Komando Hamza Kalala aliyelala stendi akisubiri ajira

Muktasari:
Sifa zake zilianza kuzagaa wakati alipokuwa akicharaza gitaa la solo kwa umahiri mkubwa akiwa katika bendi mbalimbali jijini Dar es Salaam zikiwemo za UDA Jazz, Super Matimila, Washirika Tanzania Stars, Vijana Jazz na nyingine nyinginezo.
MKONGWE wa muziki wa dansi Hamza Kalala, alilala stendi ya basi Morogoro akiwasubiri viongozi wa Morogoro Jazz na Cuban Marimba ili aombe kazi.
Hayo aliyatamka mweyewe wakati wa mahojiano maalumu na mwandishi wa makala haya nyumbani kwake jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Hamza Kalala alijipatia sifa lukuki katika nyimbo nyingi kama vile Sifa za Stella, Mzee TupaTupa, (Vijana Jazz), Nimekusamehe lakini Sitakusahau, Nalila Masumanda (Washirika - Tanzania Stars), Almasi Orchestra, alipiga solo, Matimila bila ya kuusahau ‘Ngozi ya Kitimoto’ alioutunga na kuuimba kwa hisia kali wakati huo akiwa na bendi yake ya The Bantu Group uliowavutia wapenzi wa muziki wa dansi.
Wimbo huo ulikuwa ukianza hivi….
“Toka lini ngozi ya kiti moto ikawambwa ngomaa… kama si miujiza ni nini!! iyele iyele iyele.” hii ni sehemu ya maneno katika wimbo uliochezwa na Bendi ya Bantu Group.
Komandoo Hamza Kalala amejipatia sifa nyingi kufuatia tungo za nyimbo zake kuwa msumari kwa yeyote anayeguswa na ujumbe huo.
Makala haya yanapambanua wasifu wa mwanamuziki huyo mkongwe katika tasnia ya muziki hapa nchini.
Sifa zake zilianza kuzagaa wakati alipokuwa akicharaza gitaa la solo kwa umahiri mkubwa akiwa katika bendi mbalimbali jijini Dar es Salaam zikiwemo za UDA Jazz, Super Matimila, Washirika Tanzania Stars, Vijana Jazz na nyingine nyinginezo.
Katika mahojiano maalumu, Kalala alisema alizaliwa mkoani Tanga na kupewa jina la nyumbani upande wa baba yake la Kapesula.
Anasema babu yake Mzee Kalala aliingia nchini akiwa na dada zake wawili wakitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wakafikia katika Kijiji cha Ipwaga huko Inyonga.
Babu huyo aliishi kwa muda murefu kijijini humo hadi akawa maarufu kisha akaaminika na kufanywa kuwa mtemi.
Kalala anasema ufikapo Inyonga, familia ya Kalala ni maarufu sana hadi leo.
Mzee Kalala alikuwa mfanyakazi wa Shirika la Reli (TRC) na baadaye alihamishiwa Tanga.
Akiwa huko alibahatika kuoa mke wa kabila la Kizigua, ambaye ndiye mama wa Hamza Kalala.
Hamza alipofikisha umri wa kwenda shule alipelekwa kusoma hadi kumaliza shule ya msingi na sekondari mkoani humo.
Alianza kuhamasika katika mambo ya muziki akiwa shule ya msingi darasa la nne mwaka 1966.
Wakati huo alikuwa akimshudia baba yake akiimba na kucheza Ngoma ya Kinyamwezi ya Manyanga huko huko Tanga.
Kalala alisema hakufundishwa muziki na mtu bali ni kutokana na ngoma hizo alizokuwa akicheza na kuimba baba yake.
Aliiga upigaji wa gitaa toka kwa mjomba wake ambaye alikuwa nalo nyumbani.
Zao kuu la biashara mkoani Tanga wakati huo lilikuwa ni mkonge.
Wakata mikonge ‘Manamba’, siku za mapumziko za mwisho wa wiki walikuwa wakifanya mashindano ya ngoma za Kinyamwezi na makabila mengine waliokuwa katika mashamba tofauti ya Mkonge.
Mashamba hayo ni ya Kibaranga, Amboni na mengine mengi.
