Kocha Kitayosce apania usajili Ligi Kuu

Muktasari:

  • Mkanwa alikabidhiwa timu hiyo mzunguko wa pili akichukua mikoba ya mtangulizi wake, Ahmed Soliman raia wa Misri, ambapo amefanikiwa kuipandisha daraja na msimu ujao itakiwasha ligi kuu.

KOCHA mkuu wa Kitayosce, Henry Mkanwa amesema hatakurupuka kwenye usajili isipokuwa atakuwa makini kutafuta watu wa kazi watakaoiwezesha kukaa ligi kuu muda mrefu, huku akichekelea rekodi yake.

Mkanwa alikabidhiwa timu hiyo mzunguko wa pili akichukua mikoba ya mtangulizi wake, Ahmed Soliman raia wa Misri, ambapo amefanikiwa kuipandisha daraja na msimu ujao itakiwasha ligi kuu.

Kocha huyo anafikisha timu nne kupandisha ligi kuu alipoanza na Polisi Dodoma (kwa sasa Dodoma Jiji), Polisi Moro (kwa sasa Polisi Mara (Biashara United) na sasa anaipandisha Kitayosce.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo alisema tayari wamevunja kambi wakiendelea na mapumziko huku akiwa tayari amekabidhi ripoti kwa viongozi kwa mastaa anaowataka msimu ujao.

Alisema katika usajili wake hatakurupuka bali atakuwa makini kuangalia ni nani awe naye msimu ujao na kwamba anachotaka ni kuona Kitayosce inadumu ligi kuu na siyo kwenda msimu mmoja na kurudi championship.

“Bahati nzuri nimecheza soka la ushindani kwa miaka 14, wachezaji wote hapa Tanzania nawajua, hivyo siwezi kutenga muda kumfuatilia mmoja mmoja muda ukifika nitajua nani niende naye,”

“Najivunia kuendeleza heshima na rekodi yangu kupandisha timu ligi kuu, lazima makocha wazawa tupewe heshima siyo kila muda wanakumbatiwa wale wa kigeni,” alisema Mkanwa.

Nyota huyo aliyezichezea Reli FC na Polisi Moro hadi kutundika daruga mwaka 2004, aliongeza kuwa atatumia vyema uwezo na uzoefu alionao kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri ligi kuu msimu ujao.