Kalala afichua mazito kuhusu Muna Love

Muktasari:
Muna alidai kwamba hata mumewe huyo alijua kwamba alipata ujauzito huo wa Casto siku chache kabla ya ndoa yao, lakini walificha iwe siri ya ndoa hiyo iliyodumu kwa miaka 10.
MAMBO ni mengi muda mchache. Habari ya wiki hii ilikuwa ni talaka ambayo msanii wa filamu nchini, Rose Alphone ‘Muna Love’ ameipata kutoka Mahakama ya Mwanzo Magomeni iliyovunja ndoa yake na aliyekuwa mumewe, Peter Komu.
Mume yule ambaye aliingia naye kwenye bifu zito kilipotokea kifo cha mtoto Patrick, ambaye Muna alimzaa ndani ya ndoa hiyo, lakini alipofariki alidai kwamba hakuzaa na Peter bali na mtangazaji wa Clouds, Casto Dickson.
Muna alidai kwamba hata mumewe huyo alijua kwamba alipata ujauzito huo wa Casto siku chache kabla ya ndoa yao, lakini walificha iwe siri ya ndoa hiyo iliyodumu kwa miaka 10.
Mvutano wa nani amzike mtoto kama baba mzazi kati ya Peter na Casto Dickson ulimalizwa kidiplomasia kwa Peter kwenda kuzika baada ya pande mbili (upande wa mume na upande wa mke) kila mmoja kuandaa shughuli za msiba kivyake na kisha pande hizo kukutana njiani na kwenda moja kwa moja makaburini kuzika baada ya mwili wa marehemu kuwasili kutokea Kenya alikofia.
Na wiki hii, ndoa hiyo ikafikia tamati ikivunjwa na Mahakama baada ya mvutano wa muda mrefu kati ya pande hizo mbili. Na sasa kilichobaki ni mvutano wa kujua mgawanyo wa mali, hasa nyumba inayodaiwa wamejenga walipokuwa kwenye ndoa iliyopo maeneo ya Mwananyamala jijini Dar.
Mambo ni mengi. Likiisha hili kuna lile.
Mwanaspoti leo lipo na suala moja ambalo liliwahi kusambaa mtandaoni miaka minne iliyopita kwamba muimbaji wa Bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’, Kalala Junior na Muna Love walifunga ndoa.
Katika mazungumzo yake na Mwanaspoti nyumbani kwake Sinza Afrika Sana, Kalala Junior anafunguka kuhusu uhusiano wake wa kimapenzi na Muna pamoja na safari yake ya muziki, mafanikio na changamoto alizokutana nazo kufikia alipo sasa.
Kalala amekana habari hiyo iliyokuwa ikisambaa katika mitandao ya kijamii na mtaani akisema ilimharibia jina lake kwani hakuwahi kuoa wala kumuoa Muna Love katika maisha yake.
Hata hivyo, Kalala amekubali kuwa alikuwa anajihusisha kimapenzi na Muna na kuishi naye nyumba moja kwa muda wa miaka mitatu, lakini hakumuoa.
“Huwezi amini hii habari ya mimi kuwahi kumuoa Muna inaniumiza hadi leo kila ninapoikumbuka, sababu yule dada sikuwahi kufunga naye ndoa ya kiserikali, kimila na wala ya kidini, ila aliwahi kuwa mpenzi wangu na nilikuwa naishi naye ndani ya nyumba kwa muda wa miaka mitatu na nilimmwaga kipindi kilekile cha hizo habari zilivyoanza kusambaa
“Picha zilizokuwa zikionekana katika mtandao ile ilikuwa ni wimbo ambao uliitwa ‘Muna’, niliutunga mimi ulikuwa unahusu ndoa. Pale ilikuwa ni katika harakati za kufanya maandalizi ya video yake, ndio tukaanza kuweka zile picha kama vile ‘coming soon’ ya kitu kipya. Sasa watu walipoona vile ndio walianza kusema tumefunga ndoa na waliunganisha matukio kwakuwa sisi tulikuwa wapenzi,” anasema Kalala Junior
MKE WA MTU
Wakati Kalala Junior yuko na Muna kimapenzi, mwanadada huyo alikuwa kwenye ndoa na Peter Zacharia Komu.