Katika ushindani huo ngoma ya Manyanga ya Wanyamwezi na ile ya Wamakonde, ndizo zilizokuwa zikitia fora kila mara.
Kalala anasema mjomba wake alikuwa na gitaa nyumbani, yeye alikuwa akijaribu kulishika gitaa hilo kama anavyoshika mjomba huyo.
Kipaji chake kilianza kijitokeza baada ya kuona haikumsumbua sana kujua kuzichambua nyuzi za gitaa hilo.
Komando Kalala mwaka 1968, alianza kupiga muziki katika bendi ndogo ya mkoani Tanga, iliyokuwa ikiitwa Kwanduru Jazz.
Bendi hiyo ilikuwa katika mashamba ya Mkonge, baadaye Hamza Kalala akajiunga na Amboni Jazz.
Alijipima uwezo wake wa muziki alipojiaunga na bendi zilizokuwapo kwenye mashamba ya mkonge kama Kwanduru na Amboni Jazz.
Hata hivyo, Kalala hakuvutiwa na maisha ya mashambani, hivyo aliamua kurudi Tanga mjini, ambako aliendelea na mazoezi ya kupiga gitaa nyumbani kwao.
Siku moja alipita raia mmoja wa Kikongo aliyekuwa akijulikana kwa jina moja la Chivosha, akavutiwa jinsi alivyokuwa akipiga gitaa. Chivosha akamuomba akajiunge katika bendi yao ya Villa Negro Successes.
Komando Kalala alisimulia kwamba alikuwa anatoroka kwenda kupiga muziki.
Baba yake alikasirika sana baada ya kusikia kuwa mwanaye anaimba na kupiga muziki katika Ukumbi wa Mwananchi uliokuwa maarufu sana wakati huo mkoani Tanga.
Mzee huyo huku akiwa amefura kwa hasira aliingia ukumbini humo kumtafuta, lakini hakumtambua.
“Baba hakunitambua mara moja, haikuwa rahisi kunifahamu kutokana na nilivyokuwa nimejiremba. Unajua kuwapo katika bendi ya Wakongo ambao wanapenda kujiremba,” alisema Kalala.
Katika bendi hiyo kulikuwepo wanawake wa viongozi wa bendi hiyo, kazi yao kubwa ilikuwa ni kumremba, ambapo siku hiyo aliyokuja baba yake alikuwa amechoma nywele, alivaa nadhifu kama wanamuziki wa Kikongo wanavyojikwatua.
“Moja ya sifa za mwanamuziki kufanya kazi na wanamuziki wa Kikongo ilikuwa uwe nadhifu, na wakiridhishwa na kazi yako wako radhi kukugharamia.
“Wanawake wao walikuwa wanachukua karibu nusu siku kunipendezesha, na kwa kweli nilikuwa nikibadilika kabisa,” anasema Kalala.
Baba yake licha ya kukodoa macho kwa kila mwanamuziki, hakuweza kumtambua kabisa mwanawe akaamua kuondoka.
Hamza Kalala anasema kabla ya kukutana na baba yake ili kujieleza juu ya suala hilo, bendi yao ilipata safari ya kwenda Nairobi nchini Kenya.
Kalala akatoroka akifuatana na Bendi ya Villa Negro Successes.
Aliporudi alimfungashia baba yake zawadi ya fulana ya kisasa wakati huo, na kumueleza wazi kuwa alikuwa Nairobi, kimuziki na ndiyo kazi anayofanya kwa wakati huo.
“Baba aliipenda sana zawadi niliyomletea, alinisifia kwa kujiheshimu kipindi chote kiasi cha yeye kushindwa kubaini kuwa mimi ni mwanamuziki.
“Akanitaka niendelee kuwa na heshima katika kazi yangu hiyo,” anasema Kalala.
Kalala anakumbuka fedha ya kwanza kulipwa katika muziki zilikuwa ni shilingi saba kwa mwezi.
Kwa kuwa hakuwa na ‘Viwalo’ vya kutosha, pesa yote aliimaliza kwa kununua nguo, kama suruali aina ya pekosi, viatu vya raizoni na Itali vilivyokuwa vimechongoka mbele kama mkuki na mashati ya slimu fit yaliyokuwa yanashika mwili.
