KVZ yaizima Malindi, ikiingia vita ya ubingwa

Muktasari:
- Ushindi huo uliopatikana kwenye Uwanja wa Mao A umeifanya KVZ kufikisha pointi 47, moja pungufu na ilizonazo Mafunzo inayoongoza msimamo ambayo nayo jana ilibanwa mbavu na Zimamoto kwa kutoka suluhu katika mechi nyingine ya ligi hiyo.
MAAFANDE wa KVZ jana imeizima Malindi kwa mabao 2-1 na kuchupa hadi nafasi ya pili kutoka ya nne ikiingia katika vita ya ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL).
Ushindi huo uliopatikana kwenye Uwanja wa Mao A umeifanya KVZ kufikisha pointi 47, moja pungufu na ilizonazo Mafunzo inayoongoza msimamo ambayo nayo jana ilibanwa mbavu na Zimamoto kwa kutoka suluhu katika mechi nyingine ya ligi hiyo.
Michael Joseph aliitanguliza KVZ kwa bao la dakika ya 23 kabla ya mchezaji huyo kuongeza la pili dakika ya 38 na kufanya hadi mapumziko maafande hai wawe mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili timu zote ziliungia na nguvu na hasa baada ya mabadiliko kadhaa ya wachezaji na Malindi kunufaika kwa kupata bao la kufutia machozi.
Katika mechi nyingine ya Ligi hiyo, Mafunzo na Zimamoto zilitoka suluhu kwa kutofungana Uwanja wa Mao B, huku JKU ikikumbana na kipigo cha 2-1 kutika kwa Junguni United kwenye Uwanja wa FFU Finya kisiwani Pemba.
Andrea James wa Junguni aliweka kimiani bao la kwanza dakika ya tano kabla ya Fredy Suleiman kuisawazishia JKU ambao ni watetezi wa ZPL dakika ya 55 na Chawaka alipachika bao la pili katika dakika 90+3 za nyongeza.
Ligi hiyo itaendelea leo jioni kwa Mlandege kuvaana na Tekeleza kwenye Uwanja wa Mao A. Tekeleza tayari imeshashuka daraja na msimu ujao itacheza daraja la kwanza, huku Uhamiaji itachuana na Mwenge Uwanja wa Mao B na Chipukizi watakutana na Mwembe Makumbi kwenye Uwanja wa Finya, Pemba.