Prime
Dabi ya Kariakoo yapelekwa mkutano mkuu Yanga

Muktasari:
- Kwa mujibu wa Katiba ya Yanga, ili kuitishwa kwa mkutano mkuu wa dharura inategemea idadi ya wajumbe waliopo na ridhaa ya kamati ya utendaji ya klabu au kwa shinikizo la wanachama.
BAADHI ya wanachama wa Klabu ya Yanga wamefikia hatua ya kuiandikia barua Kamati ya Utendaji kuomba kufanyika mkutano mkuu wa dharura kabla ya Juni 15, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Katiba ya Yanga, ili kuitishwa kwa mkutano mkuu wa dharura inategemea idadi ya wajumbe waliopo na ridhaa ya kamati ya utendaji ya klabu au kwa shinikizo la wanachama.
Lakini, Katiba imeelekeza kwamba mkutano mkuu ili ufanyike inalazimu wanachama watano wa klabu hiyo kutoka kila tawi wahudhurie ambao ni wajumbe.
Kwa mujibu wa wanachama hao ambao ni viongozi wa matawi ya Yanga mkutano huo mkuu wanataka ajenda kuu iwe kujadili mchezo wa Dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba ulioahirishwa Machi 8, 2025 na kupangiwa Juni 15, 2025.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari, Mratibu wa Matawi Mkoa wa Dar es Salaam, Shabani Omary Mngoja alisema mechi hiyo namba 184 ilishapita kwa hiyo hawakubaliani na uamuzi wa Bodi ya Ligi kuipangia tarehe.
“Mashabiki 40,000 walikata tiketi bado ambao wamesafiri kutoka mikoa mbalimbali kuja Dar es Salaam, lakini Bodi ya Ligi imepanga ratiba ambayo hawakujali wale waliopata hasara ya nauli zao kutoka mikoani (ilipoahirishwa).
“Zile fedha za viingilio hakuna maelekezo ya wapi zilikwenda, Yanga sio ya viongozi tu ila wanachama. Kwa hiyo tunaungana pamoja kwamba mechi namba 184 haipo.
“Hatutakwenda kucheza mechi hiyo, kama wanaona tuna makosa basi watuchulie hatua, ifike mahali Yanga tusimame kutetea soka la Tanzania.
“Tunaiandikia rasmi Kamati ya Utendaji Yanga kwamba tunataka mkutano wa dharura, kuanzia sasa mpaka tarehe 15 Juni tutapata muda wa kulikamilisha hilo sawa sawa na katiba yetu inavyosema.
“Tunatenga siku tano za maandalizi, tutawapelekea Kamati ya Utendaji kupitia kwa mtendaji mkuu wa klabu ambayo ina orodha ya wanachama walio hai na ni wajumbe wa kamati kuu. Ili hilo liwe ajenda ya mkutano wetu mkuu wa dharura, utakuwa na mamlaka sawa na ule mkuu na uamuzi utakaofanyika ni halali, tumedhamiria na kwa hili hatutarudi nyuma.
“Mwisho wetu ni hatutacheza mechi na niwaombe Wanayanga kwamba tuna mechi tatu tumalize ligi, ukiachana na michuano ya FA na kote tuungane na timu kuisapoti,” alisema Mngoja.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Yanga, Mohamed Msumi, alisema Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ni taasisi iliyosajiliwa kama Klabu ya Yanga na zote zimesajiliwa chini ya sheria ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT). “Sisi ndio waajiri wa viongozi kwa hiyo wenye mali tunasema tupeni wenyewe mzigo wetu tunawasaidia kwa kufanya mkutano wa dharura sawa na katiba ya mwaka 2021 ibara ya 22,” alisema Msumi.
“Mkutano huu unatuhusu sisi wanachama, ndio maana tunataka ajenda tuiandae, uongozi umepeleka kesi CAS, ila tunataka kuifungua mahakama ya hapahapa.”
Viongozi wa juu wa Yanga hawakupatikana kuzungumzia madai hayo ya wanachama, lakini Ofisa Habari, Ally Kamwe alisema haipo tayari kucheza mchezo huo hadi watakapopata majibu ya kueleweka kwa nini Simba haikutokea uwanjani. Machi 8 mwaka huu, ilipangwa kuchezwa mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya Yanga dhidi ya Simba, lakini iliahirishwa na Bodi ya Ligi (TPLB) baada ya kuwepo malalamiko ya Simba kuzuiwa kufanya mazoezi Uwanja wa Mkapa siku moja kabla na watu waliotambulika kuwa ni walinzi wa Yanga.
Hata hivyo, Yanga iliweka wazi haikuridhishwa na majibu ya Bodi ya Ligi juu ya barua ya kutaka kupatiwa alama tatu za mchezo huo kwa madai kwamba kanuni za kuahirishwa mchezo zilikiukwa na kuamua rasmi kufungua kesi hiyo Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) ambayo nayo ilitoa taarifa ya kufuta na kutoendelea na shauri hilo.
CAS iliiagiza Yanga kupeleka shauri hilo kwanza katika mamlaka za ndani za uendeshaji soka na baada ya hapo ndio ilifikishe katika mahakama hiyo. Licha ya CAS kuiamuru Yanga kurudi kwanza kwenye Kamati za ndani za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kushughulikia malalamiko yao, lakini klabu hiyo imeendelea kushikilia msimamo wake wa kutocheza mechi hiyo ikikataa maagizo hayo ikieleza kutokuwa na imani na mamlaka za soka nchini, ikidai kuna uonevu, uvunjwaji mkubwa wa kanuni na upendeleo wa wazi kwa baadhi ya timu.