Kwa Mukoko mtateseka sana

AINA ya uchezaji wa kiungo mpya wa Yanga kutoka DR Congo, Mukoko Tonombe imewakosha wadau mbalimbali wa soka wakiwamo nyota wa zamani wa kimataifa na kusema kwa pira lake, wapinzani wa Yanga watateseka sana, kwani jamaa atafunika zaidi kadri Ligi Kuu itakavyosonga mbele.

Mukoko aliyesajiliwa msimu huu kutoka AS Vita, ameshaifungia Yanga bao moja katika ligi, huku kwenye mechi za kirafiki jamaa ametisha zaidi kwani amekuwa akifunga, lakini aina yake ya uchezaji katika kuituliza timu imewafanya wakongwe kumfungukia.

Straika wa zamani wa Yanga, Simba na Taifa Stars, Edibily Lunyamila akizungumza na Mwanaspoti mara baada ya mchezo wa kirafiki kati ya Yanga na Mwadui, alisema Mukoko ni mchezaji anayefiti vipindi vyote, akifafanua akianza kipindi cha kwanza anatuliza timu na akiingia kutoka benchi huwa mtamu zaidi.

Lunyamila alisema Mukoko ni kiungo aliyejaliwa akili ya kuusoma mchezo, kisha anajua ni jinsi gani anaweza akaisaidia timu yake kuweza kupata matokeo dhidi ya wapinzani wao ndio maana anaamini kadri akavyozoea mazingira ya soka la Tanzania, jamaa atawasumbua sana.

“Mfano mzuri ni kwenye mechi hii ya Mwadui, Mukoko na Carlinhos walipoingia tu uwanjani walibadilisha mchezo, mpaka Farid Mussa ambaye mwanzoni alionekana wa ovyo kuchezaa vizuri kwa kuchangamka,” alisema Lunyamila na aliongeza;

“Eneo la kiungo ni muhimu, ndio maana linatakiwa liwe na watu wenye maarifa mengi kama ilivyo kwa Mukoko na wenzake Yanga, ambao naamini kabisa watakuwa na msaada mkubwa kwenye timu.”

Naye Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ aliyewahi kukipiga pia Simba, Yanga na Stars, alisema Mukoko anatambua anahitaji kitu gani akiwa uwanjani, kitu kinachofurahisha kwa mchezaji huyo ni namna anavyotumia nguvu na akili kwa muda mmoja.

“Kadri anavyocheza nagundua ni mchezaji mwenye madini mengi mguuni yatakayoisaidia Yanga kwenye ligi msimu huu kwani ni mgunduzi wa haraka kujua eneo hili lina shida na anakwenda kuibia majukumu ya wengine ili mradi timu isielemewe,” alisema Malima.

Naye Mukoko alisema atazidi kujituma.