani ikiwemo kuainisha thamani zao, timu na makocha kulingana na soko lilivyo.

Mtandao huo hutumia pia takwimu za ligi na mashindano pamoja na na taarifa za mitandaoni kuhuisha taarifa na kuweka makadirio ya thamani halisi za wanamichezo ambazo mara nyingi zimekuwa zikionekana kuwa sahihi kwa kiasi kikubwa.