Kalala anakumbuka jinsi alivyokuwa anapata tabu kutoka kwa kina dada ambao walikuwa wanampapatikia kutokana na unadhifu wake. Kuna kipindi alilazimika kujificha ili kuepuka usumbufu.
Villa Negro Successes ilisambaratika kutokana wanamuziki kugombania fedha, baadhi walisema hawalipwi vizuri. “Wakongo wengi wana miili mikubwa siku hiyo walipigana sana, sikuthubutu kuingilia ugomvi wao. Baada ya hapo bendi ilikufa kutokana na baadhi yao kuamua kurundi kwao Kongo usiku huo huo.”
Mwaka 1969 Hamza Kalala aliachana na bendi hiyo, akaamua kwenda mkoani Morogoro, akiwa na nia ya kujiunga katika Bendi ya Morogoro Jazz au Cuban Marimba.
Lakini alibadili uamuzi huo akaelekea Kilosa ambako alikuwa akijua kuwa Mwanamuziki Abel Balthazar yuko kule.
Alipofika akaambiwa kuwa Balthazar alisharejea Dar es Salaam.
Kwakuwa hakuwa na pesa mfukoni, akalazimika kuomba kazi ya kupiga gitaa katika bendi iliyokuwepo hapo Kilosa.
Kalala alipiga muziki hapo mjini Kilosa kwa kipindi kifupi, akaamua kuondoka kwakuwa hakuona ushindani katika bendi hiyo.
Komandoo akarudi kwao Tanga, ambako alikutana mwanamuziki mwenzake, wakapanga safari ya kwenda Morogoro.
Walifika katika mji huo wakiwa na hali mbaya sana kifedha. Kalala wakati huo alikuwa akivuta sigara, hivyo alijikuta amefika mjini Morogoro akiwa na senti 15, ambazo zisinge tosha kununua chochote.
Mwenzake aliyekuwa naye hakuwa mvutaji, alikuwa na akiba ya senti 50, zilizowawezesha kupata kifungua kinywa.
Kwa kuwa hawakuwa na sehemu ya kulala mjini humo, Kalala na mwenzake wakaenda kujihifadhi kwenye stendi ya mabasi, wakalala hadi asubuhi.
Kulipokucha wakaanza kuzitafuta ofisi za klabu za bendi hizo za Morogoro Jazz na Cuban Marimba. Bahati haikuwa upande wao kwani waliambiwa bendi hizo ziko safari nje ya Morogoro.
Bendi ya Cuban Marimba ilikuwa Songea (Ruvuma) wakati wanamuziki wa Morogoro Jazz walikuwa wameenda Zanzibar.
Lakini kwa bahati nzuri alibakia mwanamuziki mmoja wa Cuban Marimba, mpiga gitaa la solo anaitwa Waziri Nyange, wakaelekezwa alipo. “Tulipofika nyumbani kwake alitupokea, tukajieleza sisi ni mgeni tumetoka Tanga, tumekuja kwa ajili ya kutafuta bendi ya kupigia muziki.
“Nyange akatukaribisha na kutuambia tutaishi kwake, hadi bendi itakaporudi,” alisema Kalala.
Baada ya wiki moja bendi ya kwanza kurudi ilikuwa ni Morogoro Jazz.
Mbaraka Mwinshehe alimwita Kalala ambaye alikuwa na taarifa ya uwapo wake kwenda kufanyiwa usaili, ambapo aliambiwa apige gitaa wimbo wa ‘Sina pesa miye.’
Komandoo Kalala au Kapesula alifanya ‘kufuru’ kwa kulicharaza gitaa hilo kwa umahiri mkubwa, mara moja akachukuliwa katika bendi hiyo.
Hamza Kalala anasema aliporudi Juma Kilaza, aliyekuwa kiongozi wa Cuban Marimba, hali ikawa tofauti. Kilaza alimwita na kumueleza kwa nini amejiunga na bendi ya Moro Jazz wakati alipokelewa na Waziri Nyange ambaye ni mtu wao?
Kulingana na ukweli alioambiwa ikabidi aondoke Moro Jazz na kujiunga na Cuban Marimba.
