Kagera, Simba shoo ya kibabe

HARAKATI za Simba kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, zinaweza kunogeshwa au kukwaa kigingi mbele ya Kagera Sugar ugenini leo Jumatano kwenye Uwanja wa Kaitaba, kuanzia saa 10 jioni.

Ikifahamu fika ushindi utaiweka katika nafasi nzuri ya kusaka fursa ya kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi, Simba inapaswa kuingia kwa hesabu na tahadhari kubwa katika mchezo huo kutokana na historia ya ushindani na ugumu inaoupata pindi inapocheza na Kagera iwe nyumbani au ugenini.

Kumbukumbu zinaonyesha Kagera imekuwa na hulka ya kuivimbia Simba hata inapokuwa inafanya vibaya na hapana shaka mechi baina yao huwa na ushindani na mvuto wa kipekee.

Kudhihirisha hilo, katika mechi 10 za mwisho zilizokutana katika ligi, Simba imeibuka na ushindi mara tano na Kagera Sugar nayo imeibuka na ushindi mara tano na hawajatoka sare.

Katika mechi Kagera Sugar inazokuwa uwanja wa nyumbani, Simba imeibuka na ushindi mara tatu huku Kagera kishinda mara mbili na la kushangaza, matokeo ya sare kwa timu hizo pindi huwa ni nadra kutokea.

Ushindi utaifanya Simba kufikisha jumla ya pointi 55, ikibakiwa na mechi tatu mkononi, ikiwa itaibuka na matokeo mazuri katika mechi hizo itaongoza msimamo wa ligi kwa takribani pointi saba.

Wenyeji Kagera inaingia katika mchezo huo ikiwa haipo katika hali nzuri kutokana na mwendelezo wa kufanya vibaya kwenye ligi.

Timu hiyo inayonolewa na Kocha Francis Baraza, haijapata ushindi katika mechi 10 mfululizo na imetoka sare sita na kupoteza nne na hilo limechangia kwa kiasi kikubwa kuwafanya wawe katika nafasi za chini kwenye msimamo wa ligi, nafasi ya 13 na pointi 27.

Inakutana na Simba ambayo siku za hivi karibuni imekuwa moto na kudhihirisha hilo, imecheza mechi 15 mfululizo za ligi bila kupoteza na imeshinda 12 na kutoka sare tatu lakini katika mechi zake tano za ugenini zilizopita imeshinda zote.

Licha ya kuwakosa wachezaji wawili ambao ni nahodha Erick Kyaruzi na Sadath Mohamed ambao hawako vizuri kiafya, Baraza alisema wamejiandaa vyema kwa mechi hiyo hasa wakichagizwa na kuwa fiti kwa nyota wake Yusuph Mhilu na Mwaita Gereza.

“Tunakutana na miongoni mwa timu bora Afrika, lakini huu mchezo ni wa kwanza kwangu nikiwa Kagera Sugar nyumbani, nilichobaini kwenye michezo miwili ugenini kimenipa wapi pakuanzia nitakapokutana na hao Simba” alisema Baraza.

Kocha wa Simba, Didier Gomes alisema anafahamu ushindani utakuwapo katika mechi hiyo kutokana na wapinzani walivyo kwenye ligi na kuwa nyumbani na ameyafanyia kazi mapungufu yaliyoonekana katika mchezo uliopita dhidi ya Mwadui.

“Tutamkosa Morison tu mwenye adhabu ya kadi ya njano, ila wengine wako fiti na tayari kwa mechi, ninafahamu mechi itakuwa ngumu kutokana na wapinzani walivyo ila kwa maandalizi tuliyofanya tutaondoka na pointi tatu,” alisema Gomes.