KISA MAYELE...Mastaa Yanga waonywa

KISA MAYELE...Mastaa Yanga waonywa

PRESHA ya nyota wa Yanga, Fiston Mayele kutaka kufunga baada ya mechi tatu mfululizo bila bao kumetajwa kuichelewesha timu hiyo utangaza mapema ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, huku nyota wa timu hiyo wakionywa na kurudishwa kambini haraka leo kuendelea na mazoezini makali.

Sare ya juzi imepunguza gepu la pointi kwa Simba ambayo kama itashinda leo dhidi ya Kagera, itasalia na pointi nane ili kuifikia Yanga kwenye msimamo, wakati huo ikiombea timu hiyo ipoteze mechi tatu mfululizo huku wachezaji wa Yanga wakilaumiwa kwa kupoteza nafasi.

“Hii inaonyesha katika saikolojia ya wachezaji wa Yanga kuna kitu wanataka kumtengenezea Fiston Mayele, jambo ambalo kwa kipindi hiki ambacho wako kwenye vita ya ubingwa hawapaswi kuwa na fikra hizo itawagharimu,” alisema mchambuzi na nyota wa zamani wa timu hiyo, msomi Ally Mayay.

“Hata ilivyotokea penalti, Djuma Shaban angeweza kupiga kwani ana rekodi nzuri ya penalti, lakini Saido alichukua mpira na kumpa Mayele, ni kama wachezaji wanataka kumbusti Mayele kwenye ufungaji, hiyo ni sawa, lakini waangalie kwanza matokeo ya timu, vinginevyo itawagharimu,” alisema.


KOCHA KAGERA APIGA SIMU

Kocha Francis Baraza wa Kagera amekiri kwamba alipiga simu Yanga kumpa somo kijana wake, Denis Nkane. Alisema kwenye mechi kadhaa, Yanga wamepoteza pointi kwa kumuangalia Mayele na wachezaji kutaka kulazimisha mchezaji huyo afunge jambo ambalo halina afya kwa timu.

“Kufunga ni bahati, hakuna mchezaji ambaye anatoka nyumbani na kusema leo nakwenda kufunga, mfano ni Manchester United, Cristiano Ronaldo ni mfungaji bora wao, lakini ikitokea penalti anafunga Fernandes sababu ni mtaalamu wa kupiga penalti.

“Yanga wanachokifanya kipindi hiki ni kama wanamuangalia Mayele, kuna mechi kama si ya Ruvu Shooting basi ni ya Simba, Nkane alikuwa na nafasi ya kufunga lakini alimuangalia Mayele, kilichotokea walikosa pointi mbili, nakumbuka nilimpigia simu Nkane baada ya ile mechi nikamsema.

“Fei Toto pia juzi amepata nafasi ya wazi kabisa, ambayo angefunga, lakini akamuangalia Mayele, matokeo yake ni nini? wamepoteza pointi nyingine mbili, wamepata penalti, Djuma ndiye mfungaji wao wa penalti, lakini mpira anapewa Mayele, wamekosa pointi mbili tena, hii inawagharimu.

“Hata leo wakisema Mayele na Mpole kwenye timu zao wapewe penalti zote wapige wao, suala la mfungaji bora analifahamu mwenyezi Mungu, lakini Yanga wasipoondoa fikra hiyo na kutaka Mayele tu ndiye afunge itawagharimu,” alisema.