Kocha Serengeti Boys freshi tu

WENYEJI wa Fainali za Afrika kwa Vijana U17, Serengeti Boys ya Tanzania imeanza vizuri michuano ya kusaka wawakilishi wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kwa fainali hizo za 2019, huku kocha mkuu wake, Oscar Milambo akichekelea.
Serengeti iliichapa Burundi kwa mabao 2-1 na Kocha Milambo amesema ushindi huo umetoa taswira ya kikosi chake kilivyo kuelekea kwenye ushiriki wa fainali hizo za U17 mwakani.
“Tumeanza vizuri kwa ushindi, naamini kabisa hatutawaangusha Watanzania kwani najua wapo nasi, kikubwa ni kufanya vizuri hadi fainali zenyewe zitakapofika mwakani hapa nchini,” alisema.
Wakati huo huo Kocha wa Burundi, Rwasamanzi Yves, amesema katika michuano hiyo ya kusaka mwakilishi wa Cecafa anawahofia wenyeji kutokana na rekodi yao ya ubingwa.
“Unajua hii timu ndio mabingwa kwa miaka miwili mfululizo wa Cecafa, hivyo unapocheza nao lazima uwe mwangalifu, timu nyingine ni nzuri, ila tuliihofia zaidi Tanzania na wametulaza pamoja na kufanya jitihada kubwa,” alisema.