Kesi ya Mkude, Simba ngoma nzito

HATMA ya kesi ya kiungo Jonas Mkude dhidi ya klabu yake ya Simba inatarajiwa kufahamika leo saa 10 jioni baada ya juzi kesi hiyo kushindwa kumalizika.

Mkude ameshtakiwa na uongozi katika Kamati ya Nidhamu na Maadili ya Simba, akituhumiwa kutokuwepo kwenye mazoezi bila taarifa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, RPC wa zamani Suleiman Kova aliliambia Mwanaspoti kuwa, kesi hiyo ilisikilizwa Jumamosi lakini haikumalizika.

“Muda haukutosha, hivyo kesho (leo) itaendelea na hadi kufikia saa 10 jioni hukumu itakuwa imetolewa,” alisema Kova.

Alisema Jumamosi walimsiliza Mkude na Mwanasheria wake na kisha upande wa Simba na Mwanasheria wake, lakini muda haukutosha kutoa hukumu.

Akizungumzia kesi hiyo, Kova alisema Mkude anatuhumiwa kutokuwepo mazoezini Mei 18 bila taarifa.

“Ni kama alijipa ruhusa mwenyewe, kwani baada ya Simba kurejea nchini wakitokea Afrika Kusini Mei 17, waliruhusiwa kwenda nyumbani na kutakiwa kambini Mei 18 saa 3 asubuhi. Hakutokea.”