Kazumba ndio basi tena Prisons

Muktasari:
- Kazumba amekuwa kikosini humo kwa muda mrefu, ambapo licha ya kutoelezwa sababu haraka lakini inadaiwa kuondoshwa katika nafasi hiyo.
Baada ya kuitumikia kwa muda mrefu, inasemekana Tanzania Prisons imemuondoa Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Shaban Kazumba huku nafasi yake ikichukuliwa na Shaban Mtupa aliyekuwa akiinoa timu ya vijana (U-20).
Kazumba amekuwa kikosini humo kwa muda mrefu tangu alipostaafu kuichezea mwaka 2006 na kupewa majukumu hayo hadi kufikia uamuzi huo jana jioni.
Bila kutaja sababu za Kocha huyo kuondoshwa nafasi hiyo, Katibu Mkuu wa timu hiyo, Anthony How amesema kesho Jumatatu ndio atalifafanua zaidi atakapofika ofisini kwani ni tamko kutoka juu.
Amesema kuondoshwa kwa mkongwe huyo, Mtupa ndiye atachukua mikoba yake kusaidiana na Kocha Mkuu, Patrick Odhiambo kuendelea na program.
"Mabadiliko hayo bado ila yapo nadhani kesho Jumatatu nikifika ofisini ndio nitajua sababu zaidi kwakuwa ni tamko kutoka juu, nafasi yake atachukua Mtupa aliyekuwa na timu ya vijana" amesema How.
Hata hivyo habari za ndani zinasema kuwa katika mechi iliyopita dhidi ya Biashara United, hakukuwapo mawasiliano mazuri kwenye benchi la ufundi, lakini ishu ya usajili kwa wachezaji nayo inatajwa.
Pia inasemekana kuwapo mgogoro wa kimaslahi kwa wachezaji Askali na raia wa kawaida kutofautiana kwa posho zinazotolewa lakini pia nyota wanaotumika zaidi kikosini kwa maslahi madogo.