Kama sio gundu kumbe nini?

USIKU wa jana Jumamosi ulikuwa muhimu kwa staa wa Liverpool, Mohamed Salah, kuikataa rekodi mbaya ya kuingia kwenye orodha ya mastaa wa maana wa soka la dunia walioshindwa kuonja utamu wa kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Staa huyo wa kimataifa wa Misri jana alitarajia kukiongoza kikosi chake cha Liverpool kwenye fainali ya michuano hiyo ya Ulaya kwa kucheza na Real Madrid huko mjini Kiev, Ukraine. Kilichotokea huko ndio kama ulivyosikia.

Cheki hii hapa orodha ya mastaa wa maana kweli kweli waliowahi kutamba katika soka la dunia lakini kwa uhodari wao wote na kucheza timu kubwa zilizobeba taji hilo la Ulaya, wao hawakufanya kutwaa taji hilo walipokuwa kwenye timu hizo.

Phillip Cocu

Cocu kwa sasa ni kocha wa PSV, lakini kwenye michuano hiyo ya Ulaya akiwa mchezaji alicheza mechi 79, akianzia kwenye kikosi hicho cha Uholanzi kabla ya kwenda kudumu kwa miaka sita katika kikosi cha Barcelona.

Kwa bahati mbaya, Cocu aliondoka Camp Nou kuachana na Barca muda mfupi tu kabla ya wababe hao wa Hispania kuanza kutawala kwenye soka la Ulaya, ambapo walinyakua taji kwa mara ya kwanza mwaka 2006, ikiwa ni miaka miwili baada ya Cocu kuondoka.

Patrick Vieira

Vieira ni kiungo mwingine wa nguvu aliyecheza mechi kibao kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kufanya hivyo mara 76 katika klabu tatu; Arsenal, Juventus na Inter Milan.

Staa huyo wa Ufaransa alikaribia kabisa kubeba taji hiyo, lakini ndiyo hivyo mambo hayakuwa mazuri kwa upande wake. Aliondoka Arsenal miezi 12 kabla ya wakali hao wa London kufika fainali mwaka 2006 ambako walikwenda kupigwa na Barcelona na alipokuwa Inter Milan, aliondoka Januari 2010, wakati mwisho wa msimu wenzake walikwenda kubeba taji hilo la Ulaya, hivyo akakosa medali ya ubingwa.

Fabio Cannavaro

Mmoja wa magwiji wa soka la Italia. Cannavaro alicheza mechi 138 za kimataifa na alikuwa moto, alishinda pia tuzo ya Ballon d’Or mwaka 2006.

Lakini, mambo hayakuwa hivyo kwenye soka lake la klabu, akipita kwenye timu nyingi kubwa kama vile, Parma, Inter, Juventus na Real Madrid na kushindwa kuibuka na medali ya ubingwa wa michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakati baadhi ya timu hizo alizochezea zimewahi kunyakua ubingwa wa michuano hiyo ya Ulaya.

Cesc Fabregas

Fabregas amecheza zaidi ya mechi 100 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini Mhispaniola huyo ameishia kushika namba mbili tu kwenye ubingwa huo wakati huo alipokuwa Arsenal na kuchapwa na Barcelona kwenye fainali ya mwaka 2006.

Baadaye aliondoka kwenda Barcelona akiwa na ndoto za kunyakua taji hilo, lakini hilo halikutimia kwa sababu staa huyo anayecheza Chelsea kwa sasa, alipishana tu na kipindi muhimu za Barcelona kubeba ubingwa huo wa Ulaya.

Alikwenda Barcelona wakati wakiwa wameshabeba mataji manne na alipoondoka mwaka 2014, huko nyuma wenzake wakabeba taji la tano. Cesc ameshindwa kusoma alama za nyakati.

Ruud van Nistelrooy

Akiwa na mabao 56 aliyofunga kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Van Nistelrooy, ni mmoja wa wafungaji wa mabao mengi katika michuano hiyo ambao wameshindwa kubeba ubingwa wenyewe.

Straika huyo wa Kidachi alitua Manchester United miaka miwili baada ya kushinda ubingwa michuano hiyo mwaka 1999 na aliondoka kwenye kikosi miaka miwili kabla ya kubeba ubingwa wao mwingine wa Ulaya. Huko alikokwenda, Real Madrid, alishindwa pia kubeba taji hilo kwa miaka minne aliyotumikia timu hiyo ya Santiago Bernabeu. Ndiyo hivyo, Van Nistelrooy amejikuta tu na bahati mbaya licha ya kufunga mabao 56 katika mechi 73 alicheza katika michuano hiyo.

Hernan Crespo

Alikuwa kwenye kikosi kimoja cha Parma iliyokuwa na staa Cannavaro. Fowadi huyo wa Kiargentina alikwenda kucheza pia klabu bora kabisa za Ulaya na hata aliwahi hata kufunga mabao mawili katika mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini hakushinda ubingwa.

Bahati mbaya kwa Crespo ni kwamba mwaka 2005 kwenye fainali dhidi ya Liverpool, alifunga mabao mawili na kuifanya AC Milan kuongoza 3-0 hadi mapumziko. Lakini, kwenye kipindi cha pili, Liverpool walirudisha mabao yote hayo na kwenda kushinda fainali hiyo kwa mikwaju ya penalti.

