Prime
Msimu wa adhabu Simba yaipiga bao Yanga
WATANI wa jadi, Simba na Yanga mbali ya ushindani wa kuwania mataji, kusajili wachezaji nyota katika vikosi vyao, awamu hii klabu hizo kongwe zimekutana kwenye anga lingine.
Katika msimu huu wa 2025-2026 wa Ligi Kuu Bara inayosimamiwa na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), hautabaki na kumbukumbu ya burudani ya uwanjani pekee, bali kanuni zilivyosimamiwa na kutoa hukumu bila ya upendeleo au kuangalia hawa ni Simba au Yanga.
Ingawa faini hizo zimezikumba timu mbalimbali, kuanzia Ligi Kuu Bara, Championship, First League na Ligi Daraja la Pili, Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya TPLB ilitoa adhabu zilizowagusa wachezaji, makocha, viongozi, waamuzi, mashabiki na klabu, huku Simba na Yanga zikiwa vinara kwa kukamuliwa mamilioni ya fedha.
Takwimu zinaonyesha kati ya Sh384.4 milioni zilizokusanywa, klabu zilichangia Sh357.7 milioni, sawa na asilimia 93.1 ya fedha zote. Simba na Yanga pekee zimelipa faini ya Sh110 milioni kati ya hizo zilitokana na mechi za dabi mbili zikichangia Sh45 milioni.
Mbali ya klabu hizo kongwe, wachezaji mbalimbali walitozwa faini jumla ya Sh20.4 milioni (asilimia 5.3) huku viongozi na maofisa wakichangia Sh6.3 milioni (asilimia 1.6) kupitia faini zao.
SIMBA WANAONGOZA
Simba imeongoza kwa kulipa faini nyingi zaidi msimu huu ambayo ni Sh60 milioni, kutokana na mfululizo wa makosa ya kiutawala, nidhamu ya mashabiki na matukio ya uwanjani yaliyogusa moja kwa moja kanuni mbalimbali za TPLB.
Mojawapo ya matukio makubwa ni mchezo wa dabi ya kwanza iliyopigwa Zanzibar dhidi ya Yanga ambapo Simba ilitozwa Sh5 milioni kwa kuingia uwanjani kupitia mlango usio rasmi, kinyume cha Kanuni ya 17:62, inayosimamia taratibu za kuingia na maandalizi ya mchezo. Pia, katika mchezo huo, Simba iliongezewa Sh5 milioni nyingine baada ya kukataa kutumia chumba rasmi cha kubadilishia nguo, hatua iliyokiuka Kanuni ya 17:20.
Katika tukio jingine, walinzi wa klabu hiyo walihusishwa na fujo na matumizi ya lugha chafu, hali iliyosababisha Simba kutozwa Sh5 milioni chini ya Kanuni ya 47:1, inayohusu udhibiti wa tabia za maafisa wa timu na mashabiki.
Mashabiki wa Simba pia waliigharimu klabu hiyo kwa mara mbili tofauti, ambapo klabu ilitozwa Sh10 milioni kila tukio baada ya mashabiki kuwarushia chupa za maji waamuzi wasaidizi katika michezo dhidi ya Azam FC na Pamba Jiji, hilo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1, inayowawajibisha klabu kwa matendo ya mashabiki wao.
Katika mechi dhidi ya Dodoma Jiji, Simba ilitozwa Sh5 milioni nyingine baada ya muokota mipira kumwaga vimiminika karibu na eneo la lango la wapinzani, kitendo kilichotafsiriwa kuwa ni imani za kishirikina chini ya Kanuni ya 47:2, inayopiga marufuku vitendo vya aina hiyo uwanjani.
HIKI KILIIGHARIMU YANGA
Yanga imeshika nafasi ya pili kwa kulipa Sh50 milioni huku sehemu kubwa ya adhabu ikitokana na ukiukwaji wa taratibu za maandalizi ya mchezo na nidhamu ya uwanjani.
Adhabu kubwa zaidi ilikuwa Sh30 milioni, baada ya klabu hiyo kukataa kutumia chumba rasmi cha kubadilishia nguo katika mchezo wa marudiano wa dabi dhidi ya Simba kwenye Uwanja Meja Jenerali Isamuhyo, kinyume cha Kanuni ya 17:20, inayolazimisha matumizi ya vyumba rasmi vilivyopangwa na kamishna wa mechi.
