Kama sio Ajibu basi ni Fei Toto

Muktasari:
Kufuatia kuadhibiwa kwa Andrew Vicent 'Dante' kutokana na utovu wa nidhamu alioufanya kwenye mchezo wa Simba na Yanga, Ninja ambaye alikuwa akitumika kama kiungo mkabaji amejikuta akipangwa kwenye mchezo uliopita dhidi ya KMC nafasi aliyoizoea ya beki wa kati.
UNAAMBIWA ukicheza na Yanga usipoadhibiwa na Ibrahimu Ajibu 'Kadabra' basi kaa ukijua atakufyekelewa mbali ni Feisal Salum 'Fei Toto' kwa mipira ya kutenga ‘faulo’.
Juzi Alhamisi usiku Uwanja wa Taifa, Fei Toto alionyesha kuwa na yeye yumo kwenye upigaji wa mipira ya kutenga kwa kukwamisha mpira nyavuni mwa KMC dakika ya 89 ya mchezo huo uliomalizika kwa Yanga kushinda bao 1-0.
Awali, Yanga ilikuwa ikimtegemea Ajibu pekee alinayeonekana na ustadi mkubwa wa kupiga mipira ya kutenga maarufu kama faulo nje ya 18 au karibu ya goli la wapinzani wao.
Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amefurahishwa namna ambavyo Fei Toto alivyomfunga kipa wa KMC, Juma Kaseja kwa kusema anatakiwa nyota wake huyo kufanya mazoezi zaidi ili awe na kiwango bora zaidi cha upigaji wa faulo.
“Feisal anatakiwa kuendelea kufanya mazoezi zaidi ili awe bora. Tunaye Ajibu ambaye ana uwezo wa kupiga faulo kwa hiyo naona ni faida kwetu kuwa na mchezaji zaidi ya mmoja wenye uwezo wa kutusaidia kufunga kwa njia hiyo,” alisema kocha huyo.
Hata hivyo, Zahera alimwagia sifa kiungo huyo kwa kusema amekuwa akicheza kwa kufuata maelekezo ya kucheza mbele ya mabeki wa kati licha ya kuwa na uwezo wa kucheza kama kiungo mshambuliaji.
Zahera amekuwa akipenda kumtumia Feisal kwenye eneo hilo ili kutengeneza uwiano wa uchezaji kuanzia kwenye eneo la nyumba kwenda kwenye eneo la ushambuliaji.
NINJA KWA YONDANI FRESHI
Beki wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ amesema anavutiwa kucheza na Kelvin Yondani kwa kusema mara zote amekuwa na maelewano mazuri pindi anapopata nafasi ya kucheza naye.
“Yondani ni mzoefu na isitoshe ana uwezo wa kuongoza na kuelekeza namna gani ya kufanya kazi kwa pamoja, nina vitu vingi vya kujifunza kutoka kwake,” alisema beki huyo.