Khatma kocha wa kwanza mwanamke ZPL
Muktasari:
Katika hatua za lala salama na harakati za kujiondoa kwenye hatari ya kushuka daraja, New King ilimaliza ligi hiyo ikiwa mikononi mwa mwanamama huyo, hata hivyo hakufanikiwa kuiokoa.
LICHA ya New King kushuka daraja msimu wa 2025-2026 ilipomaliza nafasi ya 13, lakini Khatma Khamis Mwalimu maarufu Betina, ameandika historia ya kuwa kocha mkuu wa kwanza wa kike kufundisha timu ya wanaume ya Ligi Kuu Zanzibar (ZPL).
Katika hatua za lala salama na harakati za kujiondoa kwenye hatari ya kushuka daraja, New King ilimaliza ligi hiyo ikiwa mikononi mwa mwanamama huyo, hata hivyo hakufanikiwa kuiokoa.
Baada ya kuandika historia hiyo, kocha huyo amesema anajisikia furaha kukabidhiwa majukumu hayo makubwa ya kufundisha timu ya Ligi Kuu Zanzibar kwani awali alikuwa anafundisha wanawake pekee.
“Nimejisikia furaha sana kwa sababu hakuna kitu ambacho nakipenda kwenye maisha yangu zaidi ya mpira, hivyo kupata nafasi hii ni jambo la kujivunia kwangu,” amesema.
Alieleza, baada ya kumaliza masomo yake ya ukocha, amepata nafasi ya kuaminiwa kuongoza jahazi la New King hadi kumalizika kwa msimu wa 2025-2026 akichukua mikoba ya Ali Shein.
Amesema kupata nafasi hiyo ndiyo mwanzo wa safari yake akiamini kwamba ipo siku atafundisha timu kubwa zaidi baada ya kuanza na timu changa iliyopanda daraja.
Alibainisha, anaamini uzoefu wa mtu unapimwa kutokana na changamoto, hivyo kila anapopata changamoto mpya anajiona atakuwa vizuri mbele ya safari.
Amesema ligi ya wanaume ina hamasa zaidi ya wanawake, hivyo amejiona mwenye thamani kuaminiwa.
Wakati Khatma akiandika historia hiyo, msimu wa 2025-2026 katika Ligi Kuu ya Ujerumani maarufu Bundesliga, Kocha Marie-Louise Eta naye alikuwa mwanamke wa kwanza kufundisha timu ya ligi kuu wanaume akiwa na kikosi cha Union Berlin. Haikuishia hapo, pia amekuwa mwanamke pekee kufundisha timu ya ligi kuu wanaume katika ligi tano bora Ulaya.
Msimu wa 2024-2025, Jackline Juma aliandika historia ya kuwa kocha wa kwanza mwanamke kufundisha Ligi Kuu Soka ya Kenya akiwa na kikosi cha Talanta FC.
Kwa Tanzania Bara, Kocha Mkuu wa Yanga Princess, Edna Lema, amekuwa na matamanio ya muda mrefu kuandika historia kama hiyo na Aprili 2025, alipata fursa ya kuwepo kwenye benchi la ufundi la Yanga lililokuwa likiongozwa na Kocha Mkuu, Miloud Hamdi, wakati timu hiyo ilipocheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar.