Kamusoko ampa Manji straika, atamba heshima itarudi

Muktasari:

KIUNGO wa zamani wa Yanga, Thaban Kamusoko ‘Kampa Kampa tena’ amesikia kishindo cha ujio wa Mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Yusuf Manji akamsisitiza kwamba akitaka kufaidi aanze usajili na straika wa maana, aliyekomaa na anayeliona goli.

KIUNGO wa zamani wa Yanga, Thaban Kamusoko ‘Kampa Kampa tena’ amesikia kishindo cha ujio wa Mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Yusuf Manji akamsisitiza kwamba akitaka kufaidi aanze usajili na straika wa maana, aliyekomaa na anayeliona goli.

Akizungumza kwa njia ya simu na Mwanaspoti Kamusoko, alisema tajiri huyo ujio wake utakuwa na faida kubwa Jangwani kwavile anajua fika kwamba ni mtu wa matumizi na anapenda kitu kizuri kwavile amefanya nae kazi Yanga.

Kamusoko ambaye ni Mzimbabwe, alisema Manji na GSM ambao wako Yanga kwa sasa, anajua wanatafuta mastraika lakini wanatakiwa kuhakikisha wanapata mshambuliaji aliyekomaa kiakili kwa ushindani na sio kuchukua mchezaji anayechipukia na ili kufanikisha hilo lazima wakubali kutumia gharama kubwa vinginevyo watakuwa wanafanya masihara tu.

“Nimeona sehemu Manji amerudi,namjua Manji nimefanya naye kazi huyo ni bosi ambaye anajua kutumia pesa kwa ushindani sasa ukichukua nguvu yake akakaa kwa pamoja na hao GSM wanaweza kufanya usajili mzuri.

“Washambuliaji wazuri wana gharama sana sio rahisi na hii sio tu Yanga ni duniani mshambuliaji anahitaji pesa nyingi sasa kama wataunganisha nguvu wataweza kufanya usajili ambao utawapa heshima katika mashindano ya Afrika,”alisema Kamusoko ambaye amebeba taji la Zambia msimu huu akiwa na Zesco.

“Nimeona hapo Tanzania kwamba msimu ujao mtaingiza tena timu nne ila akili yangu ipo kwa timu yangu ya Yanga ni lazima sasa viongozi wajue mahitaji ya timu yao na aina gani ya wachezaji wanaotakiwa kuwatafuta,”alisema Kamusoko ambaye alikuwa na heshima kubwa kwa soka lake la kampa kampa tena.

“Unaona miaka ya karibuni wameyumba sana Yanga ilikuwa inachukua wachezaji watoto hawajakomaa kwa ushindani wa hapo Tanzania,kuichezea Yanga na ukang’aa sio kitu chepesi unatakiwa ukomae kiushindani na kichwani kwako,”alisema na kuongeza kwamba kwenye michuano hiyo ya Afrika inayoanza mwezi Septemba, Yanga inapaswa kurudi kwa kishindo na kuzidi rekodi zao za miaka ya nyuma ili kuonyesha kuwa wana kitu cha ziada kuliko watani zao, Simba.

“Watafute mastraika waliofanya vizuri kwa muda mrefu na sio mtu wa kuja kukua hapo,Yanga anatakiwa mshambuliaji awe na ubora wa kufunga kama vile alivyokuwa Tambwe (Amissi) hata siku akifanya vibaya akizomewa akili yake itulie na aendelee kujituma na sio kukata tamaa atapotea.

“Hapo kuna presha kubwa sana sio rahisi sasa kwa mazingira ya hapo lazima mchezaji awe amekomaa kiakili na washambuliaji hao wapo ila ni jinsi gani ya kuwapata hapo ndipo unapotakiwa kutulia,”alisema Kamusoko ambaye pia awali alijulikana kwa jina la rasta.

Kocha wa Yanga, Nabi Mohammed ambaye ni raia wa Tunisia, ameliambia Mwanaspoti kwamba usajili wa msimu ujao anafanya kwa kusaidiana na maskauti wa nje na tayari ameshawaunganisha na viongozi na kuwaambia anataka wachezaji wa aina gani.

Licha ya Kocha huyo kufanya siri lakini Mwanaspoti limedokezewa na uongozi kwamba anataka wachezaji wapya nane, watano kati ya hao wakiwa wa kigeni ambao ni kipa mzoefu, beki wa kati, winga, kiungo na straika.

Katika mastaa wa kigeni waliopo Yanga, Mwanaspoti linajua amewaambia viongozi kwamba anataka kusaliwa na wanne tu ambao ni Saido Ntibazonkiza, Yacouba Songne, Tuisila Kisinda na Mukoko Tonombe.