Kocha Migne aitwa Dar fasta

Muktasari:

KWA mujibu wa Yanga, kabla timu hiyo haijakanyaga uwanjani kwenye mechi yoyote ile ya kimashindano lazima Kocha Mkuu ambaye ni raia wa kigeni awe kambini pale Kigamboni.

KWA mujibu wa Yanga, kabla timu hiyo haijakanyaga uwanjani kwenye mechi yoyote ile ya kimashindano lazima Kocha Mkuu ambaye ni raia wa kigeni awe kambini pale Kigamboni.

Ingawa wanafichaficha lakini Mwanaspoti limejiridhisha kwamba Yanga imemalizana Mfaransa Sebastian Migne baada ya kushindwa na Hubert Velud ambaye awali alikuwa chaguo lao la kwanza lakini akazingua.

Mwanaspoti ambalo limetimiza miaka 20 sokoni, limejiridhisha pia kwamba Yanga wameachana na Velud kwavile alitaka mshahara wa zaidi ya Sh50 milioni na mambo mengine ambayo yako juu ya bajeti na uhalisia wa uchumi wa klabu hiyo ya wananchi.

Mshauri wa Uongozi wa Yanga, Senzo Mazingisa ameliambia Mwanaspoti mambo manne yaliyozaa uamuzi huo wa kumleta Kocha nchini kwa haraka.

Senzo ambaye ni Msauzi, alifafanua kwamba sababu ya kwanza iliyowafanya kufikiria upya uamuzi huo wa kutaka Kocha mpya aanze msimu ujao ni kwamba wamegundua kwamba bado wana nafasi ya kuchukua ubingwa wa ligi lakini pia hata Kombe la FA na kocha huyo atawaletea mzuka mpya.

Hata hivyo, Senzo akasema nafasi ya kocha wao Juma Mwambusi itabaki palepale kuhakikisha anamsaidia kocha atakayekuja kutokana na mzawa huyo kuijua vyema timu hiyo akianza nayo mwanzo wa msimu.

“Tumeona ni lazima tupate kocha mpya haraka na mchakato ulikuwa unaendelea na sasa tupo katika hatua ya mwisho kabisa, tunataka kuhakikisha kabla ya timu haijarejea uwanjani tuwe tayari ameshakuja,” alisema Senzo licha ya kutotaka kumtaja jina.

“Tunaona kuna nafasi kubwa tu ya kuwa bingwa msimu huu bila kujali tulivyoteleza hapa kati, huu ni upepo tu na umepita hatua muhimu ni kuinuka na kuendelea na safari kwa umakini.

“Siyo hatumuamini Mwambusi, tunaheshimu kazi kubwa anayofanya sasa na hata kabla kocha Mwambusi lakini tunataka kumuongezea mtu ambaye atasaidiana naye kuweza kufikia malengo yetu.

“Hata kocha atakayekuja tutataka afanye kazi na Mwambusi ili aweze kumsaidia kujua historia ya kikosi na hata aina ya ligi ya hapa hataweza kufanikiwa bila kuwa na msaada wa aina ya Mwambusi,” alisema Senzo ambaye aliwahi kupata mafanikio makubwa na Simba kama Ofisa Mtendaji Mkuu.

Aliongeza kuwa sababu ya pili ni kurudisha usiriazi kwa wachezaji wa timu hiyo ambao wanajua akija kocha mpya kila mtu atapambana kutafuta nafasi hali ambayo itarudisha ushindani wa namba.

Sababu yake ya tatu ni kuwarudisha uwanjani mashabiki wao ambao wataamini kuna mabadiliko makubwa huku akisisitiza kwamba kocha anayekuja atakuwa na ubora wa kubadilisha upepo kwa haraka.

“Wachezaji siku zote wakisikia kuna kocha mpya amekuja kila mtu utaona amebadilika atataka kutafuta nafasi, hii italeta ushindani, itasaidia timu sana lakini pia kuna mashabiki wetu ambao wapo ambao baadhi wamekata tamaa, hawapaswi kuwa hivyo, tunataka wajue bado tuko vitani na huo ndio ukweli, wakiona kuna kocha mpya watarudisha nguvu ya kuja kuipa nguvu timu yao.”

Sababu nyingine ya Senzo ni hatma ya mashindano ya Kimataifa kwa msimu ujao ambapo wanataka kocha huyo aje haraka ili aweze kuisoma timu inahitaji kipi katika kukiboresha kabla ya mashindano hayo.

“Kama kocha atakuja baadaye atakosa kujua kipi kinahitajika kwenye timu yake lakini akija sasa atapata muda wa kujua ni aina gani ya usajili tutahitaji,” aliongeza.

Kocha Migne aliifikisha Harambee Stars AFCON.