Kumbe Julio hajamalizana na Singida FG

Muktasari:

  • Julio alijiunga na timu hiyo Machi 13, hadi mwisho wa msimu huu akiwa na wasaidizi wake Ngawina Ngawina na Ally Mustapha ‘Barthez’ wakirithi mikoba ya Thabo Senong na msaidizi wake, Nizar Khalfan, na kuiongoza mechi mbili.

Wakati uvumi wa Kocha Mkuu wa Singida Fountain Gate, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ wa kuachana na timu hiyo ukiendelea kuenea, uongozi wa timu hiyo umeibuka na kudai kwamba bado uko kwenye mazungumzo ya kukamilisha mkataba na kocha huyo.

Julio alijiunga na timu hiyo Machi 13, hadi mwisho wa msimu huu akiwa na wasaidizi wake Ngawina Ngawina na Ally Mustapha ‘Barthez’ wakirithi mikoba ya Thabo Senong na msaidizi wake, Nizar Khalfan, na kuiongoza mechi mbili.

Katika mechi hizo walishinda mchezo mmoja wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo 1-0 na kupiteza wa kombe la shirikisho mbele ya Tabora United walipolazwa 3-0 na kuondoshwa katika michuano hiyo.

Hata hivyo, baada ya mchezo huo, Julio hakuonekana tena kikosini humo kilichopo hapa jijini Mwanza na mechi yao dhidi ya Yanga timu ilikuwa chini ya Ngawina Ngawina walipolala 3-0.

Ofisa Habari wa klabu hiyo, Hussein Massanza amesema kocha huyo bado ni mali ya Singida Fountain Gate na alishiriki kwenye programu zote za maandalizi ya mchezo dhidi ya Yanga.

Amesema kinachoendelea kwa sasa ni mazungumzo kati ya Julio na Rais wa klabu hiyo, Japhet Makau kuweka sawa vipengele kwenye mkataba wake na muda wowote ataungana na timu.

“Kutokuonekana kwake leo (juzi) siyo kwamba hayuko na timu bali anaendelea na mazungumzo na rais wa klabu kuna mambo ya kimkataba yalikuwa hayajakamilika ndiyo yanaendelea kushughulikiwa,” amesema.

“Lakini siyo shida ya fedha anashiriki kikamilifu kwenye timu na hata programu za mchezo wa Yanga ameandaa yeye, tutatoa taarifa rasmi.”