Kipa Ihefu akubali yaishe, amsikilizia Maxime

ALIYEKUWA kipa namba moja wa Ihefu FC, Fikirini Bakari amekubali upinzani alioupata dhidi ya mwenzake kikosini, Khomein Aboubakari aliyesajiliwa dirisha dogo kutoka Geita Gold akisema analazimika sasa kuongeza juhudi binafsi katika kurejesha namba yake, huku akimsikilia kocha mkuu.

Kwa muda mrefu Fikirini aliyewahi kutamba na Coastal Union na KMC, alikuwa mhimili na panga pangua langoni katika kikosi hicho wakati Ihefu ikiwa chini ya Kocha Zuberi Katwila aliyeitema timu hiyo na kurejea Mtibwa Sugar, lakini kwa sasa kipa huyo mambo yameonekana kuwa tofauti.

Tangu alipokabidhiwa majukumu ya kuiongoza timu hiyo, Mecky Maxime ameonekana kumWamini zaidi kipa Khomein, huku akimpiga chini Fikirini anayefahamika zaidi kama Mapala.

Fikirini ameliambia Mwanaspoti anakubali upinzani alioupata, huku akiendelea kujifunza kwa mwenzake huyo, lakini akiongeza juhudi hasa kwenye mazoezi ili kumshawishi kocha Maxime.

Amesema kila kocha huwa na falsafa yake kutokana na aina ya mchezo, hivyo kuwekwa benchi kwa sasa haiwezi kumvuruga akili akiamini muda wake utafika tena na kuendeleza majukumu.

“Kila Kocha na mipango yake, lakini kwa mwenzangu najifunza kitu kwa sababu makipa tunatofautiana uwezo, nachofanya ni kuongeza nguvu na juhudi binafsi ili kutengeneza nafasi yangu,” amesema kipa huyo.

Fikirini ameongeza pamoja na timu hiyo kutokuwa na mwanzo mzuri, lakini kwa sasa yapo matumaini ya kufanya vizuri na kumaliza nafasi nzuri bila presha.

Amesema maandalizi waliyonayo kambini jijini Arusha yanawapa nguvu na matarajio makubwa ya kufanya vizuri na kila mchezaji kiu yake ni kuipa mafanikio timu.

“Sisi hatukuwa na mapumziko yoyote, hii ni kwa sababu ya mipango na malengo ya timu kuhakikisha tunasahihisha makosa yetu na kufanya vizuri, tunaamini tutabaki salama Ligi Kuu,” amesema kipa huyo.