Kocha Zanzibar apangua kikosi akiivaa Tanzania Bara

Muktasari:

Zanzibar walishika nafasi ya pili katika mashindano ya Chalenji yaliyofanyika mwaka 2017 huko Kenya baada ya kufungwa na wenyeji kwa mikwaju ya penati 3-2 katika mchezo wa fainali uliokwisha kwa sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 90.

Kampala, Uganda. Benchi la ufundi la timu ya Taifa ya Zanzibar 'Zanzibar Heroes' limefanya mabadiliko ya wachezaji watatu katika kikosi chake cha kwanza kabla ya kuwavaa ndugu zao Tanzania Bara katika mashindano ya Chalenji huku likionekana kuendelea kutumia mfumo wa 4-2-3-1 kama ilivyokuwa dhidi ya Sudan.

Baada ya kutocheza katika mchezo uliopita wachezaji Kassim Khamis, Issah Haidar na Haruna Abdallah 'Boban' leo wamepata nafasi ya kuanza katika mechi hiyo iliyoshikilia hatma ya kila timu kwenye Kundi B.

Mshambuliaji wa Azam FC, Kassim Khamis amepata nafasi ya kuanza kuziba nafasi ya Ibrahim Ilika ambaye anatumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata katika mchezo dhidi ya Sudan.

Katika mabadiliko hayo yaliyofanywa na benchi la ufundi la Zanzibar chini ya kocha Hemed Morocco, beki wa kulia, Ame Abubakar 'Luiz' leo ataanzia benchi kumpisha Issah Haidar 'Dau' wakati Haruna Boban ataanza badala ya Awesu Awesu.

Kuingia kwa beki wa kati Issah Haidar anayecheza nafasi ya beki wa kati, kutamlazimisha Ali Ali kucheza nafasi ya beki wa kulia ambayo katika mchezo dhidi ya Sudan, alicheza Abubakar Ame 'Luiz'

Kikosi kamili cha Zanzibar Heroes kinachoanza leo ni Ahmed Suleiman, Ali Ali, Haji Mwinyi, Issa Haidar, Abdallah Kheri, Abdulaziz Makame, Haruna Abdallah, Mudathir Yahya, Kassim Khamis, Feisal Salum 'Fei Toto' na Mohamed Issah 'Banka'.