Ken Gold kuzipeleka Simba, Yanga Chunya

Muktasari:

  • Ken Gold imepanda Ligi Kuu msimu huu, huku ushindi wa leo wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania ikiwafanya kuwa mabingwa kwa pointi 70, huku nyota wake William Edgar akiwa kinara wa ufungaji akitupia mabao 21.

'Tanzania tunaitaka Chunya'. Ni kauli ya Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbarack Batenga akielezea Ken Gold kutumia Uwanja wa Chunya kwa ajili ya mechi zao za nyumbani Ligi Kuu msimu ujao.

Uwanja huo ambao ulitumika katika michuano maalumu ya Mbeya Pre Season, una uwezo wa kubeba watazamaji 20,000 ambao kwa sasa unaendelea na ujenzi na ulitarajiwa kutumika katika mzunguko wa pili wa Championship kwa timu hiyo.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo wa kufunga msimu wa 2023/24 leo Aprili 28 ambao Ken Gold imeshinda 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania, Batenga amesema heshima waliyoiweka wachezaji lazima Tanzania ipelekwe Chunya.

Amesema kupanda Ligi Kuu na kumaliza kinara kwa pointi 70 haikuwa kazi rahisi bali ni mipango na kwamba haijapanda bahati mbaya isipokuwa kujituma na kuipambania Mbeya kwa ujumla.

"Hiki kipo upande wetu kama serikali, cha kuwaahidi ni kuona Tanzania tunaipeleka Chunya, timu haijapanda wala kubeba ubingwa kibahati mbaya, niwapongeze viongozi na wachezaji kwa ujumla," amesema Batenga.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ken Gold, Keneth Mwambungu amesema haikuwa kazi rahisi kufikia malengo, lakini ushirikiano wa pamoja na wadau mbalimbali imewezesha kumaliza safari ya misimu minne.

"Kwa maana hiyo tunaomba uwanja pale Chunya timu ichezee pale, ile ni wilaya yenye madini na vyanzo vingi vya uchumi, hivyo serikali tunaomba hilo lifanyiwe kazi," amesema Mwambungu.

Mmoja wa wadau wa soka na mkazi wa Chunya, Ayoub Omary amewapongeza wachezaji kwa kazi nzuri huku akiwazawadia pesa zaidi ya Sh1 milioni.

"Sasa kazi imeisha, tusibweteke huko tuendako bali tujipange na msimu ujao kuhakikisha tunacheza Ligi Kuu kwa mafanikio bila kushuka daraja," amesema Omary.

Ken Gold pamoja na Pamba Jiji FC zimepanda Ligi Kuu Bara moja kwa moja kwa kushika nafasi ya kwanza na ya pili mtawalia, huku Mbeya Kwanza na Biashara United Mara zitatafuta nafasi ya kupanda kupitia mtoano (playoff). Mshindi kati yao atakutana na mshindi wa play-off ya Ligi Kuu Bara itakayozikutanisha timu ya 13 na 14 katika msimamo.