Kundemba yaizima JKU, Malindi ikizinduka ZPL

Muktasari:
- JKU inayoongoza msimamo wa Ligi ikihitaji pointi mbili tu itangaze ubingwa mapema, ilikumbana na kipigo hicho kwenye Uwanja wa Mao A, mjini Unguja.
VINARA wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), JKU jana ilijikita ikisimamishwa na Kundemba kwa kulimwa mabao 2-0 katika mechi za lala salama za Ligi hiyo, huku Malindi ikizinduka kwa Uhamiaji.
JKU inayoongoza msimamo wa Ligi ikihitaji pointi mbili tu itangaze ubingwa mapema, ilikumbana na kipigo hicho kwenye Uwanja wa Mao A, mjini Unguja.
Kipigo hicho kimeiacha JKU ikisaliwa na pointi 62 na michezo miwili kabla ya kufunga msimu, huku Kundemba ikisalia nafasi ya 12 ikiwa na alama 29.
Mabao yaliyoizamisha JKU yaliwekwa kimiani yote na Abdulhamid Juma Abdi aliyefunga dakika ya tatu na 14 ya mchezo huo. Mabao hayo yamemfanya Abdi sasa kufikisha 10 huku timu yake ikisaliwa na mechi mbili kufunga msimu.
Katika mechi nyingine iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mao B, mabingwa wa zamani wa Tanzania, Malindi iliinyoa Uhamiaji na kuiporomosha kwa nafasi japo zinalingana pointi 35 kila moja kwa sasa.
Malindi imepanda kutoka nafasi ya 11 hadi ya tisa, huku Uhamiaji ikitoka ya tisa hadi ya 10.
Uhamiaji ndio iliyokuwa ya kwanza kufunga bao dakika ya 71 kupitia Yahya Haji Salmin kabla ya Ramadhan Mponda kuisawazishia Malindi dakika ya 74 na Feisal Nassor kufunga bao la ushindi dakika moja kabla ya filimbi ya mwisho.