Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kocha Berkane aondoka na jina la staa huyu Simba

MUTALE Pict

Muktasari:

  • Berkane ilitwaa ubingwa huo wa CAF ikiifikia CS Sfaxien ya Tunisia, baada ya kubebwa na matokeo ya jumla ya mabao 3-1 kwa kushinda 2-0 nyumbani mjini Berkane, Morocco na kuikatili Simba iliyokuwa ikisaka taji la kwanza la michuano ya CAF tangu kuasisiwa kwa klabu hiyo mwaka 1936.

KOCHA wa RS Berkane, Moine Chaabani, amekiri pamoja na timu anayoinoa kubeba ubingwa wa tatu wa Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuzidi akili Simba ikiwa nyumbani kwa kulazimisha sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar, lakini kuna jina la mchezaji waliloondoka nalo.

Berkane ilitwaa ubingwa huo wa CAF ikiifikia CS Sfaxien ya Tunisia, baada ya kubebwa na matokeo ya jumla ya mabao 3-1 kwa kushinda 2-0 nyumbani mjini Berkane, Morocco na kuikatili Simba iliyokuwa ikisaka taji la kwanza la michuano ya CAF tangu kuasisiwa kwa klabu hiyo mwaka 1936.

Pamoja na kubeba taji hilo, kocha wa Berkane, Chaaban ameweka wazi namna kikosi kilivyovurugwa hasa kipindi cha kwanza na kiwango cha kiungo mshambuliaji wa Simba, Joshua Mutale ambaye alitajwa pia kuwa Mchezaji Bora wa Mechi hiyo ya fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyopigwa juzi, Jumapili  kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Chaabani alisema, Mutale aliwasumbua mno kwa kasi yake, uwezo wa kupenya, na maamuzi ya haraka  akidai kuwa alibadilisha kabisa ramani ya mechi tofauti kabisa na hesabu zake zilivyokuwa.

"Mutale alituvuruga sana. Tulijua Simba wana viungo wenye ubora, lakini tulivyokutana naye uwanjani, alitufanya tubadilishe hata muundo wa ulinzi wetu. Ni mchezaji mwenye akili ya haraka, ana maono na hutoka sehemu ya kati kwa spidi inayowatatiza mabeki. Kipindi cha kwanza tulikuwa hatuna jawabu kwake,” alisema Chaabani.

Mutale alicheza sambamba na Charles Jean Ahoua na Elie Mpanzu nyuma ya mshambuliaji wa mwisho Steven Mukwala, wakitengeneza safu iliyokuwa inasumbua sana ngome ya Berkane.

Simba ilitangulia kupata bao la kuongoza kupitia Mutale kabla ya RS Berkane kusawazisha kipindi cha pili kupitia Soumaila Sidibe.

Baada ya mechi, Mutale mwenyewe akiongea na Mwanaspoti alizungumza baada ya kuchaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi, akisema:

“Ninajivunia tuzo hii, lakini ukweli ni kwamba ingekuwa na maana zaidi kama tungeweza kubeba kombe. Tumepambana kama timu, tumepitia changamoto nyingi, lakini tuliamini. Tulianza kwa nguvu, tukapata bao mapema, lakini matokeo yalikwenda kinyume. Ni fursa ya kujifunza.”

“Kikubwa zaidi, namshukuru Mungu kwa kila hatua. Ni heshima kubwa kuchaguliwa kuwa mchezaji bora katika mechi kubwa kama hii. Bila wenzangu isingewezekana, walikuwa bega kwa bega nami kila dakika uwanjani,” aliongeza Chabaan.

Mutale pia aligusia hali ya mechi  baada ya kadi nyekundu ya Yusuf Kagoma dakika ya 50, akisema: "Tulibaki pungufu mapema sana kipindi cha pili. Hiyo ilibadilisha kabisa jinsi tulivyokuwa tumepanga kucheza. Lakini bado tulijituma, tulipambana hadi mwisho. Tuliamini kuwa tunaweza, na nina uhakika tumejifunza mengi ambayo yatatufanya kuwa bora zaidi msimu ujao.”

Nyota huyo wa Zambia alihitimisha kwa kutoa ujumbe kwa mashabiki: "Kwa mashabiki wetu, ahsanteni kwa sapoti yenu isiyoisha. Mmekuwa nasi kila hatua, kutoka mechi ya kwanza hadi hii ya mwisho. Tumeumia pamoja leo, lakini tutaamka na kurudi kwa nguvu zaidi. Hii ni Simba hatukati tamaa.”

Kocha Chaabani alihitimisha kwa kusema kuwa licha ya ushindi wa jumla ya mabao 3-1 mechi hiyo ilikuwa mgumu sana na ni kati ya fainali zenye ushindani mkali alizowahi kushuhudia.

Fainali hiyo imeacha hisia tofauti kwa mashabiki wa Simba, lakini kiwango cha Mutale kimeonekana kama nuru ya matumaini kwa kikosi cha kocha Fadlu Davids kuelekea mwishoni mwa msimu.