Mwanaspoti lilimuuliza Kalala Junior aliwezaje kuishi na mke wa mtu ndani ya nyumba kwa muda wa miaka mitatu na muimbaji huyo akajibu: “Mimi nilikuwa naishi na Muna miaka yote hiyo sababu aliachana na mume wake, na nilimuuliza Muna kuhusu mumewe akanijibu hawako pamoja wameshaachana.”
KALALA ALIMFAHAMU MUME WA MUNA KUMBE
Kalala alikuwa mtu wa karibu na wanandoa hao (Muna na Peter). Hata katika shoo za Twanga Pepeta, Muna na mumewe Peter walikuwa hawakosi kuhudhuria. Na wakiwa ukumbini ilikuwa haipiti siku bila ya kumtuza fedha Kalala Junior jukwaani akiwa anaimba, anafunguka muimbaji huyo.
Baada ya wawili hao kutengana na Kalala Junior kuanza kuishi na Muna, muimbaji huyo anasema hakuwahi kufuatwa na Peter kuulizwa kwanini anaishi na mke wake.
“Sikuwahi kufuatwa na Peter kuhusu kuishi na Muna, na nilikuwa naishi pamoja na mtoto wake Patrick (Mungu amrehemu).
AWATAKA WANAMUZIKI WENZAKE ‘WAJIBRAND’
Kwasasa muziki wa dansi ni kama mgonjwa aliye katika chumba cha walio katika uangalizi maalumu (ICU).
Soko la muziki huo limeshuka, zile shoo za kibabe za unzinduzi wa albam kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee zimebaki historia na bendi zinapumulia mashine.
Wakati baadhi ya wanamuziki wanarushia lawama vyombo vya habari kuwa ni chanzo cha anguko la muziki wao kutokana na kuupa kisogo katika promosheni, huku madai mengine yakisema sababu ni wanamuziki kuishiwa ubunifu, Kalala ana mtazamo wake:
“Binafsi sikubaliani sana na hoja hizo zote mbili kwani ukiangalia bendi kama Twanga Pepeta, Sikinde, Msondo, Mapacha na zingine tunajitahidi kutoa nyimbo nzuri, sema sisi wanamuziki tuna tatizo, yaani nyimbo zako zisipochezwa na media fulani basi hauwezi kufika mbali, nasema hivi sababu hii tabia ipo kwa wanamuziki wengi kuchagua media.
“Kingine wanamuziki kujibrand sisi wenyewe ni tatizo. Wanamuziki tunahitaji ushauri nasaha. Sawa media zinabana, tujiulize na sisi tunafanya nini? Kujibrand hatuwezi. Utakuta mwanamuziki ni mzuri kwenye muziki ila mtatufe katika mitandao kama WhatsApp, YouTube, Facebook, Twitter na Instagram huwezi kumkuta au kukuta kazi yake. Inabidi tujitangaze, tusijiwekee unyonge kwamba tunaonewa.”
Aidha, Kalala Junior anasema utaratibu ulioanzishwa na kituo kimoja cha radio kwamba wimbo usizidi urefu wa dakika tatu kweli ulikuwa ni tatizo kwa sababu muziki wa dansi una ladha yake ambayo inatakiwa upigwe kwa dakika tano au sita na kwamba sasa hivi wamerudi kupiga dakika tano au sita na mambo yanaenda vizuri.
MIAKA 19 KWENYE MUZIKI
Ni miaka 19 sasa imetimia imetimia tangu Kalala Junior, ambaye ni mtoto wa gwiji wa muziki wa dansi Komandoo Hamza Kalala, alipoanza safari yake katika muziki wa dansi nchini.
