Kisa bao moja... Mastaa wataka Yacouba aanze

Wednesday October 13 2021
yacoub pic
By Olipa Assa

MASTAA wa zamani wa Yanga, Malimi Busungu na Said Bahanunzi wamesema kwa kile alichokionyesha straika wa timu hiyo, Yacouba Sogne msimu ulioisha, aliomaliza na mabao nane ni mtaji kuwa na mtu wa uhakika wa kufunga mabao.

Busungu alisema japokuwa mbele ya mashabiki linaonekana jina la Sogne kufifia badala yake wanaotamba ni Fiston Mayele na Heritier Makambo na Jesus Moloko(bao moja), alishauri staa huyo angaliwe kwa jicho makini.

Alisema alimuona Sogne kwenye mechi mbalimbali za msimu ulioisha na namna alivyoanza ligi kuu inayoendelea, alichokiona ana presha ya kutaka kuwaonyesha mashabiki kwamba bado anaweza, licha ya kuongezeka wageni kwenye nafasi yake.

“Najua Yanga ilivyo na presha, hivyo kama mchezaji hana mwanzo mzuri anaweza akawa kwenye nyakati ngumu ambazo kocha asipomjengea kujiamini anaweza akaondoka kwenye mstari,”alisema Busungu.

“Sogne kuendelea kuwepo na timu ni mtaji kwa Yanga ama kwa kocha kuwa na uhakika wa mtu wa kufunga kwasababu tayari anajua aina ya uchezaji wake na ameishayazoea mazingira ya ligi kwa ujumla,”alisema.

Hoja yake iliungwa mkono na Bahanunzi aliyesema mwanzo wa ligi unakuwa na presha kubwa, jambo linalozidi kumpa imani kwamba Sogne akipata utulivu atafunga mabao mengi na kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania kiatu cha dhahabu.

Advertisement

“Mshambuliaji yoyote asipofunga anakuwa na presha kubwa, mfano Meddie Kagere baada ya kufungua akaunti ya bao, nategemea atacheza kwa utulivu mkubwa, kwani tayari amepata ujasiri wa kupeleka mpira nyavuni,”alisema.

Kwa upande wa Oscar Joshua ambaye aliichezea timu hiyo nafasi ya ulinzi, alimzungumzia Mukoko Tonombe ”Binafsi bado namkubali Mukoko kwamba atafanya kitu, ikiwemo na Sogne,”alisema.

Mshambuliaji mkongwe wa kike, Asha Rashid ‘Mwalala’ alisema bado Sogne ni mchezaji hatari na hapaswi kubezwa.

Advertisement