Kocha Dodoma Jiji aihofia Mbeya City

WAKATI Dodoma Jiji ikiikabili Mbeya City leo jioni kocha wa kikosi hicho Mbwana Makata amesema ataingia kwa tahadhari kubwa katika mchezo huo kwani wapinzani wao wameonekana kuimarika kwa siku za karibuni.
Dodoma Jiji itakuwa ugenini leo kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya kucheza na Mbeya City ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Kiwango cha Mbeya City katika mechi tano zilizopita ndicho kimeshtua Makata ambaye amewaambia wachezaji wake wanatakiwa kuwa waangalifu leo ili kuhakikisha wanavuna pointi tatu na kuisogelea nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi.


Makata alisema Mbeya City amebadilika sana katika raundi ya pili hivyo hawatawakabili kizembe lakini kutokana na ubora wa kikosi chake anaamini ataibuka na ushindi.
"Ni mechi muhimu kushinda ili tuzidi kubaki nafasi za juu kwenye msimamo. Hivyo tunatakiwa kuendelea kupambana sana katika mechi zetu kuhakikisha tunaingia nne bora.
"Tunakutana na Mbeya City ambayo raundi  hii ya pili wamebadilka sana kwani  katika mechi tano, wamepoteza moja tu  na sare nne hivyo utaona ni jinsi gani wana mabadiliko makubwa kiuchezaji tofauti na mzunguko wa kwanza.
"Nilichokiona kutoka kwao kwenye ulinzi wako vizuri sana ila kwenye ushambuliaji bado hivyo tutahakikisha  tunajipanga vema ili kupata pointi tatu.tunatumia udhaifu huo kuweza kupata kile tunachokihitaji, "alisema Makata.
Makata alisema wachezaji wake wanajua umuhimu wa kushinda mchezo huo hivyo kazi kwao kujitoa uwanjani na kutimiza majukumu yao.
Dodoma Jiji imekwua na mwendelezo mzuri kwenye ligi kwani katika mechi nne zilizopita, imeshinda tatu na kutoka sare mchezo mmoja.