Kalala Junior kwasasa ni Kiongozi wa bendi ya Twanga Pepeta baada ya kuchukua mikoba ya Luiza Mbutu ambaye kwasasa ni Mkurugenzi wa bendi hiyo. Anasema mabadiliko hayajafanyika kwenye uongozi tu bali hadi jina la bendi limebadilika ambapo Bendi ya The African Stars Twanga Pepeta kwa sasa itakuwa inaitwa Twanga Pepeta Entertainment.
Anasema katika miaka hiyo 19 ya muziki anashukuru Mungu amevuna vitu “nusu na robo” kwa miaka hiyo, na robo iliyobaki ndio anasaka kuikamilisha sasa.
“Katika miaka 19 ya muziki, kwanza nashukuru kuwa na uzoefu kwenye muziki, na kwa upande wa mafanikio unajua kila binadamu huwa ana mahitaji yake. Mimi pia kuna malengo niliyokuwa nahitaji kuyafikia katika maisha yangu. Nashukuru muziki umenifanya kidogo kwenye asilimia mia, nimefikia nusu na robo (asilimia 75). Namshukuru Mungu, japo huwa sipendagi sana kutaja kuwa nina hiki au kile hivyo nashukuru Mungu. Na hiyo robo iliyobaki nadhani inaishia ishia sababu muziki ukiuheshimu utakuheshimu na utakupa hitaji lako.
“Sababu muziki ni kama kazi nyingine, nashukuru Mungu mahitaji tunayapata yote, pia katika mafanikio niliyotarajia kuyapata ni kuwa kiongozi wa bendi nashukuru nimekuwa kiongozi, maana nilishawahi kuwa mkurugenzi wa bendi.”
AZUNGUMZIA MAPACHA WATATU
Katika miaka hiyo 19 ya muziki wa dansi, Kalala Junior aliwahi kujiajiri kwa kumiliki bendi ya muziki wa dansi, akiwa ni mmoja wa wamiliki wa bendi ya Mapacha Watatu pamoja na Khalid Chokoraa na Jose Mara.
Anasema hatasahau bendi ya Mapacha Watatu ilivyokuwa ikiwapelekesha bendi kama African Stars ‘Twanga Pepeta’ FM Academia na Mashujaa Misica kwa kujizolea mashabiki wengi na hadi kuchukua tuzo ya Kilimanjaro Tanzania Music Awards 2011 wimbo ulikuwa ‘Shika Ushikacho’ kipengele cha Wimbo Bora kwa upande wa bendi.
Kalala Junior anasema sababu ya kutwaa tuzo na kutingisha bendi ya Mapacha wa Tatu kwa kipindi hicho walikuwa na upendo na mshikamano huku wakisikilizana ikiwa ni pamoja na sapoti kutoka kwa aliyekuwa meneja wao mwenye kuujua muziki wa dansi, Khamis Dacota ndio kiliwasababisha kutunga tungo nzuri.
Anasema kuna changamoto nyingi katika hivyo vitu viwili mfano akizungumzia kabla ya kujiajiri alitokea Twanga Pepeta lakini walitengeneza kitu kikawa juu na mafanikio yakaonekana.
“Kumiliki bendi we acha tu, japo sikufikia kuwa kama Asha Baraka ila kuna changamoto kubwa sana. Unajua kuzoea kuingiza kipato ukiwa umeajiriwa na matokeo yake sasa unakuwa unatoa tu hii ni changamoto. Sasa mimi nikaona kipindi hicho bado sijafika kuwa na ukakamavu wa kuwa kama Asha Baraka, ila wenzangu Chokoraa na Jose Mara kama inavyoona walikomaa hadi sasa kama unavyowaona kila mmoja ana bendi yake
“Yaani mimi isingetokea matatizo binafsi, saa hizi tungekuwa mbali zaidi kwani japo tulikuwa wakurugenzi ila tulikuwa na mtu ambaye mpambanaji katika muziki wa dansi kama nilivyosema mwanzo, Khamis Dacota alikuwa meneja wa Bendi ya Mapacha Watatu, yaani tulikuwa tunakubaliana sisi tukiwa jukwaani ukurugenzi tunauweka pembeni na kumuachia majukumu meneja na sio tu tukiwa jukwaani. Dacota alikuwa anapambana kutafuta shoo Dar na mikoani.”
