REKODI; Tisa kati ya 10 Afrika zatinga 32 Bora
Muktasari:
- Baada ya hatua ya makundi kukamilika, Afrika imeweka rekodi mpya kwa kushuhudia timu tisa kati ya 10 zilizoliwakilisha zikitinga hatua ya 32 bora, huku Tunisia ikiwa timu pekee iliyoshindwa kuvuka hatua ya makundi.
HAKUNA anayebisha tena kuhusu ukuaji wa soka la Afrika. Kama kulikuwa na mashaka kuongeza nafasi za bara hilo kutoka timu tano hadi 10 katika Kombe la Dunia la 2026 kungepunguza ushindani, majibu yametolewa.
Baada ya hatua ya makundi kukamilika, Afrika imeweka rekodi mpya kwa kushuhudia timu tisa kati ya 10 zilizoliwakilisha zikitinga hatua ya 32 bora, huku Tunisia ikiwa timu pekee iliyoshindwa kuvuka hatua ya makundi.
Hii ndiyo idadi kubwa zaidi ya timu za Afrika kuwahi kufika hatua ya mtoano katika historia ya Kombe la Dunia.
Mafanikio hayo yanamaanisha asilimia 90 ya wawakilishi wa Afrika wameendelea na safari licha ya mmoja kati ya wawakilishi hao ambao ni Afrika Kusini alikuwa na kazi ya kufanya usiku wa kuamkia leo, Jumatatu akijitetea katika hatua ya 32 bora dhidi ya Canada.
Jambo linaloonyesha wazi Afrika kwa sasa imepunguza pengo dhidi ya mataifa makubwa ya Ulaya na Amerika Kusini.
MOROCCO vs UHOLANZI
Baada ya kufika nusu fainali mwaka 2022, Morocco iliingia katika michuano ya 2026 ikibeba matumaini makubwa ya Afrika, ilimaliza hatua ya makundi kwa kiwango kizuri huku ikikusanya pointi saba na kufuzu hatua ya 32 bora, ikithibitisha mafanikio yao ya Qatar hayakuwa ya bahati mbaya bali ni matokeo ya uwekezaji mkubwa katika maendeleo ya soka.
Ikiwa kundi C ilianza fainali hizo kwa kuitoa jasho Brazil katika sare ya bao 1-1 kisha ikaifunga Scotland bao 1-0 na kuishushia mvua ya mabao 4-2 Haiti na kumaliza hatua hiyo kibabe nyuma ya Brazil wote wakiwa na pointi sawa tofauti yao ikawa mabao ya kufunga na kufungwa.
Kwa sasa wababe hao wanakabiliwa na kibarua kigumu usiku wa kuamkia Juni 30 saa 10:00 alfajiri kwa saa za Afrika Mashariki dhidi ya Uholanzi katika mechi inayotajwa kuwa moja ya vita vikubwa vya hatua ya mtoano.
WASAUZI HAWANA DENI
Bafana Bafana wamekuwa moja ya hadithi nzuri zaidi za michuano hii. Baada ya miaka mingi ya kusubiri kurejea katika fainali hizo, walifuzu hatua ya mtoano na usiku wa kuamkia leo, Jumatatu wamekipiga na Canada.
Iwapo itashinda, inaweza kukutana na mshindi wa mchezo kati ya Morocco na Uholanzi katika hatua inayofuata, safari ambayo inaweza kuwapeleka mbali zaidi kuliko wengi walivyotarajia.
SENEGAL YAONYESHA UZOEFU
Licha ya kuangukia katika moja ya makundi magumu zaidi yaliyokuwa na Ufaransa, Norway na Iraq, Senegal ilionyesha kwa mara nyingine ni moja ya mataifa yenye uzoefu mkubwa katika soka la Afrika.
Ingawa ilianza vibaya kwa kupoteza mechi mbili za kwanza, haikukata tamaa na ilipigania nafasi yake hadi dakika za mwisho za hatua ya makundi.
Safari ya Simba wa Teranga ilianza kwa kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya Ufaransa katika mechi ya ufunguzi wa Kundi I. Baada ya hapo walikutana na Norway na kupambana lakini wakaondoka tena mikono mitupu baada ya kufungwa mabao 3-2, matokeo yaliyowaweka kwenye hali ngumu kutinga mtoano.
Wakiwa hawana chaguo jingine zaidi ya kushinda mchezo wao wa mwisho, Senegal iliingia uwanjani dhidi ya Iraq ikiwa na presha kubwa. Iliitumia vyema nafasi hiyo kwa kuichapa mabao 5-0 katika ushindi mkubwa uliowapa pointi zao za kwanza na kuboresha tofauti ya mabao.
Ushindi huo uliifanya Senegal kumaliza nafasi ya tatu ikiwa na pointi tatu na tofauti ya mabao ya +2 (mabao 8 ya kufunga na 6 ya kufungwa), jambo lililoiwezesha kuingia hatua ya 32 bora kama moja ya timu bora zilizomaliza nafasi ya tatu.
