Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kutana na ‘Mfalme’ Okwi wa Simba

Makamu wa Rais wa Simba ,Godfrey Nyange 'Kaburu' akiwa na okwi Desembaa mwaka juzi baada ya mechi ya Nani Mtani Jembe wakati mchezaji huyo akiwa Yanga.Simba ilishinda mabao 3-1

Muktasari:

Okwi alitoka kwao Uganda akiwa mchezaji asiye na umaarufu mkubwa, lakini mwenye kipaji cha hali ya juu na chenye mvuto. Amekuwa akicheza kandanda safi kwa muda wote lakini baadaye viongozi wa Simba walianza kumharibu taratibu baada ya kumtengenezea mazingira ya kuwa Mfalme ndani ya timu hiyo.

MSHAMBULIAJI wa Simba, Emmanuel Okwi, raia wa Uganda, ni kama mfalme ndani ya kikosi cha timu hiyo. Amekuwa staa wa timu na maisha yake yanakwenda kifalme.

Okwi alitoka kwao Uganda akiwa mchezaji asiye na umaarufu mkubwa, lakini mwenye kipaji cha hali ya juu na chenye mvuto. Amekuwa akicheza kandanda safi kwa muda wote lakini baadaye viongozi wa Simba walianza kumharibu taratibu baada ya kumtengenezea mazingira ya kuwa Mfalme ndani ya timu hiyo.

Ni ukweli kwamba Okwi amekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi cha Simba, amekuwa akicheza kwa kiwango cha juu na kuisaidia timu yake, lakini kitendo cha kumfanya Mfalme kimeanza kuwa na madhara kwenye timu kwani kimeanza kuwagawa wachezaji kwenye makundi.

Baadhi ya wachezaji wamekuwa wakikerwa na upendeleo wa wazi unaofanyika kwa Okwi. Baadhi ya viongozi wa Simba wamekuwa wakishindwa kuficha mapenzi yao kwa mchezaji huyo, wamekuwa wakiyaonyesha waziwazi jambo linaloonekana kuwakera wengine.

Inasemekana kuwa maisha ya kifalme aliyokuwa akiishi Okwi kwenye kikosi cha Simba ndiyo yaliyomfanya ayaone maisha ya Yanga kuwa magumu wakati ilipomsajili. Hakukuwa na upendeleo ndani ya kikosi cha Yanga jambo lililomfanya Okwi aone kama anaishi kwenye Dunia nyingine. Ufalme wake haukuwepo kabisa.

Ikiwa ni miezi sita pekee tangu Okwi arejee kwenye kikosi cha Simba, fahamu namna viongozi wa klabu hiyo walivyomruhusu Okwi kuwa Mfalme;

Kutumia gari binafsi mazoezini

Wakati amejiunga tu na timu hiyo baada ya kuvunja mkataba wake na Yanga, Okwi alianza kuhudhuria mazoezi ya timu hiyo akiwa na gari binafsi tofauti na wachezaji wengine waliokuwa wakitumia basi la klabu.

Mara nyingi Okwi alionekana akiwa kwenye gari hilo dogo pamoja na aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, Joseph Owino huku wengine wakipanda basi hilo la klabu, ilionekana dhahiri hakuna usawa.

Tiba ya kipekee akiumia

Wachezaji wengi wamekuwa wakiumia kwenye kikosi cha Simba. Msimu huu pekee wachezaji zaidi ya 10 wamekumbana na hali hiyo. Walioumia ni Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Raphael Kiongera, Jonas Mkude, Nassoro Said ‘Cholo’, Ivo Mapunda, Hussein Shariff ‘Casillas’ na wengine kadhaa.

Hao wote hawakupewa uzito sana, lakini alipoumia Okwi tu ikawa tatizo. Mmoja wa viongozi wa Simba tena wa juu kabisa, bila aibu alitaka kumtimua kazi Daktari wa timu hiyo, Yassin Gembe, kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kuyachukulia poa majeraha ya Okwi.

Kiongozi huyo hakuhangaika na wachezaji wengine waliokuwa majeruhi bali ni Okwi pekee. Mbaya zaidi ni kwamba kiongozi huyo aliibua mgogoro huo mbele ya wachezaji wengine wa timu jambo ambalo lilionekana dhahiri kuwa ni kitendo cha kumfanya Okwi kuwa Mfalme mbele yao.