Usikose Mwanaspoti kesho ujue sababu yake ya kujitoa Mapacha Watatu na skendo yake ya mademu na Chaz Baba.
KWANINI ALIJITOA MAPACHA WATATU
Hatua ya Kalala kuondoka Kundi la Mapacha watatu iliibua mjadala mkubwa kwa mashabiki wa kundi hilo na kutafsiriwa kama usaliti kwake, huku akibainisha sababu za kuondoka kuwa ni pamoja na kutofautiana na wenzake katika masuala ya kuongoza kundi pamoja na ujana.
“Unajua kila mmoja alikuwa ni Mkurugenzi wa Bendi na ukiangalia wote ni vijana si unajua tena, kwa hivyo ule utaratibu wa kujiongoza ukawa na dosari, hivyo Juni 2012 niliamua kupumzika nyumbani kwa muda wa miezi minne bila kuimba, bendi nyingi sana zilihitaji kunichukua lakini nilikataa
“Niliongea na wenzangu nikachukua shea zangu bila ya kugombana ndio maana hata leo unaona nina uwezo wa kupanda kwa chokoraa au Jose Mara “ anasema Kalala Junior.
Hata hivyo, ushawishi ulioupata kutoka bendi mbalimbali ulimulazimu kuchukua sehemu ya umiliki wake katika Kundi la Mapacha na kurudi ‘Twanga Pepeta akieleza kuwa kurejea huko ndiyo sababu ya kutoa albamu ya Nyumbani ni nyumbani.
SAFARI YAKE YA MUZIKI
‘Bantu Group’ inayomilikiwa na mpiga gitaa maarufu la solo nchini na mwimbaji Hamza Kalala, ambaye pia ndiye baba wa Kalala Junior, hiyo ndiyo bendi ya kwanza kuifanyia kazi akiwa mwimbaji mwaka 2000.
Mwanamuziki huyo alianza muziki miezi michache baada ya kumaliza kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Makongo iliyopo jijini Dar es Salaam na kushiriki kuandaa albamu mbalimbali ikiwamo ‘Tutabana hapahapa’ na Ngozi ya Kitimoto.
“Ilipofika mwaka 2002 nikahamia bendi moja iliyokuwa ikiitwa ‘Bambino Sound’ ikiwa chini ya Banza Stone, mkoani Arusha. Baba alikubaliana na hatua hiyo akiwa kama meneja wangu kwa kipindi hicho,” anasema Kalala.
Hata hivyo, anasema kuwa hakuweza kukaa kwa muda mrefu katika bendi hiyo baada ya Kapteni John Komba kupitia Bendi ya TOT Plus, alifanikiwa kupanda dau na kumwamishia bendi hiyo.
Anabainisha baadhi ya sababu zilizomshawishi kukubaliana na mkataba wa TOT kuwa ni ahadi ya kuboreshewa mazingira ya kuanza maisha na kwamba hatua yake ya kuhama ilitokana na ushindani uliokuwepo kwenye bendi na maslahi. “TOT ndiyo walionipatia msingi nikaanza maisha. Mzee wangu akakubali kama meneja na nilianza kula matunda ya kazi ya uimbaji katika bendi hiyo kuanzia mwaka 2003 mpaka mwaka 2005 nilipohamia bendi nyingine ya ‘Mchinga Sound’,” anasema Kalala.
Pamoja na kuondoka bila utata katika bendi hiyo, Kalala alifanikiwa kushiriki uandaaji wa albamu iitwayo ‘Mwaka wa Taabu’.