Sasa Simba wa Teranga wanakabiliwa na mtihani mwingine mkubwa dhidi ya Ubelgiji Julai mosi katika hatua ya mtoano. Pamoja na kuingia kwa njia ya timu bora zilizomaliza nafasi ya tatu, uzoefu wao katika mashindano makubwa na uwezo wa nyota kama Sadio Mané, Kalidou Koulibaly na Pape Matar Sarr unawafanya kuwa wapinzani ambao Ubelgiji haiwezi kuwabeza.
HUKU MISRI KULE IVORY COAST
Baada ya kukosa mafanikio katika baadhi ya fainali zilizopita, Misri imeonyesha ukomavu mkubwa katika hatua ya makundi.
Mafarao hao ambao walimaliza hatua ya makundi wakiwa na pointi tano sasa watacheza dhidi ya Australia wakisaka nafasi ya kutinga 16 bora na kurejesha heshima ya moja ya mataifa makubwa zaidi ya soka Afrika.
Kwa upande wa Ivory Coast wameonyesha kwa nini waliitwa miongoni mwa timu zenye uwezo mkubwa zaidi kutoka Afrika.
Baada ya kuvuka makundi wakiwa na pointi sita sawa na Ujerumani iliyoongoza kundi E, sasa watakutana na Norway katika pambano ambalo wengi wanaamini linaweza kuwapa nafasi nzuri ya kufika hatua ya 16 bora iwapo wataendelea kucheza kwa nidhamu waliyoionyesha.
GHANA WAMEWEZA
Baada ya miaka ya kupanda na kushuka, Black Stars wamerejea kwenye ushindani mkubwa.
Kitendo cha Ghana kuvuna pointi nne katika mechi mbili za kwanza katika hatua ya makundi kufuatia kuichapa Panama bao 1-0 kisha kutoa suluhu dhidi ya England kiliwafanya kuwa na nafasi ya kusonga mbele hata kabla ya mechi ya mwisho ya hatua hiyo ambayo walipoteza dhidi ya Croatia kwa mabao 2-1 hivyo kushika nafasi ya tatu.
Hivyo kufuzu kama moja ya timu bora iliyoshika nafasi ya tatu. Kituo kinachofuata kwao ni kucheza dhidi ya Colombia, mechi ambayo itahitaji nidhamu ya hali ya juu na kutumia vizuri nafasi chache watakazozipata mbele ya moja ya timu bora kutoka Amerika Kusini.
CAPE VERDE NA DR CONGO
Huenda hakuna timu iliyowashangaza wengi kama Cabo Verde. Nchi hiyo ndogo imeendelea kuandika historia kwa kufuzu hatua ya mtoano katika ushiriki wake wa kwanza wa Kombe la Dunia, jambo lililoifanya kuwa moja ya hadithi kubwa za mashindano haya.
Changamoto yao inayofuata ni Argentina, mabingwa watetezi, mechi ambayo itakuwa kipimo kikubwa cha uwezo wao.
Kwa upande wao, Leopards waliandika historia kwa kupata ushindi wao wa kwanza kabisa katika Kombe la Dunia walipoifunga Uzbekistan mabao 3-1 na kufuzu hatua ya mtoano.
Sasa wanakutana na England, lakini tayari wameonyesha kuwa hawapo Marekani, Canada na Mexico kwa ajili ya kushiriki tu bali kushindana.
ALGERIA ILIFUNGA HESABU
Algeria ilithibitisha kwa mara nyingine kuwa ni moja ya mataifa yenye roho ya upambanaji Afrika baada ya kufuzu hatua ya 32 bora kupitia Kundi J.
Mbweha wa Jangwani walimaliza hatua ya makundi kwa sare ya kusisimua ya mabao 3-3 dhidi ya Austria, matokeo yaliyowahakikishia tiketi ya kuendelea na mashindano kama moja ya timu bora zilizomaliza nafasi ya tatu.
Sasa Algeria inakabiliwa na mtihani mwingine mkubwa dhidi ya Uswisi katika hatua ya 32 bora.
Mechi hiyo inaonekana kuwa na ushindani mkubwa na nafasi zikiwa karibu kufanana kwa pande zote mbili, hali inayowapa Mbweha wa Jangwani matumaini ya kuandika historia nyingine kwa kutinga hatua ya 16 bora endapo wataendelea kuonyesha kiwango na ari waliyoionyesha katika hatua ya makundi.
SA’ITAKUWAJE
Kama mashindano ndio yameanza sasa katika hatua ya 32 bora. Timu nyingi za Afrika zimepangwa dhidi ya vigogo wa soka duniani kama England, Argentina, Ubelgiji na Uholanzi lakini historia ya hivi karibuni inaonyesha hakuna timu inayopaswa kudharauliwa.
Morocco tayari ilifika nusu fainali mwaka 2022, Senegal imewahi kucheza robo fainali, Ghana iliwahi kugusa nusu fainali kwa sekunde chache mwaka 2010 kabla ya kibao kuwageukia na kutupwa nje huku Ivory Coast, Algeria na Misri zikiwa na vikosi vyenye uzoefu mkubwa.
Iwapo angalau timu tatu au nne zitaingia hatua ya 16 bora, Afrika itaendelea kuweka rekodi nyingine huku ndoto ya kupata bingwa wa kwanza kutoka Afrika ikiwa haionekani tena kuwa mbali kama ilivyokuwa miaka iliyopita.