Kama zali vile, Yanga imepindua meza aisee

Muktasari:

Wawakilishi hao wa Tanzania waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 kwenye mechi ya kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Aprili 7 ingawa ilipoteza mechi ya marudiano huko Ethiopia, juzi Jumatano, Aprili 18.

YANGA imefuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuitoa Welaytta Dicha ya Ethiopia kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1.

Wawakilishi hao wa Tanzania waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 kwenye mechi ya kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Aprili 7 ingawa ilipoteza mechi ya marudiano huko Ethiopia, juzi Jumatano, Aprili 18.

Kufuzu kwa Yanga kwenye hatua hiyo kunakamilisha miaka 10 ya ubabe wa klabu hiyo kongwe nchini dhidi ya watani wao wa jadi, Simba ambao ni wapinzani wao wakuu katika medani ya soka nchini.

Kuanzia mwaka 2000 hadi 2007, Simba ndio ilikuwa ikitajwa kama timu tishio na iliyofanya vizuri zaidi katika soka hapa Tanzania lakini baada ya hapo, Yanga imeonekana kubadilisha upepo na kuwaacha mbali kimafanikio watani wao. Watoto wa mjini wanasema Yanga imepindua meza.

Mataji 7 Ligi Kuu

Hadi mwaka 2007, Yanga ilikuwa imechukua ubingwa wa Ligi Kuu mara 21 huku Watani wao wa Jadi, Simba ambao walikuwa wametwaa ubingwa mara 16 ikiwa ni tofauti ya mataji matano baina yao.

Baada ya hapo Yanga imetanua pengo dhidi yao na Simba katika kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu, kwani kuanzia mwaka 2008 hadi sasa, Watoto wa Jangwani wamechukua ubingwa mara sita huku Wekundu wa Msimbazi wakichukua mara mbili na kufanya wazidiwe mataji tisa ya Ligi Kuu kutoka matano yaliyokuwepo hapo mwanzo.

Kwa jumla hadi sasa, Yanga imechukua ubingwa wa Ligi Kuu mara 27 huku Simba ikiwa imetwaa mara 18.

Kombe la Kagame

Hadi mwaka 2007, Simba ilikuwa imetwaa mataji matatu zaidi ya Yanga kwenye Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame). Mwaka huo Yanga ilikuwa imechukua ubingwa huo mara sita huku watani wao wa jadi wakitwaa mara tatu.

Hata hivyo, Yanga imeonekana kukitumia vizuri kipindi cha miaka 10 kuutikisa ufalme wa Simba, Afrika Mashariki na Kati kwani imekuwa ndio timu iliyotwaa taji hilo mara nyingi zaidi katika kipindi hicho kuliko nyingine.

Yanga imetwaa kombe hilo mara mbili ,mwaka 2011 na 2012 huku mabingwa wa kihistoria wa mashindano hayo, Simba wakitoka patupu jambo linalofanya Yanga iwe imechukua kombe hilo mara tano ambazo ni moja pungufu ya Simba.

Mafanikio Afrika

Simba ndio ilikuwa ikionekana kama mkombozi wa soka la Tanzania katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho kutokana na rekodi yake ya kufika hatua za juu zaidi za mashindano hayo katika miaka ya nyuma.

Mambo yamegeuka katika miaka 10 ya hivi karibuni kwani Yanga imekuwa na rekodi nzuri ya ushiriki wa mashindano ya kimataifa kulinganisha na Simba.

Katika kipindi hicho cha miaka 10, Yanga imefuzu mara mbili katika hatua ya makundi ya mashindano ya Afrika kwa ngazi ya klabu tofauti na Simba ambayo imegeuka kuwa msindikizaji.

Yanga imeingia katika hatua hiyo mara mbili, 2016 na mwaka huu ingawa ni katika Kombe la Shirikisho ambalo ni mashindano ya pili kwa ukubwa kwa ngazi ya klabu Afrika.

Vita ya usajili

Simba imeonekana kuonewa kwa mafanikio ya ndani ya uwanja lakini hata nje ya uwanja bado imeendelea kuwa wanyonge kwa Yanga katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Katika muda huo, Yanga imefanikia kuvuna idadi kubwa ya wachezaji kutoka Simba huku watani wao wa jadi wakinasa nyota wachache.

Nyota wa Simba waliotimkia Yanga katika kipindi hicho ni Juma Kaseja, Kelvin Yondani, Rashid Gumbo, Hassan Kessy, Ally Mustafa ‘Barthez’, Emmanuel Okwi na Ibrahim Ajibu wakati Simba yenyewe iliwanasa Amir Maftah na Haruna Niyonzima tu kutoka Yanga.