Kumekucha Kilimanjaro Marathon 2019

Muktasari:
- Mgeni rasmi katika mbio hizo ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe
Dar es Salaam. Macho yote na masikio yanaelekezwa Moshi wikiendi hii kushuhudia wanariadha gani wataweka rekodi mpya katika mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon 2019.
Zaidi wa washiriki 10,000 wanataraji kushiriki mbio hizo na waandaaji wamekamilisha masuala ya usajili kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi walichukua namba zao za ushiriki.
“Muamko ni mkubwa mno na tunatarajia kuwa mbio za mwaka huu zitakuwa kubwa pia,” ilisema taarifa ya waandaaji.
Waandaaji hao walisema safari hii usajili kwa njia ya mtandao na Tigo Pesa ilifanikiwa kabisa huku zaidi ya asilimia 90 ya washiriki wa mbio za kilomita 42 na 21 wakijisajili kwa njia hii ya mtandao na Tigo Pesa.
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Pamela Kikuli wadhamini mbio za Kilomita 42 alisema sisi wadhamini wakuu tunafarajika kujihusisha na tukio hili ambalo linaendelea kukua mwaka hadi mwaka,” .
Alisema inatia moyo kuona jinsi gani mbio ndefu zimekuwa maarufu mno miongoni mwa watanzania na wageni.
Meneja wa Tigo Kanda ya Kaskazini, Lilian Mwalongo alisema wamejiandaa vizuri kwa mbio za kilomita 21 na wanafurahia kudhamini mbio ambazo zimejizolea umaarufu mkubwa mno tangu waanze udhamini huu.
“Hili ni tukio kubwa na tunawaomba washiriki wote na watazamaji kuja kushuhudia kasi kubwa ya mtandao wetu wa 4G huku tukifurahia KIli Marathon,” alisema.
Meneja wa kinywaji cha Grand Malt, Silvanus Mazula alisema, mbio zetu za Kilomita 5 imekuwa kivutio kikubwa kwa wengi mwaka hadi mwaka hivi tunatarajia mashindano mazuri na makubwa zaidi mwaka huu ambapo washiriki pia watapata fusra ya kufurahia kinywaji chao cha Grand Malt.
Mgeni rasmi katika mbio hizi ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe anayetarajiwa kuanzisha mbio za kilomita 42 saa 12:45 asubuhi. Mbio za kilomita 21 zitaanza saa 1:00 asubuhi na zile za kilomita tano zitaanza saa 1:30 asubuhi.
Wadhamini wa mwaka huu ni Kilimanjaro Premium Lager, wakiwa wadhamini wa mbio za kilomita 42, Tigo mbio za kilomita 21 na Grand Malt Kilomita 5 Fun na wadhamini wa meza za maji KK Security, Keys Hotel, Kilimanjaro Water, TPC Sugar, Simba Cement, AAR, Kibo Palace, Barclays Bank, Precision Air na CMC Automobiles.