Kilichoiangusha Tabora United hiki hapa

Muktasari:
- Timu hiyo inayofahamika kwa jina la utani la ‘Nyuki wa Tabora’, ilianza msimu vizuri lakini hadi sasa imekuwa na wakati mgumu wa kupata matokeo mazuri, japo kwa sasa inakabiliwa na changamoto kuu tatu zinazoifanya kuendelea kufanya vibaya.
KICHAPO cha bao 1-0, ilichokipata Tabora United dhidi ya KMC FC, Mei 14, 2025, kimeifanya timu hiyo kufikisha mechi sita mfululizo za Ligi Kuu bila ya ushindi, tangu mara ya mwisho ilipoifunga Dodoma Jiji FC 1-0, nyumbani, Februari 28, 2025.
Timu hiyo inayofahamika kwa jina la utani la ‘Nyuki wa Tabora’, ilianza msimu vizuri lakini hadi sasa imekuwa na wakati mgumu wa kupata matokeo mazuri, japo kwa sasa inakabiliwa na changamoto kuu tatu zinazoifanya kuendelea kufanya vibaya.
Changamoto hizo ni kwenye safu ya ushambuliaji na eneo la mabeki ambapo katika mechi 28 ilizocheza msimu huu imefunga mabao 27 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 39, ikishika nafasi ya tano na pointi 37.
Offen Chikola anayeongoza katika kikosi hicho kwa mabao akiwa amefunga saba, anakabiliwa na ukame tangu mara ya mwisho alipofunga moja kwenye kichapo cha kikosi hicho cha 2-1, ikiwa nyumbani dhidi ya maafande wa JKT Tanzania Machi 7, 2025.
Nyota wa zamani wa Yanga, Heritier Makambo amefunga mabao matano ya Ligi Kuu, ingawa hadi sasa ameshindwa kufunga, tangu mara ya mwisho alipofunga katika sare ya bao 1-1, kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi dhidi ya KenGold Februari 14, 2025.
Ukame wa nyota hao, umeifanya Tabora kuteseka hadi sasa ambapo katika mechi sita ilizocheza mfululizo bila ya ushindi wa Ligi Kuu Bara, imefunga bao moja tu lililokuwa la Offen Chikola dhidi ya maafande wa JKT Tanzania, huku ikiruhusu 13.
Sababu nyingine ya timu hiyo kufanya vibaya ni mabadiliko ya mara kwa mara ya benchi la ufundi, ambapo kikosi hicho hadi sasa kimeongozwa na makocha wanne tofauti, hali inayochangia kutokana na kila mmoja kuanza upya kuingiza falsafa zake.
Timu hii ilianza msimu na makocha raia wa Kenya, Francis Kimanzi na msaidizi wake, Yusuf Chippo, waliojiunga nayo Julai 31, 2024, japo, Oktoba 21, 2024, waliondoka kwa kile kilichoelezwa kufikia makubaliano ya pande mbili kati yao na klabu.
Makocha hao waliondoka baada ya kuiongoza mechi nane za Ligi Kuu Bara msimu huu, ambapo kati ya hizo walishinda mbili tu, sare pia mbili na kupoteza minne, wakikiacha kikosi hicho kikiwa katika nafasi ya 11, kwenye msimamo na pointi nane.
Novemba 2, 2024, uongozi wa Tabora United ulimtangaza Mkongomani, Anicet Kiazayidi kuchukua nafasi ya Kimanzi kumalizia msimu wa 2024-2025.
Hata hivyo, kocha huyo aliondoka Machi 28, 2025 kwa makubaliano ya pande mbili kati yake na klabu hiyo, huku nafasi yake akichukua Kocha, Mzimbabwe Genesis ‘Kaka’ Mangombe.
Anicet tangu ajiunge na kikosi hicho akichukua nafasi ya Francis Kimanzi aliyeondoka Oktoba 21, 2024 kwa makubalino ya pande mbili, aliiongoza Tabora United katika mechi 14 ya Ligi Kuu Bara, akishinda saba, sare mitano na kupoteza miwili.
Kiujumla, Anicet aliiacha timu hiyo ikiwa nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi 37, baada ya kucheza mechi 23, ikishinda 10, sare saba na kupoteza sita, huku ikifunga mabao 27 na kuruhusu 28.
Kwa upande wa Kocha, Mangombe aliyetambulishwa Machi 28, 2025, hakudumu katika kikosi hicho kwani aliondoka Aprili 18, 2025, kwa makubaliano ya pande mbili, huku akiiongoza jumla ya mechi nne za kimashindano na kushuhudia akipoteza zote.
Katika mechi hizo, Mangombe alianza kwa kutolewa na Kagera Sugar kwa kuchapwa kwa penalti 5-4, baada ya sare ya bao 1-1, dakika 90, hatua ya 16, bora ya Kombe la Shirikisho (FA), huku Ligi Kuu akichapwa na Yanga mabao 3-0, Aprili 2, 2025.
Baada ya hapo, Mangombe aliyechukua nafasi ya Mkongomani Anicet Kiazayidi, akachapwa tena bao 1-0, dhidi ya Pamba Jiji Aprili 5, huku mchezo wa mwisho ni wa kichapo kutoka kwa ‘Wazee wa Mapigo na Mwendo’, Mashujaa cha 3-0, Aprili 10, 2025.
Kitendo cha kuondoka Mangombe, kikaufanya uongozi wa kikosi hicho kumuajiri Kocha, Mzambia Simonda Kaunda hadi mwisho wa msimu huu, huku akiwahi kuzifundisha pia Nkana FC, Forest Rangers, Chambishi FC na Roan United FC zote za kwao Zambia.
Licha ya matarajio makubwa ya Tabora kwa Simonda ili kubadili upepo wa hali inayoendelea katika kikosi hicho, ila mambo bado yamekuwa ni magumu kwake, ambapo amekiongoza kwenye mechi mbili za Ligi Kuu Bara na zote ameshuhudia akipoteza dhidi ya Singida Black Stars 3-0 na 1-0 mbele ya KMC.
Timu hiyo imebakisha mechi mbili za kuhitimisha msimu huu, dhidi ya Azam ambapo duru la kwanza Tabora United ilishinda 2-1, kisha dhidi ya Coastal Union ambapo duru la kwanza zilitoka sare ya bao 1-1.
Akizungumzia kiwango cha timu hiyo, Kocha wa Tabora, Simonda Kaunda alisema hawezi kubadilisha hali iliyopo kwa haraka kutokana na kutokuwa na muda mrefu katika kikosi hicho, ingawa anafurahishwa sana na maendeleo ya mchezaji mmoja mmoja.
“Mwenendo wetu sio mzuri kwa sababu ya hali iliyopo ila ni suala la mchakato, unapopoteza mechi moja baada ya nyingine kwa hakika inashusha morali ya timu kiujumla, ingawa muda huu wa mapumziko tunaendelea kurekebisha changamoto zilizopo,” alisema kocha huyo.