Kagere: Nimejifungia ndani napiga tizi kinoma

LIGI Kuu Bara imesimama kutokana na timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kucheza Kombe la Chan nchini Cameroon na itarejea kutokana na timu hiyo itakapoishia kwenye mashindano hayo ambayo yanashirikisha wachezaji ambao wanacheza ligi za ndani.

Katika kolamu yangu wiki hii ningependa kuzungumzia mambo ambayo yanahitajika kufanywa na wachezaji ambao hawapo katika timu za taifa kwa maana ya kucheza mashindano hayo muda huu ambao tupo likizo fupi.

Jukumu la kwanza kila mchezaji anatakiwa kutambua kazi yake ni mpira. Kwa maana hiyo anatakiwa kuishi katika mazingira ambayo sio shawishi kwa masuala ya mpira ambayo yanawezakupotezea ufiti au utimamu wa mwili ambao alikuwa nao wakati Ligi Kuu inaendelea.

Wanatakiwa kula vyakula ambavyo sio vya mafuta mengi na havitawaongeza miili yao kuwa minene au kuongezeka uzito ili kubaki kama walivyokuwa awali, lakini kwetu Simba tumekuwa na utamaduni wa kupima uzito kabla ya kuondoka na tukirejea.

Mara nyingi tukiwa tunapima uzito wakati wa kuondoka kama hivi kipindi cha likizo huwa tunambiwa au kuachiwa maagizo, kila mmoja anatakiwa kulinda kilo ambazo aliachwa nazo zisiongezeke wala kupungua kwani hizo ndizo sahihi.

Kuna baadhi ya timu katika kipindi kama hiki ligi imesimama huwa wanapewa programu ya kufanya mazoezi wakiwa majumbani kwao ili kuendelea kulinda viwango vyao, lakini miili yao hubaki katika hali ya ushindani ili tutakapokutana pamoja wote tuwe tayari.

Wachezaji tunatakiwa kufanyia kazi ratiba hizo ambazo huwa tunapewa na makocha, lakini ni jambo jema kuongeza na yako binafsi ili kuwa fiti zaidi na inaweza kukusaidia endapo ligi itakaporejea unakuwa upo tayari kwa ushindani dhidi ya aina yoyote ya mpinzani ambaye utakutana naye.

Kama ikitokea kuna mchezaji ambaye atashindwa kufanya hivyo na hatakuwa anaishi katika misingi hiyo, maana yake ligi itakaporejea atakuwa sio bora kama ambavyo alicheza kipindi haijasimama.

Wakati huu ligi imesimama ni vyema kwa mchezaji kupata muda mwingi wa kupumzika kwa maana ukimaliza ratiba yako ya mazoezi unatakiwa kupata saa vyingi za kulala au kukaa bila kufanya shughuli nyingi kama wakati tupo katika mashindano.

Kipindi ligi inaendelea ni ngumu mchezaji kupata siku zaidi ya tatu kuwa nyumbani kupumzika, badala yake utakuwa unasafiri kwenye viwanja mbalimbali kucheza mechi, ratiba za mazoezi kama sio asubuhi, basi jioni au vyote viwili kwa wakati mmoja.

Lakini sasa unaweza kujikuta siku zaidi ya tatu upo nyumbani unatakiwa kupumzika kadri ambavyo unaweza ili ukianza mihangaiko wakati msimu unaendelea uwe tayari kwa hilo, lakini kama ukishindwa kutumia muda huu vizuri unaweza kujikuta ligi inaendelea huku umechoka.

Kipindi hiki pia ni kizuri kuwa karibu na familia ambayo nayo mara zote sio rahisi kuwa na wewe mara kwa mara kutokana na kuwa unaingia muda mfupi na kuwa nje kuitumikia timu kwa muda mrefu.

Kwa mfano, mimi familia yangu ipo huku Rwanda. Kwa hiyo nikiondoka hapa inaweza kupita si chini ya miezi sita bila kurudi kuwaona. Mara zote tunawasiliana na kuonana kupitia simu, kwa hiyo ninapopata muda wa likizo kama hivi nautumia vizuri kuwa karibu nao.

Kwa mfano, tangu nimerudi nyumbani Rwanda sijaenda mahala popote muda wote nipo ndani nafanya mazoezi yangu binafsi ili kuendelea kuuweka mwili wangu fiti na katika hali ya ushindani.

Nina imani kwa upande wetu muda ambao tutaungana na wenzetu ambao wapo katika majukumu ya kitaifa wote tutakuwa sawa, ila eneo ambalo watatuzidi wamekuwa wakicheza mpira na wengine mechi.

Unajua mchezaji unaweza kuwa fiti kimwili, lakini kama ukikosa muda mwingi wa kucheza mpira au mechi siku ambayo utarudi uwanjani lazima kuna mahala utakuwa na upungufu, lakini ukipata muda wa kucheza unarudi katika hali ya ushindani.

Ili mchezaji uwe fiti katika maeneo yote ni lazima pia upate muda wa kucheza mechi, ndio maana unaweza kumkuta mchezaji ana kiwango bora lakini akiwa nje kwa muda mrefu bila kucheza mechi mara kwa mara siku ambayo anarudi uwanjani anaonekana wa kawaida.

Kwa hiyo mwanzoni hapa katika mechi za mwanzo tunaweza kuwa kama tupo chini na sio Simba tu, bali timu zote, lakini baada ya muda mfupi tutarudi katika hali ya ushindani na kila mmoja kucheza katika kiwango chake.