Kocha awapa dawa simba

Muktasari:

  • Kibadeni (pichani) anasema kiuhalisia Yanga hivi sasa ni timu bora zaidi ya Simba, lakini hilo haliwezi kutoa majibu ya moja kwa moja kwamba itakuwa mechi rahisi upande mmoja ila amewasisitiza Simba kuwa makini na mambo mawili.

Wengi wanasema Dabi ya Kariakoo huwa haina mwenyewe. Mkongwe, Abdallah Kibadeni ‘King Kibadeni’ ambaye ana rekodi ya hat trick katika dabi hiyo ya Jumamosi, naye ametia neno lake juu ya mchezo huo, huku akiwapa dawa ya ushindi Simba.

Kibadeni (pichani) anasema kiuhalisia Yanga hivi sasa ni timu bora zaidi ya Simba, lakini hilo haliwezi kutoa majibu ya moja kwa moja kwamba itakuwa mechi rahisi upande mmoja ila amewasisitiza Simba kuwa makini na mambo mawili.

Kwenye kiungo hana wasiwasi nako ila watumie akili za ziada kwenye ushambuliaji na kulinda.

“Kuna shida eneo la ushambuliaji, hata ulinzi pia hawapo vizuri, hivyo lazima warekebishe maeneo hayo ili kuwa bora zaidi kama wenzao Yanga kama wanataka kushinda mechi hii. Umakini kila dakika ni muhimu sana, hii ni dabi.”

“Timu zote nimekuwa nikizifuatilia namna zinavyocheza, nimeona Yanga wapo vizuri sana kuanzia safu yao ya ulinzi hadi ushambuliaji. Mechi zao wanavyocheza unaona kabisa kuna jambo fulani wanalitafuta na mwisho wa siku wanalipata.

“Chukulia mfano Yanga wamecheza mechi mbili dhidi ya Mamelodi katika michuano ya kimataifa bila ya wachezaji wao muhimu, lakini kila mmoja ameona nini kilitokea, ndiyo maana nasema Yanga wamekamilika, wana kikosi ambacho akikosekana mtu fulani, inakuwa kama vile hakijatokea kitu.

“Simba wameamua kuweka kambi Zanzibar kwa sababu kubwa ya kuhitaji utulivu, wameona wakiendelea kuwepo kule wanapokaa siku zote, hawatakuwa na utulivu wanaouhitaji kwani huko wanakuwa wenyewe tu, lakini wakikaa Dar, inakuwa rahisi kwa wachezaji kukutana na familia au hata rafiki zao wa karibu, kitu ambacho kinaweza kuwafanya wasiwe na utulivu.”

Kibadeni anayeshikilia rekodi ya kufunga hat trick iliyodumu miaka 47 sasa ambapo mwenyewe amesisitiza kwamba: “Kama kuna mtu anataka kuivunja rekodi yangu ya hat trick, basi lazima aje kuniomba.”

Kibadeni aliweka rekodi hiyo katika dabi iliyochezwa Julai 19, 1977 ambapo alifunga mabao matatu wakati Simba wakiibuka na ushindi wa mabao 6-0. Alifanya balaa hilo dakika ya 10, 42 na 89, huku mengine yakifungwa na Jumanne Hassan ‘Masimenti’ aliyefunga mawili dakika ya 60 na 73 na beki wa Yanga, Selemani Sanga alijifunga dakika ya 20.

“Unajua kwamba kila mmoja kinapofika kipindi kama hiki cha dabi huwa anazungumzia ile rekodi yangu ya hat trick kwani imekuwa na muda mrefu haijavunjwa, unajua kwa nini, kwa sababu hakuna aliyekuwa tayari kuivunja.

“Tunaweza kuona dabi yanafungwa mabao mengi kwenye mechi tofauti, kama ile iliyopita Yanga walishinda 5-1, kuna mchezaji alifunga mabao mawili (Maxi Nzengeli), lakini akashindwa kuifikia rekodi yangu.

“Sasa kama kuna mchezaji anataka kuivunja rekodi yake, aje aniombe, kama hakuna atakayefanya hivyo, basi hakuna kitu kitakachotokeo zaidi ya hapo,” alisema Kibadeni ambaye aliwahi kuikochi Simba kwa nyakati tofauti.

Alipoulizwa kwa nini mpaka waende kumuomba, Kibadeni alisema: “Mimi ndiye nina hiyo siri, siwezi kuisema sasa, hivyo waje tu waniombe, iwe mchezaji wa Simba au Yanga, siwezi kumkatalia.”


KAMBI YA ZANZIBAR

Katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa Machi 8, 2015, wakati Simba ikiwa inanolewa na Kocha Mkuu, Dylan Kerr, walishinda bao 1-0, mfungaji akiwa ni Emmanuel Okwi. Kabla ya mchezo huo, Simba iliweka kambi ya muda mfupi Zanzibar.

Baada ya hapo, mchezo wa Februari 25, 2017, wakashinda tena mabao 2-1 dhidi ya Yanga kwa mabao ya Laudit Mavugo na Shiza Kichuya, huku lile la Yanga mfungaji akiwa Simon Msuva. Hapa Simba waliweka kambi Zanzibar, timu ikiwa chini ya Kocha Joseph Omog.

Mwanzoni mwa msimu wa 2017/18 ambapo timu hizo zilikutana katika Ngao ya Jamii iliyochezwa Agosti 23, 2017. Dakika tisini za mchezo huo matokeo yalikuwa 0-0. Simba iliyokuwa ikinolewa na Joseph Omog, ikashinda kwa penalti 5-4.

Mara ya mwisho kwenda Zanzibar wakati wakijiandaa na mchezo wa Kariakoo Dabi, ilikuwa katika mechi ya Septemba 30, 2018, ikamalizika kwa matokeo 0-0.

Walivyojiandaa kucheza dhidi ya Al Ahly, licha ya kwamba hawakwenda na wachezaji wote kutokana na wengine kuwa na majukumu ya timu za taifa kipindi cha Kalenda ya FIFA, lakini Kocha Abdelhak Benchikha alisisitiza kwamba ameamua kuipeleka timu huko kutokana na kuhitaji utulivu zaidi.

Kwa sasa Simba inapitia wakati mgumu, mashabiki wa timu hiyo wamekuwa wakitoa vitisho kwamba kama timu ikiendelea kutopata matokeo mazuri, watalazimika kufanya jambo tofauti ikitafsiriwa ni kufanya vurugu.

Kwa upande wake, Uhuru Seleman Mwambungu ambaye aliwahi kuwa kiungo mshambuliaji wa Simba, alisema: “Dabi haijawahi kuwa rahisi kama wengi wanavyodhani, nimecheza na najua namna ilivyo na haiwezi kuzoeleka.

“Kutokana na hilo, viongozi huhitaji timu ifanye maandalizi katika eneo tulivu ambalo kutakuwa na usiri na wala hakuna kitu kingine cha ziada.”