Prime
Kombo: Tunataka zote 3
BEKI wa TRA United, Nasri Kombo amesema timu yao haiendi kwenye mechi ijayo dhidi ya Yanga kwa lengo la kuisaidia timu nyingine, bali inalenga kupambana kwa manufaa yao.
TRA United itashuka dimbani Juni 27, ugenini dhidi ya Yanga, ikiwa na rekodi ya kutoka sare mfululizo dhidi ya Coastal Union na Namungo. Mara ya mwisho timu hiyo ilipata ushindi Juni 12, 2026 ilipoifunga KMC.
Kwa sasa TRA inashika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi ikiwa imecheza mechi 28, ikishinda 11, sare tisa na kupoteza nane, hivyo kufikisha pointi 42.
Akizungumza na Mwanaspoti, Nasri amesema katika hatua za mwisho za ligi, kila timu inakuwa na malengo yake, hivyo hakuna anayepaswa kuingia uwanjani akiwa na fikra za kuichezea timu nyingine.
Amesema TRA inatambua ukubwa wa mechi pamoja na ubora wa wapinzani wao, lakini hilo halibadilishi malengo waliyojiwekea.
Alieleza, mechi hiyo itakuwa na ushindani mkubwa kwa kuwa kila upande unahitaji matokeo mazuri.
“Tunakwenda kutafuta ushindi kwa manufaa yetu sisi na si kwa ajili ya kuisaidia timu nyingine. Kwenye ligi kila timu inapambana kwa malengo yake.”
Nasri amesema wanaelewa wanakwenda kucheza dhidi ya Yanga, timu yenye kikosi imara na uzoefu mkubwa wa mechi za ushindani, lakini TRA haitaingia uwanjani ikiwa tayari imejiona dhaifu.
Alikumbushia mchezo wa mzunguko wa kwanza waliokutana Arusha na walitoka sare, akisema matokeo hayo yanawapa imani ya kwenda kushindana tena.
“Tunaifahamu Yanga ni timu nzuri, lakini tulipopata nao sare Arusha tuliona inawezekana kupambana nao. Tunajua safari hii itakuwa mechi ngumu zaidi kwa sababu wanaweza kuingia wakitaka kulipa kisasi.”
“Katika kipindi hiki hakuna timu inayocheza kwa mazoea na kila pointi imekuwa na uzito wake. Hivyo, TRA United itaingia uwanjani ikiwa na lengo la kupambana hadi mwisho ili kupata matokeo tunayoyahitaji,” amesema Nasri.