“Kilaza alikuwa mbabe kidogo, hivyo alikuja kunichukua kwa nguvu Moro Jazz na mimi sikuwa na budi kukubali, kutokana na ukweli walioniambia na hadi wakati huo nilikuwa naishi kwa Nyange,” alisema Kalala.
Anaendelea kusimulia kuwa, licha ya kukubali kujiunga na Cuban Marimba kutokana na hisani aliyofanyiwa na Nyange, alikuwa anatamani sana kubaki Moro Jazz, kutokana na ucheshi wa Mbaraka Mwishehe na unadhifu waliokuwa nao wanamuziki wa Moro Jazz ukilinganisha na Cuban Marimba.
Kalala anakumbuka kama kulikuwa na bendi zina upinzani wa kweli wa muziki, ilikuwa ni hizo mbili, zilikuwa zinashindana na kupiga muziki wa kweli.
Alizitaja nyimbo za majibizano zilizokuwa zinaonyesha upinzani wao ni ule wa Moro Jazz, uliokuwa unaitwa ‘Moto wako washa nje hapa maji yatazima’, na Cuban wakawa na mtindo kila baada ya kumaliza wimbo wanasema ‘Dawa ya moto ni moto siyo maji’, ikiwa ni kama kuwajibu Moro.
Alivyoiacha Cuban Marimba
Siku moja usiku alikuja Katibu wa Chama wa Wilaya ya Bagamoyo aliyekuwa akijulikana kwa jina la Mwita, alikuwa ametumwa na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo (wakati huo), Mosses Nnauye kwenda kumchukua Waziri Nyange, aende naye Bagamoyo kuendesha bendi ya Vijana ya Tanzania Youth League (TYL).
Nyange alikuwa na familia yake pale Morogoro, hivyo ilimuwia vigumu kwenda Bagamoyo.
Nyange akampasia pande Hamza Kalala kwenda Bagamoyo, akaanza kazi kupiga muziki ambako kila Jumamosi walikuwa wakienda Ruvu kuwaburudisha wapigania Uhuru wa chama cha FRELIMO cha Msumbiji.
Kalala anasema Mwaka 1970, akasikia fununu kuwa Bendi ya Vijana Jazz inaanzishwa.
Kabla hakwenda kuomba kazi, alifuatwa na mwanamuziki aliyemtaja kwa jina la Ndala Fasutine.
Alipofika mbele ya uongozi wa Vijana, alioneshwa vyombo vya muziki, lakini akaambiwa hakukuwa na mpango wa kuanzisha bendi.
Kalala akafikiria jinsi ya kuishi jijini Dar es Salaam, ndipo akamfuata John Ondolo Chacha aliyekuwa Ofisa Uhusiano wakati huo.
Ondolo alimueleza kwamba vyombo hivyo vimefungiwa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana baada ya kuvunjwa kwa bendi ya Green Jazz na kwamba hivi sasa hapana mpango wa kuanzisha tena bendi.
Ofisa huyo akamuuliza anapiga chombo gani akamweleza kuwa anapiga gitaa.
John Ondoro aingia, ataka akamsikilize
Kalala alikubali akapiga nyimbo zake kama usaili, baadaye Chacha akaridhika na kuwapa pesa za chakula.
Kalala alipelekwa Kinondoni, Mango Garden akaanza kufanya mazoezi ya kupiga muziki, akishirikiana na wanamuziki wengine waliongezeka wakiwa katika kambi kama ya jeshi.
Wanamuziki hao walikuwa kina Ramadhan Mtoro aliyekuwa akipiga drums, Abdallah Kwesa na Hassan Hokororo.
Bahati nyingine ikatokea baada ya Katibu Mkuu wa Chama, Michael Baruti alikuwa akipita, akawakuta wakipiga muziki akawapenda sana.
Wakati wa maadalizi ya maadhimisho ya miaka Kumi ya Uhuru, Ondoro alienda kwenye shirika la mazao wakati huo.
Aliwashawishi kwamba wanayo bendi ambayo inaweza kuburudisha kwenye banda lao.
Baada ya kuwashawishi, makubaliano yalikuwaje? Itaendelea kesho