Kagera Sugar, Namungo zapasuka nyumbani

WASHAMBULIAJI wa Dodoma Jiji, Anuary Jabir na Emmanuel Martin wameifanya Namungo kula Christmas vibaya baada ya kuichapa mabao 2-1 nyumbani kwake kwenye Uwanja wa Ilulu, Lindi.
Namungo ambao walikuwa wenyeji wa mchezo huo walianza mechi vibaya kwa kufungwa bao la mapema dakika ya 18 kupitia kwa Jabir aliyefunga akimalizia pasi safi ya Abubakar Ngalema kabla ya dakika ya 26 kusawazisha kupitia kwa Bigirimana Blaise akimalizia pasi ya Sixtus Sabilo.
Baada ya kusawazisha, timu zote mbili ziliendelea kucheza kwa tahadhari na kipindi cha kwanza kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Kipindi cha pili kilirejea kwa timu zote kufanya mabadiliko ambayo yalionekana kuinufaisha zaidi Dodoma Jiji na kupata bao la pili kupitia kwa Martin aliyefunga dakika ya 73.
Katika mchezo mwingine uliopigwa leo, Mbeya Kwanza imetakata ugenini kwa kuichapa Kagera Sugar bao 2-0 mabao yakifungwa na Wiliam Edgar dakika ya 36 na Oscar mwajanga aliyegongelea msumari wa mwisho dakika ya 85.
Baada ya matokeo hayo, Dodoma imepanda hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi na alama 16 huku namungo ikianguka nafasi ya saba na alama zake 12.

Kwa upande wa kagera wao wamekaa nafasi ya 11 na pointi tisa huku Mbeya kwanza ikiwa nafasi ya tisa na alama 10.
Baada ya michezo hiyo kumalizika makocha wa Namungo Hemed Seleman 'Morocco' na Mbwana Makata wa Dodoma walizungumzia namna mchezo ulivyokuwa.
Morocco amesema; "Nawapongeza waachezaji wangu kwa mchezo, tumefanya makosa tukaadhibiwa lakini pia tulitengeneza nafasi ambazo hatujazitumia vizuri, naamini tutafanya vizuri kwenye michezo ijayo," mesema Morocco
Naye Makata amesema; "tuliingia na mpango wa Mashambulizi ya kushtukiza na kutumia nafasi pia kujilinda kwa kutulia.Nawapongeza vijana wangu wamepambana dhidi ya Namungo waliokuwa bora na kupata ushindi" Makata.