Kocha Singida na matumaini kusalia Ligi Kuu, amfungia kazi Kyombo

Muktasari:

  • Ngawina aliyekuwa kocha msaidizi, kwa sasa anakaimu nafasi ya Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ aliyeng’atuka kikosini kwa madai ya kushindwana na mabosi wa timu hiyo katika ishu ya maslahi.

BAADA ya kuiongoza kwa mara ya kwanza na kuipa ushindi Singida Fountain Gate, kocha wa timu hiyo, Ngawina Ngawina amesema kwa sasa hesabu ni kuibakiza Ligi Kuu, huku akichora ramani ya mechi tano zilizobaki akimpa tano Habibu Kyombo.

Ngawina aliyekuwa kocha msaidizi, kwa sasa anakaimu nafasi ya Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ aliyeng’atuka kikosini kwa madai ya kushindwana na mabosi wa timu hiyo katika ishu ya maslahi.

Juzi kocha huyo akiiongoza kwa mara ya kwanza walipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji na kupanda hadi nafasi ya tisa kwa pointi 29 wakiweka hai matumaini ya kubaki salama msimu ujao.

Timu hiyo ambayo imeweka makazi yake jijini hapa imebakiza michezo mitano ikiwa ni dhidi ya Coastal Union, KMC, JKT Tanzania, Geita Gold na Kagera Sugar.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ngawina amesema ushindi huo umeweka matumaini akiwataka wachezaji wake kutobweteka kwani kazi haijaisha.

Amesema baada ya kupitia kipindi kigumu cha kusota na matokeo yasiyoridhisha kimewavurugia mipango, hivyo kwa sasa wanapambania kukwepa kushuka daraja akivutiwa kasi ya Kyombo.

“Tulikuwa na presha kubwa, lakini vijana walionesha uwezo wao, tunaenda kujipanga upya na mechi zilizobaki na hesabu zetu ni kukwepa aibu ya kushuka daraja,” amesema.

“Kyombo ni suala la muda tu, kimsingi tunaendelea kumjenga kiushindani ili kila mechi zilizobaki aweze kuendeleza kasi yake ya mabao, malengo ya timu ni makubwa,” amesema kocha huyo.