Kipre anataka Ligi awamalize

Kipre anataka Ligi awamalize

KIUNGO mshambuliaji mpya wa Azam FC, Kipre Junior amesema kutokana na maandalizi mazuri aliyopata hadi sasa anajiona yuko fiti.

Kipre aliyesajiliwa msimu huu na kikosi hicho akitokea Sol FC ya kwao Ivory Coast alisema mchezo wa kirafiki dhidi ya Coastal Union walioshinda mabao 4-2 juzi huku yeye akifunga mawili umempa taswira halisi ya Ligi Kuu Bara.

“Nipo tayari kwa ajili ya kuipambania timu yangu, nimekaa na wenzangu kwa muda mchache lakini nashukuru nimeanza kuzoea mazingira haraka huku nikijivunia sapoti na ushirikiano mkubwa ninaoupata,” alisema Kipre.

Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Abdihamid Moallin alisema hawezi kutoa sifa kwa mchezaji mmoja bali anajivunia kiwango kizuri na jitihada wanazoendelea kuzionyesha kwenye michezo ya kirafiki ambayo wamecheza hadi sasa.

“Mchezo wetu na Zesco United utaimarisha kikosi changu kwa kuangalia upungufu uliopo kwani naamini ni kipimo sahihi hasa kwa wachezaji wa kigeni kwa sababu wanahitaji muda zaidi wa kuzoeana na wenzao,” alisema.

Azam itacheza na Zesco Jumapili hii kwenye Uwanja wa Azam Complex ikiwa ni mchezo maalumu wa kutoa fursa kwa mashabiki wao kuwaona wachezaji wapya huku tamasha hilo likibatizwa jina la ‘Azamka’ lililobeba mchanganyiko wa maneno mawili ya Azam na Amka.

Azam imebeba jina la timu na Amka ni hali ya kuinua ari na shangwe kwa mashabiki kama ilivyofafanuliwa na Ofisa Habari wa klabu hiyo Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’.

Mabingwa mara tisa wa Ligi Kuu ya Zambia, Zanaco hawajawahi kukutana na Azam kwenye mashindano rasmi lakini zimekutana mara tatu kirafiki.