Anaeleza kuwa akiwa na bendi hiyo ambayo ilibadilishwa jina na kuwa Mchinga Generation, alifanikiwa kukutana na waimbaji wengine nguli akiwamo Ally Choki, Khadija Kimobitel, Rogert Hegga (Katapila) na wengineo.
“Enzi hiyo ushindani ulikuwa mkubwa sana kutoka kwa Fm Academia na African Stars (Twanga Pepeta), nilipiga kazi kwa muda mrefu kwenye bendi hiyo mpaka mwaka 2008, nilipohamia bendi nyingine ya ‘Chipolopolo,” anasema Kalala na kuongeza:
Anabainisha kwamba kuingia bendi hiyo ilikuwa ni njia nyingine iliyochangia kuelekea Twanga pepeta kutokana na umiliki wa tajiri mmoja. “Baada ya kuona uwezo wangu, mkurugenzi wa wa bendi yetu akaamua nihamie bendi yake kubwa,” anasema Kalala.
Watu wategeme e vitu vipya kwenye uongozi mpya,tumeshajua tatizo tulikosea wapi,nafai kuimudu nilishawahi kuwa mkurugenzi wa bendi tunajuana kila mtu na tabia zake, chipukizi kuwapa nafai waje waone tuliambiwa Twanga imekufa hatukufa moyo,tumejitahidi kurudi kama zamani, rasmi mwaka 2000 muziki Bantu Group
AMEJIPANGA HIVI KUONGOZA BENDI
“Kiukweli katika huu uongozi mpya ,watu wategemee mabadiriko katika bendi yetu ya Twanga Pepeta Entertaiment ,tumepanga kurudi na ‘system’ ya zamani ya kutoa wimbo na video kwa pamoja na tutakuwa tunazindua albamu kila mwaka, hivi navyokwambia mwakani tunatarajia kuzindua albamu Twanga mbele huu wimbo nimetunga mimi,Penzi sigara kali ametunga Chaz Baba, Rekebisha umetungwa na Msafiri Diof,Povu umetungwa na Haji Ramadhani ‘Haji BSS’, tunaendelea kutunga nyimbo zingine”
BANZA STONE ALIMFUNDISHA KUPANGA NA MUZIKI
“Mimi ukisema nimzungumzie Marehemu Banza Stone, ukweli Banza ndio amenifanya niwe hivi nadunda, ndio kanisababisha kujua kupanga,alinitoa nyumbani kwenda Mkoani Arusha kwenye hiyo bendi ya Bambino na kuniambia nianze maisha ya kujitegemea kwa kupanga chumba,na mbali na kunifundisha kupanga pia alikuwa ni mwalimu wangu katika kuimba, alikuwa ananiambia imba hivi fanya hivi
“Yaani namshukuru mungu hadi nilikuja chukuliwa na bendi ya Tot,kiufupi Banza alikuwa mshauri wangu sana katika muziki wa dansi,ndio maana hadi leo nimejua kuimba,kutunga nyimbo na kupiga vyombo vya muziki”
Aidha Kalala Junior anasema hata kwa Upande wa msanii Ali Choki pamoja na kufanya nae kazi,pia anatambua mchango wake kwake japo aliporudi toka Kenya Choki alimkuta Kalala Junior anaimba.
“Najivunia sana kumuita Baba mdogo Ali Choki,nimefanya kazi nae,kwa Tanzania katika muziki wa dansi hukosi kulitaja jina la Choki, alienda Nchini Kenya alivyorudi alinikuta naimbanilikuwa bendi ya Mchinga Sound, pia siwezi acha kusema nae amenipa msaada katika muziki wa dansi, Ila Banza Stone ni zaidi ya msaada kwangu na ndio watu wakanijua mimi Kalala Junior”
NDONDO INAUA MUZIKI WA DANSI?