Akaondoka hapo kwenda Inter Milan, lakini kitu kibaya kwake nako aliondoka mwaka mmoja kabla ya timu hiyo kwenda kubeba ubingwa wa Ulaya wakiwa chini ya Jose Mourinho mwaka 2010.

Pavel Nedved

Nedved, kama Crespo tu, ni miongoni mwa mastaa ambao timu zao zilifika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini ubingwa umeshindwa kupatikana. Nedved alikuwa kwenye kikosi cha Juventus kilichofika fainali na kuchapwa na AC Milan mwaka 2003.

Staa huyo wa Czech hakucheza mechi hiyo ya fainali iliyofanyika kwenye Uwanja wa Old Trafford kwa sababu alikuwa na adhabu ya kadi, hivyo aliishia kukaa tu jukwaani akishuhudia timu yake ikichapwa na hivyo ubingwa kubebwa na Rossoneri.

Ronaldo

Wajina wake, Cristiano, usiku wa jana alikua anatafuta medali ya tano ya ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini Mbrazili Ronaldo hajawahi kushinda ubingwa wa taji hilo licha ya umaarufu wake wote katika kuucheza mpira.

Kwenye soka la Ulaya, Ronaldo, alipita kwenye vikosi vya PSV, Inter, Barcelona, Madrid na AC Milan, ambavyo vyote vilikuwa vikosi matata katika kutamba kwenye michuano hiyo ya Ulaya. Mambo hayakuwa sawa na mshindi huyo wa tuzo ya mchezaji bora wa dunia kwa mwaka 1997 na 2002, hadi alipoondoka kwenye soka la Ulaya, hakuwahi kunyakua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa.

Lilian Thuram

Kama Nedved, Thuram, naye aliishia kuwa namba mbili mwaka 2003 na jambo tofauti ni kwamba Mfaransa huyo alicheza kwenye fainali hiyo akiwa kwenye kikosi cha Juventus.

Beki huyo wa kulia alitimiza wajibu wake kwa kuwabana Milan kwa dakika 120 na mechi kumalizika kwa sare ya bila kufungana, lakini David Trezeguet, Marcelo Zalayeta na Paolo Montero walikwenda kukosa mikwaju yao ya penalti na hivyo kuwafanya Milan kuibuka na ushindi. Thuram baadaye alikwenda kujiunga na Barcelona, lakini ilikuwa baada ya kubeba ubingwa wao wa Ulaya mwaka 2006 ilipoichapa Arsenal kwenye mchezo wa fainali.

Michael Ballack

Kumaliza wa pili kwenye timu moja tu si kitu kizuri, je kufanya hivyo ukiwa na timu mbili tofauti unajiona jinsi gani ulivyo na gundu. Hilo ndilo lililomtokea kjiungo wa Kijerumani, Michael Ballack.

Kwanza aliishia wa pili baada ya kikosi chake cha Bayer Leverkusen kuchapwa na Real Madrid katika mchezo wa fainali uliofanyika mwaka 2002, kabla ya jambo hilo kwenda kumtokea tena akiwa na Chelsea miaka sita baadaye. Fainali za mwanzo, Zinedine Zidane ndiye aliyemfanyia kitu kibaya akifunga bonge la bao, lakini fainali ya pili iliyofanyika mwaka 2008 dhidi ya Manchester United huko Moscow, John Terry na Nicolas Anelka ndiyo waliotibua mambo baada ya kukosa mikwaju yao ya penalti.

Zlatan Ibrahimovic

Straika huyo wa zamani wa Manchester United anashikilia rekodi hiyo mbaya kabisa asiyoitaka baada ya kucheza mechi kibao kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini akishindwa kuwa bingwa.

Zlatan amecheza mechi 120, tena kwenye timu za maana kuanzia Inter, Juventus, AC Milan, Barcelona, PSG na Man United, lakini kote huko hakuna alichoambulia linapokuja suala la kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Zlatan alipishana na ubingwa wa Ulaya wakati alipoondoka Inter, ambapo mwaka uliofuata wenzake wakabeba ubingwa na ilikuwa hivyo wakati alipoondoka Barcelona, wenzake nyuma wakanyakua taji hilo. Kama siyo gundu basi ni nini.

Gianluigi Buffon

Buffon ndiye mtu aliyecheza mechi nyingi kwenye kikosi cha Italia kuliko Cannavaro na yupo mbali kweli kweli baada ya kufanya hivyo mara 176.

Alinaswa kutoka Parma kwa ada iliyoweka rekodi ya dunia mwaka 2001, Euro 52 milioni na hakika alikuwa mmoja wa makipa mahiri kabisa kwenye kikosi cha Juventus kilichokuwa na wachezaji wengi wa maana akiwamo Alessandro Del Piero.

Lakini, Buffon, ambaye ameachana na Juventus mwaka huu, uhodari wake wote wa kuwa golini na kucheza mechi kibao za Ligi ya Mabingwa Ulaya, amejikuta akiishia kushika nafasi ya pili kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa miaka michache ya hivi karibuni, akifungwa na Barcelona na kisha kuja kufungwa na Real Madrid kwenye mechi za fainali, hiyo ni mwaka 2015 na 2017.