KenGold yawaganda mastaa, yaahidi kurudi upya Ligi Kuu

Muktasari:
- KenGold imeshuka daraja baada ya kushiriki Ligi Kuu msimu mmoja tu na sasa wanasubiria kucheza Championship msimu ujao, huku matarajio yakiwa ni kupanda tena fasta kuungana na wengine wakiwamo Yanga na Simba.
PAMOJA na kukubali kushuka daraja, kocha mkuu wa KenGold, Omary Kapilima amesema wanafanya kila linalowezekana kuwashawishi mastaa waliofanya vizuri kikosini ili wabaki nao kwa ajili ya kupambana katika Ligi ya Championship kwa lengo la kurudi upya katika Ligi Kuu Bara.
KenGold imeshuka daraja baada ya kushiriki Ligi Kuu msimu mmoja tu na sasa wanasubiria kucheza Championship msimu ujao, huku matarajio yakiwa ni kupanda tena fasta kuungana na wengine wakiwamo Yanga na Simba.
Katika kikosi cha timu hiyo, asilimia kubwa ya wachezaji mikataba yao inaisha mwisho wa msimu huu, wakiwamo mastaa waliotua katika dirisha dogo kama Bernard Morrison, Seleman Rashid ‘Bwenzi’, Obrey Chirwa, Kelvin Yondani, Zawadi Mauya, Sadala Lipangile na Kyala Lasa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kapilima alisema bado ni mapema kujua iwapo atabaki au kung’atuka baada ya ligi kuisha, akieleza kuwa kwa sasa wanasubiri kuhitimisha msimu ili kujua hatma yao.
Beki huyo wa kulia wa zamani wa Majimaji, Yanga, Mtibwa Sugar na Taifa Stars, alisema iwapo ataendelea kubaki kikosini humo, hatua ya kwanza ni kukutana na uongozi kujadiliana namna ya kuwabakiza nyota waliofanya vizuri kuwashawishi kuitumikia timu hiyo ili irejee Ligi Kuu.
“Kwa kuwa tunazo mechi mbili ni ngumu kujua kama nitabaki au kuondoka, lakini iwapo nitaendelea kuwapo nitazungumza na mabosi kushawishi waliofanya vizuri waendelee kubaki ili turudi haraka Ligi Kuu,” alisema Kapilima.
Kocha huyo, aliongeza kuwa sababu ni nyingi zilizoishusha timu hiyo Championship akifafanua katika sehemu ya ufundi, beki haikuwa bora kwa kuwa mechi walizocheza takribani zote wameruhusu bao. Alisema, kwa sasa wanakubaliana na matokeo waliyovuna, ambapo hesabu zao ni kusubiri mechi mbili zilizobaki kutafuta heshima na kujiandaa upya kwa ajili ya msimu ujao wa Championship.
“Tunakubaliana na matokeo, tunasubiri kuhitimisha ligi kwa kutafuta ushindi ili kuweka heshima tu, vinginevyo tunaenda kufanya tathmini na kujipanga upya kwa ajili ya Championship msimu ujao,” alisema.
KenGold, iliyopanda daraja msimu huu baada ya kushika nafasi ya kwanza katika Ligi ya Championship msimu uliopita ikifuatiwa na Pamba Jiji inayoendelea kupambana kusalia kwa msimu ujao wa Ligi Kuu, imekusanya pointi 16 katika mechi 28.
Katika mechi hizo 28, Wachimba Dhahabu hao wameshinda tatu tu, kutoka sare saba na kupoteza 18, huku wakifunga mabao 22 na kufungwa 52, wakiwa wa pili nyuma ya Fountain Gate iliyofungwa mabao 54, lakini wakiwa ni timu ya kwanza kushuka daraja kabla ya juzi Kagera Sugar kuwafuata.