Kumeibuka kwa wanamuziki wengi wa muziki wa dansi hawataki kuwa katika bendi au kufanya muziki binafsi na kutegemea kwenda kupiga ‘Ndondo’ kwenye bendi zingine na kupata pesa ya kula. Tabia hii ipo pia kwa wale ambao wako kwenye bendi siku bendi yake haifanyi kazi inaibuka bendi nyingine kwenda kuimba au kupiga vyombo.
Hapa Kalala Junior anafafanua faida ya ndondo kwa wanamuziki wa dansi “Unajua kupiga Ndondo inategemea ndodo ya aina gani, unaaweza mchukua mtu hawezi kupiga muziki wa dansi au kuimba nyimbo za bendi matokeo yake anakuja kuharibu hapa sasa ndio ndondo inaposhusha muziki wa dansi
“Mwanamuziki wa twanga humkuti kwenye ndondo,ukikutwa huna kazi,sisi inatakiwa upate ruhusa katika uongozi na tunaenda kusalimi sio kwenda kupiga muziki,natoka hapa kuwa leo hatupigi twanga basi naenda bendi fulani kupiga ndondo”
MBALI NA MUZIKI ANGEKUWA NANI?
Anasema Kalala Junior asingekuwa mwanamuziki angekuwa mchezaji mpira wa miguu,kwani toka akiwa mdogo anapenda kucheza mpira.
KUMBE SHABIKI WA YANGA
Kalala Junior anasema,ameanza kujitambua amekuwa akishabikia timu ya Yanga, na ni mmoja wa wajumbe wa kamati ya kuhamasisha wa timu hiyo.
FAMILIA
“Nina mtoto mmoja wa kiume, sina mke ila nina mchumba japo siishi nae hapa nyumbani kwangu, huwa anakuja na kuondoka
“Kwa upande wa Ratiba yangu ya siku, huwa naamka saa kumi asubuhi kama siku sijaenda kazini , huwa nafanya mazoezi binfasi, hii ni tofauti siku nikiwa nimeingia kazini huwa naamka saa 11 asubuhi nakimbia baada ya hapo nakunywa maziwa fresh,saa kumi basket ball baada ya hapo naingia ‘Gym’,ni kitoka ni mwendo wa kulala masaa mengi”
SKENDO YA ‘KUSHARE MADEMU’ NA CHAZ BABA
Kalala Junior na Chaz Baba ni wanamuziki marafiki na urafiki wao umepita hadi kufikia hatua ya undungu na mara nyingi katika matembezi wanakuwa pamoja, na hupenda kujiita Mapacha.Lakini mtaani kuna habari ya kudaiwa kupenda kuchangia wanawake katika mahusiano ya mapenzi.
“Unajua ukishakuwa kioo cha jamiii inabidi ukubaliane na kila kitu hivyo binadamu akiongea mwache aongee, sisi ni washikaji sasa utamtongozaje demu wa rafiki yako? Hakuna kitu kama hicho yaani sisi ni wastarabu sana tofauti na watu wanavyotufikiria”
Kalala Junior anasema alishawahi kuumizwa katika mapenzi, hivyo anafahamu uchungu wa ‘kushare demu’ na rafiki au ndugu kwani anasemamapenzi hayana mjanja na ndio maana jukwaani akiwa anaimba wimbo wa Sumu ya Mapenzi huwa anaimba kwa ‘Filling’ kutokana na kufikiria alivyoumizwa na mwanamke aliyewahi kumpenda kupita kiasi na baadae akaja kuumizwa.
“Nafahamu uchungu na maumivu ya mapenzi,kwani nilishawahi kuumizwa kwa hicho kitendo ambacho watu wanadhani kipo kwangu na rafiki yangu Chaz Baba, acha kabisa wewe maumivu ya mapenzi yanauma sana, yaani hadi leo kuna wimbo wa Sumu ya Mapenzi wa Twanga Pepeta nikiwa naimba jukwaani huwa naimba kwa hisia sana kwani huwa nafikiria maumivu ya mapenzi niliyoumizwa”amasema Kalala Junior