Pia, Yanga ilitozwa Sh5 milioni pamoja na gharama za matengenezo baada ya shabiki wake, Carlos Leonard Mayangura, kuharibu miundombinu ya chumba cha kubadilishia nguo katika mchezo dhidi ya Singida Black Stars, kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 na 47:3, zinazohusu uharibifu wa mali na udhibiti wa mashabiki.
Mbali na faini hizo, Yanga pia ilipewa onyo baada ya kuchelewa kuwasilisha leseni za wachezaji kabla ya mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar, jambo lililokiuka Kanuni ya 17:15 na 17:2 (2.2) kuhusu ratiba ya maandalizi ya mchezo (match countdown na MCM).
WENGINE ILIKUWAJE
Mtibwa Sugar imelipa jumla ya Sh35.5 milioni, ikiwa ni miongoni mwa klabu zilizoathirika zaidi na mchanganyiko wa makosa ya kiufundi, nidhamu ya mashabiki na changamoto za benchi la ufundi.
Adhabu kubwa zaidi ilikuwa Sh20 milioni, baada ya klabu hiyo kucheza mechi nne bila kocha mkuu mwenye sifa, kinyume cha Kanuni ya 77:3 na 47:19, zinazohusu sifa za makocha na adhabu kwa kila mchezo husika.
Mashabiki wa Mtibwa Sugar waliigharimu klabu Sh5 milioni baada ya kufanya fujo katika eneo la vyumba vya kubadilishia nguo dhidi ya KMC, kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1.
Aidha, benchi la ufundi nalo lilitozwa Sh5 milioni baada ya kubainika kufanya vitendo vilivyotafsiriwa kuwa ni imani za kishirikina katika mchezo dhidi ya Mbeya City, chini ya Kanuni ya 47:2.
TRA United yenyewe imelipa jumla ya Sh31.5 milioni, ambapo sehemu kubwa ya adhabu ilitokana na mapungufu ya benchi la ufundi na nidhamu ya kiutendaji ndani ya klabu.
Klabu hiyo ilitozwa Sh15 milioni baada ya kucheza mechi tatu bila kocha mkuu mwenye sifa, kinyume cha Kanuni ya 77:3, inayolazimisha kila klabu kuwa na kocha mwenye leseni A.
Aidha, kocha Etienne Ndayiragije aliigharimu klabu hiyo baada ya kushindwa kuhudhuria mikutano ya waandishi wa habari kabla na baada ya mechi. Awali alitozwa Sh5 milioni, kisha Sh11 milioni nyingine kutokana na kosa hilo kujirudia, chini ya Kanuni ya 17:58, inayowataka makocha kuhudhuria mikutano rasmi ya waandishi wa habari.
Kwa upande wa Dodoma Jiji yenyewe imelipa jumla ya Sh31 milioni, ambapo sehemu kubwa ya adhabu ilitokana na kushindwa kuwa na kocha mwenye sifa pamoja na mapungufu ya kiutawala yaliyojitokeza katika michezo kadhaa ya msimu.
Klabu hiyo ilitozwa Sh5 milioni kwa kila mchezo iliyocheza bila kocha mwenye leseni, kwa mujibu wa Kanuni ya 77:3, katika michezo dhidi ya KMC, Coastal Union ya Tanga na TRA United, hali iliyoweka wazi changamoto ya uthabiti wa benchi la ufundi ndani ya timu hiyo.
Aidha, ilitozwa Sh5 milioni kwa kuchelewa kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo (MCM) dhidi ya Mtibwa Sugar, chini ya Kanuni ya 17:2 (2.2).
Katika tukio jingine kubwa, Dodoma Jiji ilipoteza mchezo kwa mabao 3-0 dhidi ya Pamba Jiji baada ya kushindwa kuhakikisha mfumo wa taa za uwanja unafanya kazi, hali iliyosababisha mchezo kuvunjika. Hii ilitekelezwa chini ya Kanuni ya 32:1 na 32:3, inayohusu kuvunjika kwa mchezo na adhabu ya ‘walkover’ pamoja na kupokwa alama tatu.
