Kocha KenGold amshtukia Morisson, Yondani naye ndani

Muktasari:
- Morrison aliwahi kuzitumikia Yanga na Simba kwa misimu tofauti na sasa anaungana na KenGold huku wengi wakisubiri kuona utukutu kama atadumu kikosini humo.
Wakati staa wa zamani wa Yanga na Simba, Bernard Morrison akitua KenGold, benchi la ufundi la timu hiyo limeandaa programu maalumu kwa nyota huyo raia wa Ghana.
Pia limesema kabla ya kumsainisha tayari walishazungumza naye kumpa masharti ya timu hiyo na matarajio yao ni kuona anawapa kitu cha maana ndani ya uwanja.
Morrison asiyeishiwa vituko ndani na nje ya uwanja, amesaini mkataba wa miezi sita kuitumikia timu hiyo iliyopo mkiani mwa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi sita.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Omary Kapilima amesema utukutu wa nyota huyo, hautakuwa na athari yoyote kwani ameingia mazingira tofauti na aliyokuwapo awali ya Yanga na Simba.
Amesema mbali na staa huyo, timu hiyo imesheheni nyota kadhaa wakiwamo wa kigeni kutoka Zambia na DR Congo na nyota wengine wenye uwezo na uzoefu akiwamo beki Kelvin Yondani.
"Tulishazungumza naye kumpa masharti yetu tukakubaliana naye, tunajua uwezo na uzoefu alionao utatupa kitu duru la pili kuona tunaondoka mkiani,"
"Hayuko peke yake, wapo mastaa wengine kutoka Zambia na DR Congo na waliocheza timu kubwa hapa nchini kama Yondani, hivyo tunaenda kuanza upya Ligi" amesema Kapilima.
Kocha huyo ameongeza licha ya ratiba kusogezwa hadi Machi 1, kwao ni faida kwani watapata muda kutengeneza timu kutokana na maingizo mapya akisisitiza wachezaji wote kurejea kambini Januari 3.
Amesema matokeo waliyopata duru la kwanza si rafiki kwao hivyo matarajio yao ni KenGold mpya yenye soka la ushindani na ushindi kila mechi.
"Mashabiki watarajie makubwa, tunasuka timu mpya yenye soka bora na la ushindani kuhakikisha tunabaki salama Ligi Kuu, miezi miwili hii itakuwa ya faida sana kwetu," amesema Kocha huyo.