Kocha Geita aikubali Stand United

Muktasari:
- Katika mchezo wa leo, Chama la Wana imeichapa Geita Gold mabao 2-0, wafungaji ni Yusuph Adam dakika ya 14 na Omary Rajab dakika ya 85.
Kocha wa Geita Gold FC, Mohamed Muya amewapongeza vijana wake na wa Stand United, huku akisema mikakati yake ya sasa ni kurekebisha makosa yaliyojitokeza katika kikosi chao.
Muya ameyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari leo Mei 29, 2025 baada ya kumalizika kwa mechi ya marudiano ya play off kuwania kupanda Ligi Kuu Bara msimu ujao iliyochezwa Uwanja wa CCM Kambarage uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga
Katika mchezo huo, Stand United imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Geita Gold na kuifanya kushinda kwa jumla ya mabao 4-2 baada ya mchezo wa kwanza kumalizika kwa sare ya 2-2.
“Vijana wamepambana kadri ya tulivyowafundisha lakini bahati haikuwa upande wetu, tumepoteza mchezo na wenzetu wamefanikiwa kukutana na play off nyingine, tumepata nafasi lakini hatukuzitendea haki," amesema Muya.
Naye Kocha wa Stand United, Juma Masoud amesema katika kipindi hiki wanachosubiri play off ya mwisho dhidi ya timu kutoka Ligi Kuu, watakuwa wakifanya mazoezi na kucheza mechi za kirafiki,
“Kabla ya kukutana na atakayefungwa play off ya Ligi Kuu, kwanza timu itaenda mapumziko ya wiki moja baada ya hapo tutakuwa na mechi za kirafiki huku tukisubiri kucheza play off inayokuja,” amesema Masoud.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro amesema kuwa Serikali ya Shinyanga iko tayari kufanya juhudi zote katika kuiwezesha Stand United kurejea Ligi Kuu Bara.
“Timu tutakayocheza nayo play off ijayo ijipange kwa sababu Stand tunaenda kucheza Ligi Kuu, tuna imani timu yetu itaenda mbali,” amesema Mtatiro.