Kocha: Simba, Yanga 3-0 uhakika Kwa Mkapa!

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Hayo yamesemwa na kocha wa Singida Fountain Gate, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alipozungumza na Mwanaspoti akisema timu hizo zina nafasi ya kufanya vizuri katika mechi hizo mbili za nyumbani kwa kila timu kupata ushindi kuanzia mabao 3-0 ikianzia Simba mbele ya Al Ahly kesho Ijumaa.

Wakati ikisalia siku moja kabla ya Simba na Yanga kuanza kushuka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mechi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, timu hizo zimetakiwa kumaliza mechi zao kwa kushinda si chini ya mabao 3-0 nyumbani kwani jambo hilo litazipa nafasi kubwa zaidi ya kutinga nusu fainali.

Hayo yamesemwa na kocha wa Singida Fountain Gate, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alipozungumza na Mwanaspoti akisema timu hizo zina nafasi ya kufanya vizuri katika mechi hizo mbili za nyumbani kwa kila timu kupata ushindi kuanzia mabao 3-0 ikianzia Simba mbele ya Al Ahly kesho Ijumaa.

Julio alisema Simba inatakiwa kuachana na dhana kwamba imeizoea Al Ahly kwa sababu imekutana nayo sana na badala yake iingie na akili ya kuwalazimisha Waarabu hao kufanya makosa ili ipate ushindi mkubwa ambao utaipa nafasi ya kuufanya mchezo wa marudiano kuwa rahisi Ijumaa ijayo Aprili 5 jijini Cairo, Misri.

“Simba kwanza iachane na dhana kwamba imeizoea Al Ahly kwa vile imekutana nayo mara nyingi, Al Ahly ikifika maeneo haya huwa ni timu tofauti kabisa na vile inavyocheza hatua za nyuma kabla ya hatua hii,” alisema Julio ambaye ni beki na kocha wa zamani wa Simba.

“Simba inatakiwa kutafuta ushindi mkubwa hapa nyumbani ipate hata mabao matatu, ushindi kama huo ukipatikana utawapa wepesi kwenye mechi ya marudiano maana kule lazima mchezo uwe mgumu zaidi kwani Ahly wanajua kwamba mechi watakwenda kuimalizia kwao.”

Akiizungumzia Yanga, Julio alisema Wananchi wana uwezo wa kuwashangaza Mamelodi na kwamba endapo wataupiga mpira mwingi kama ule uliowapa ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria, itawamaliza kirahisi Wasauzi hao.

Julio alisema Yanga ina kikosi bora chenye kucheza soka la kuvutia la kutafuta matokeo na hatua muhimu kwao ni kupata ushindi mkubwa pale Benjamin Mkapa ili kujiweka sawa na mechi ya marudiano.

“Yanga ina kikosi imara sana, inacheza soka la kuvutia mimi nasema Yanga ikicheza kama ilivyocheza na Belouizdad itapata ushindi mkubwa, inatakiwa kurudia kucheza kwa kiwango kile mbele ya Mamelodi,” alisema Julio na kuongeza;

“Yanga hii naweza kuifananisha na ile Simba ya kina Luis Miquissone na Clatous Chama kabla ya kuuzwa mara ya kwanza, muunganiko wa wachezaji wao ni silaha kubwa mbele ya Mamelodi, ila wanatakiwa kushinda kwa ushindi mzuri ili msingi wa kufuzu kwao uanzie kwa matokeo mazuri ya kucheza nyumbani.”