Kocha Coastal awatolea uvivu chipukizi
Muktasari:
- Lazaro ambaye enzi zake alizichezea Coastal Union, African sports za Tanga na Yanga ameonyesha wasiwasi kuhusu muendelezo wa viwango vya wachezaji chipukizi.
KAIMU kocha mkuu wa Coastal Union, Joseph Lazaro amewachana wachezaji wanaochipukia kwa timu za Ligi Kuu Bara kwa kusema wanatakiwa kujituma zaidi na zaidi kwa kuonyesha ubora wao badala ya kulewa sifa ambazo zimekuwa zikifanya wapotee mapema baada ya kuwika ndani ya msimu mmoja tu.
Lazaro ambaye enzi zake alizichezea Coastal Union, African sports za Tanga na Yanga ameonyesha wasiwasi kuhusu muendelezo wa viwango vya wachezaji chipukizi.
“Wachezaji wa zamani walikuwa na uwezo wa kuonyesha makali yao kwa zaidi ya miaka mitano, lakini leo tunashuhudia wachezaji wengi wakipotea ndani ya kipindi kifupi,” alisema Lazaro.
“Sasa ni wakati wa kuacha kutafuta sifa za haraka. Badala yake, weka pamba kwenye masikio yako. Usikose kujifunza kutoka kwa wale waliotangulia.”
Kocha huyo, alieleza namna wachezaji wa zamani walivyojiweka katika viwango vya juu kwa kukaza buti na kujitolea kwa muda mrefu.
“Nimekuwa nikiwaeleza vijana kuwa na nidhamu ya hali ya juu na kujitahidi zaidi katika mazoezi, kwa kufanya hayo hakuna kocha ambaye atakunyima nafasi,” aliongeza.
Miongoni mwa vijana ambao Lazaro amekuwa akifurahia mwenendo wao ni pamoja na Lameck Lawi ambaye kabla ya kupandishwa kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo, amekuwa mfano mzuri kwa wenzake hadi sasa na amekuwa nguzo muhimu kwao kiasi cha vigogo wa Ligi Kuu Bara kuanza kumtolea macho.