KMC yapata mdhamini mpya
KLABU ya KMC iliyoshiriki Ligi Kuu Bara, imekula shavu kwa kupata mdhamini mpya walioingia nao mkataba wa miaka miwili ya kusambaziwa vifaa vya timu yao.
KMC iliyomaliza nafasi ya tano katika Ligi Kuu iliyopita, imesaini mkataba huo ambao thamani yake haikuwekwa wazi na kampuni ya Masita Sports Wear ambayo hivi karibuni iliingia mktaba kama huo na Biashara United ya Mkoa wa Mara.
Makubaliano hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam leo Jumatano chini ya Kampuni ya Level Up inayoiwakilisha wadhamini hao kutoka Uholanzi ambayo inamiliki hati miliki ya kusambaza vifaa vya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Katibu Mkuu wa KMC, Walter Harrison alisema kwa ubora wa kampuni hiyo wanaamini hata ubora wao utaongezeka baada ya kufanya kazi kwa msimu uliopita kwa kiwango kikubwa.
Awali wakisaini mkataba huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Level Up, Daud Aboud amesema ni nafasi kubwa kwao kufanya kazi na klabu kama KMC na wana imani watashirikiana vizuri katika makubaliano hayo na hivyo kutimiza malengo ya kuhakikisha wanaleta vifaa bora.