Katumbi noma, atia mkono usajili Yanga

Monday June 21 2021
katumbi pic
By Mwandishi Wetu

MABOSI wa Yanga wamepigwa na butwaa, baada ya bilionea wa TP Mazembe, Moise Katumbi kuonyesha jeuri ya fedha kwa kuifanyia umafia kwa kumchomoa juu kwa juu kiungo mmoja matata aliyekuwa anajiandaa kutua Jangwani kukiimarisha kikosi cha timu hiyo kwa msimu ujao.

Katumbi amewafanyia ukatili Yanga, baada ya kutua na begi la fedha na kumaliza biashara ya kiungo huyo aliyekuwa akitajwa kuja kuchukua nafasi ya Haruna Niyonzima na kuwaacha mabosi wa Jangwani wakicheka tu baada ya kuambiwa ‘msitume tena ile pesa’.

Ipo hivi. Yanga ilikuwa inafanya utaratibu wa kuilipa klabu ya Union Maniema ya DR Congo ambayo Mwanaspoti ilikupa mchongo mzima wa klabu hiyo kukamilisha usajili wa kiungo fundi Mercey Ngimbi ambaye alishakubali kila kitu ili atue kwenye kikosi chao.

Hata hivyo, kama tulivyokuwa tumedokeza mapema Ngimbi alishaaanza mazungumzo na TP Mazembe inayomilikiwa na Katumbi, lakini kiungo huyo aligomea dili hilo akitishwa na mkataba wa miaka mitano wa mab-ingwa hao wa DR Congo.

Hatua ya Ngimbi kugo-mea dili hilo la Mazembe, ilitokana na Yanga kumtuma Injinia Hersi Said nchini humo wakati kiungo huyo akiwa Tunisia na kikosi cha timu ya taifa na kuam-biwa katika pesa hiyo hiyo Yanga itamchukua kwa mkataba wa miaka miwili.

Yanga ilitaka kumpa Ngimbi Dola 40,000 (kama Sh92 milioni) kwa mkataba wa miaka miwili, lakini Katumbi alivyosikia hivyo akapanda dau mara mbili kwa mchezaji na kwa klabu yake yenyewe.

Advertisement

Mwanaspoti, linafahamu bilionea amewapa pesa ndefu Maniema, Dola 100,000 (kama Sh231 milioni) kama ada ya uhamisho na hapo ndipo kukawafanya Maniema kuwaam-bia Yanga tulieni msitume kwanza pesa ya Ngimbi.

Mratibu wa Maniema, Guy Kapya Kilongozi aliliambia Mwanaspoti jana, ni kweli Ngimbi atakuwa mchezaji wa Mazembe baada ya Yanga kuzidiwa dakika za mwisho na Katumbi.

“Yanga walikuja vizuri, lakini naweza kusema walichelewa pia kuweka pesa, mchezaji alitaka kuja Tanzania kuungana na rafiki zake, lakini walipochelewa Katumbi amekuja kwa haraka na pesa nyingi sana na akamchukua,” alisema Kilongozi.

“Kama Yanga ingeweka pesa kwa wakati ingempata mchezaji huyo kutokana na ukweli awali alishawagomea Mazembe lakini jana (juzi) ilibidi tuwaambie Yanga wasitishe kwanza kuingiza pesa, Mazembe walishakuja na hapa tayari na wakamwekea pesa nyingi mchezaji.

”Kwa maana hiyo, Yanga sasa inabidi ianze upya kazi ya kusaka kiungo mchezeshaji wa kuziba pengo hilo linaloachwa na Ngimbi, kwani waliamini angetua Jangwani kazi ingekuwa rahisi kwao kwa kuweza kuunganishwa pamoja na Wakongo wenzake, Mukoko Tonombe, Tuisilia Kisinda na beki Djuma Shaban aliyekamilishiwa usajili wake mapema akitokea AS Vita.

Advertisement