HAWAJAGUSWA KABISA
Katika orodha ya timu 16 za Ligi Kuu Bara kwa mujibu wa takwimu kuna timu tatu tu ambazo hazijakumbwa na adhabu ya faini ya klabu msimu huu, licha ya baadhi ya wachezaji wao kupata adhabu binafsi kutokana na matukio mbalimbali ya nidhamu uwanjani.
Kwa upande wa JKT Tanzania, mchezaji Mohamed Bakari alifungiwa michezo mitano (5) baada ya kumkanyaga kwa makusudi mchezaji wa Azam FC, Lusajo Mwaikenda, tukio lililochukuliwa kuwa ni kosa la kinidhamu.
Nyingine ni Fountain Gate, mchezaji Lamela Maneno alifungiwa mchezo mmoja (1) kutokana na kosa la kuonyesha ishara isiyo ya kiuanamichezo baada ya kuonesha kitendo cha kuifuta kadi ya njano aliyokuwa ameonyeshwa na mwamuzi, kitendo kilichotafsiriwa kama kuvunja maadili ya mchezo na mamlaka ya waamuzi.
Kwa upande wa Mbeya City, wachezaji wake wawili wakikumbwa na adhabu kali zaidi. Gabriel Daud Mwaipola alifungiwa michezo mitano (5) pamoja na faini ya Sh1,000,000 baada ya kumpiga ngumi mchezaji wa Namungo FC huku Vitalis Mayanga naye akifungiwa michezo mitano (5) na kutozwa Sh1,000,000 baada ya kumpiga kiwiko kwa makusudi mchezaji wa Simba SC, matukio yote yakionekana kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa kanuni za nidhamu.
SHIDA KUBWA
Mojawapo ya makosa yaliyoonekana kupewa uzito mkubwa na TPLB ni kucheza bila kocha mkuu mwenye leseni inayokubalika ambayo ni leseni A.
Mtibwa Sugar ndiyo iliyoathirika zaidi baada ya kulipa Sh20 milioni, TRA United nayo ilitozwa Sh15 milioni sawa na Dodoma Jiji.
Hatua hiyo inaonyesha msisitizo wa TPLB kwamba maendeleo ya soka hayawezi kutegemea uwekezaji wa wachezaji pekee bila kuwa na benchi la ufundi linalokidhi viwango vya CAF na TFF.
Vyumba vya kubadilishia nguo vikawa chanzo kingine cha rungu hilo la fedha kwa klabu Yanga ilitozwa Sh30 milioni, adhabu ambayo ndiyo kubwa zaidi kwa kosa moja lililotolewa kwa klabu msimu huu.
Lakini haikuwa Yanga pekee, Simba, Azam FC, Mbeya Kwanza na Mashujaa nazo zilitozwa faini mbalimbali kati ya Sh1 milioni hadi Sh5 milioni kutokana na makosa yanayohusiana na matumizi ya vyumba hivyo.
Kwa mujibu wa kanuni za mashindano, timu zinapaswa kutumia maeneo yaliyopangwa na kamishna wa mechi, hivyo ukiukaji wake huonekana kama kuvuruga utaratibu wa mchezo.
WAAMUZI YAMEWAKUTA
Tofauti na misimu iliyopita ambapo lawama nyingi zilielekezwa kwa waamuzi bila hatua kubwa kuchukuliwa, msimu huu TPLB ilionyesha kuwa hata waamuzi hawako juu ya sheria.
Mwamuzi wa kati Amina Kyando pamoja na mwamuzi msaidizi Abdalah Bakenga waliondolewa kwenye ratiba kwa mizunguko mitano baada ya kushindwa kutafsiri sheria katika mchezo wa Pamba Jiji dhidi ya Singida Black Stars.
Walishindwa kuchukua hatua wakati kipa aliposhika mpira nje ya eneo la penalti, Jackson Samwel na Omary Mdoe nao waliondolewa kwenye ratiba kwa mizunguko kadhaa kutokana na makosa ya kiufundi.
Gilbert Mrina pamoja na Abdallah Mwinyimkuu walishushwa madaraja baada ya tathmini ya utendaji wao.