Kocha AFC Leopards asaka nyota wa kuisuka upya

Muktasari:

Kwenye mechi hiyo, Ingwe walionyesha udhaifu mkubwa hasa kwenye safu ya kati, nafasi ambayo Mbungo anasema itakuwa ya kwanza yeye kulifanyia kazi msimu utakapomalizika.

BAADA ya kurefusha mkataba mpya wa kuifunza klabu ya AFC Leopards hivi majuzi, kocha Mrwanda Casa Mbungo sasa kaweka wazi kwamba atakuwa akiingia sokoni mara moja kufanya usajili zaidi.

Kichapo cha Jumapili cha magoli 3-1 dhidi ya Mashemejio Gor Mahia kimemfanya kocha Mbungo kutaka kurutubisha kikosi chake hata zaidi.

Kwenye mechi hiyo, Ingwe walionyesha udhaifu mkubwa hasa kwenye safu ya kati, nafasi ambayo Mbungo anasema itakuwa ya kwanza yeye kulifanyia kazi msimu utakapomalizika.

Katika Mashemeji Derby hiyo, kocha Mbungo alilazimika kumchezesha beki wa kati David ‘Cheche’ Ochieng, uamuzi anaosema uliiishia kuwakosti kwa sababu safu ya nyuma ilikosa uongozi kabisa.

Cheche ni mmoja wa wachezaji watatu aliowasajili kwenye dirisha dogo la msimu huu na amekuwa nguzo muhimu katika timu ya Ingwe akisaidia pakubwa kuyapindua matokeo mabovu ya timu hiyo.

Hata hivyo baada ya blanda kibao za difensi kwenye Mashemeji Derby, kocha Mbungo kasema atalazimika kumrejesha Cheche kwenye nafasi yake ya safu ya nyuma katika mechi zilizosalia.

“Nimekuwa nikimtumia kama kiungo mkabaji kwa sababu ya upungufu wa wachezaji nilionao kwenye safu hiyo. Wale wachezaji nilionao wa safu hiyo ni wachanga mno. Lakini baada ya mechi ya wikendi nitamrejesha kwenye safu yake aipendayo ya ulinzi hadi mwisho wa msimu nitakapoingia sokoni kusaka mchezaji mzuri wa kujaza nafasi hiyo” Mbungo amefunguka.

Hata hivyo huenda Mbungo pia akalazimika kumsaka beki mwingine wa kujaza nafasi yake Cheche endapo naye ataondoka.

Cheche alijunga na Ingwe katikati ya msimu kwa kusaini mkataba mfupi wa miezi sita. Lengo lake lilikuwa kuendelea kujiweka katika kiwango bora ya utimamu wa mwili wakati akiendelea kusaka klabu za majuu.

Hata hivyo kiwango chake kimeishia kumkosha kocha Mbungo ambaye tayari amewaomba  viongozi wa klabu kuingia kwenye mazungumzo naye na kujaribu kumshawishi aurefushe mkataba huo msimu ujao.