KMC yajipanga kuiduwaza Simba

Muktasari:

Simba inaanza kucheza kiporo kesho na KMC ni mchezo muhimu kwao wakishinda wataendelea kubaki nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kuu Bara.

Dar es Salaam. Yanga ina faida ya pointi sita ambazo watani wao Simba walizidondosha kwenye mechi nne, wakitoka sare tatu na Ndanda, Wanajangwani na Lipuli, pamoja na kipigo cha Mbao FC.


Simba wapo nyuma ya michezo minne dhidi ya Yanga na Azam FC, kesho Jumatano wanacheza na KMC iliopo nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi kuu Bara, hesabu za kocha Patrick Aussems zitakuwa ni kupunguza gepu dhidi ya watani wake.


Katika mchezo wao wa kesho Simba wanatakiwa kupiga hesabu vyema ili kulinda nafasi ya tatu waliopo kwenye msimamo wa ligi, wakati KMC wana morali ya kuendeleza ushindi baada ya kuwafunga Prisons mabao 5-1 mchezo uliopita.


Nyota wa KMC, James Msuva alisema wamejipanga kuandika rekodi ya kuwafunga Simba katika mechi yao ya kesho.

"Tunahitaji kuendeleza ushindi ambao tuliuanza dhidi ya Prisons, tunajua Simba ina wachezaji wenye uwezo wa juu, lakini tupo tayari kwa ushindani," anasema Msuva.