Kucheza bila mazoezi

Kuna mambo ambayo anaweza kuyafanya na Okwi tu katika kikosi cha Simba, mchezaji mwingine akifanya anafukuzwa ama kusimamishwa. Okwi ndiye mchezaji pekee anayeweza kucheza mechi bila hata kufanya mazoezi.

Ndani ya miezi yake sita amefanya hivyo mara nyingi. Ilianzia kwenye mechi ya Simba na Yanga Oktoba 18 mwaka jana. Kikosi cha Simba kiliweka kambi Afrika Kusini kujiandaa na mechi hiyo bila ya Okwi ambaye alikwenda kwao Uganda kwenye majukumu ya timu ya Taifa ambapo pia hakucheza.

Hata hivyo licha ya kutofanya mazoezi na timu kwa siku hizo zote, bado Okwi alicheza dakika zote 90 za pambano hilo.

Wakati wakijiandaa na pambano la Mtani Jembe, Okwi aliripoti kambini siku tano kabla ya mchezo huo wakati wenzake walianza mazoezi zaidi ya wiki mbili nyuma. Licha ya hivyo Okwi aliingia kwenye mchezo huo akiwa nahodha na kucheza kwa dakika zote 90.

Ikiwa hiyo haitoshi, baada ya pambano hilo la Mtani Jembe, Okwi alikwenda kwao Uganda kufunga ndoa na aliporejea kambini mjini Unguja, Zanzibar siku hiyo kulikuwa na mchezo wa kirafiki kati ya Simba na Taifa Jang’ombe.

Kocha Phiri hakutaka kumchezesha Okwi, lakini baadaye alipokea simu kutoka kwa wakubwa wakimtaka ampange mchezaji huyo, ikawa hivyo.

Mbali na mchezo huo wa Taifa Jang’ombe, Okwi alicheza mechi dhidi ya Kagera Sugar akiwa hajafanya mazoezi yoyote. Katika hali ya kushangaza Okwi aliingia kwenye mchezo huo wa Kagera akiwa nahodha, matokeo yake aliigharimu Simba kwa kucheza chini ya kiwango, lakini hilo haliwezi kuonekana pale Simba, kwani mchezaji huyu ni Mfalme.

Ana safari balaa

Kama huna taarifa ni kwamba wachezaji na baadhi ya viongozi wa Simba wameaminishwa kuwa Okwi kwa sasa yupo kwao Uganda kumalizia fungate, lakini si kweli, hajaondoka Dar es Salaam.

Ametulia akijichana kwa raha zake wakati wenzake wapo Zanzibar kwenye Kombe la Mapinduzi. Ameruhusiwa na viongozi wa timu hiyo ambao wamemtaka arejee kabla ya mechi za ligi kuendelea.

Wamemruhusu kutocheza Kombe la Mapinduzi (lakini wakikutana na Yanga watamwita). Ufalme ulioje. Kweli Okwi alistahili fungate, lakini kwa nini afunge ndoa wakati timu ina mechi za mashindano? Kwa nini asingefunga kipindi ligi iko kwenye mapumziko?

Alifanya makusudi kwa kuwa anajua yeye ni Mfalme ndani ya timu. Mbali na hilo, Okwi amekuwa na safari nyingi za kwenda kwao Uganda pengine kuliko mchezaji yeyote wa kigeni ndani ya Simba. Amekwenda zaidi ya mara tano ndani ya kipindi cha miezi sita. Anakwenda kadiri anavyojisikia kwa sababu anajua hakuna wa kumuuliza Mfalme.

Okwi anapotea

Ufalme huu wa Okwi ndani ya Simba ni sumu kwa kiwango chake, anakwenda akishuka kiwango siku hadi siku. Okwi wa sasa si yule wa miaka miwili iliyopita. Kiwango chake kimeshuka kutokana na ufalme aliojengewa ndani ya Simba.

Tayari Okwi ameshapoteza namba kwenye timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’. Ni dhahiri kuwa akiendelea kuishi ndani ya ufalme wake pale Simba hatoweza kucheza soka la kulipwa kwenye nchi nyingine tena kwani ataishia kuwa mchezaji wa kawaida.

Hata hivyo, endapo viongozi wa Simba wataacha kuyafanya haya yote watamsaidia Okwi ambaye bado ana kipaji cha kucheza kufikia malengo yake, kwani ana uwezo mkubwa wa kuisadia Simba.