Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kabwili afunguka kila kitu, bado yupo Yanga

MIONGONI mwa makipa ambao wanatabiriwa kufanya makubwa wakiwa wadogo ni pamoja na kipa wa Yanga na Taifa Stars, Ramadhan Kabwili.

Mwaka 2017, Kabwili akiwa na timu ya taifa ya vijana wasiozidi umri wa miaka 17, Serengeti Boys walifanya makubwa katika fainali za mataifa ya Afrika kwa U-17 kule Gabon na kuanzia hapo wadau wengi wa soka nchini wakawa na matarajio makubwa.

Baada ya hapo alijiunga na Yanga, ambapo alitumika kwenye timu ya vijana na baadaye ile ya wakubwa alikozidi kuonyesha ubora wake licha ya kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Tangu Novemba mwaka jana, Kabwili hajaonekana ndani ya kikosi hicho na mambo mengi yametokea hapo kati, lakini watu hawafahamu nini kilitochokea. Mwanaspoti limepiga naye stori kibao na mchezaji huyo ambapo kafunguka kupitia makala hii.


ALIPOANZIA SOKA

Kabwili anasema maisha ya soka alianzia katika timu ya Twalipo na kisha kucheza mechi nyingi za mtaani kwenye maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam.

Anasema kuna siku alicheza mechi za mtaani Chanika - Mbuyuni alikoonyesha kiwango bora na wengi waliohudhuria walimpongeza kwa ubora. “Nakumbuka baada ya mechi kumalizika kuna mchezaji mmoja alikuwa Azam B, wakati huo ndio alinichukua na kunipeleka kufanya majaribio katika timu yao na hapo ndipo nilikubalika,” anasema Kabwili.

“Katika majaribio hayo nilionekana kutokana na kiwango bora nilichokuwa nacho wakati huo na nikasajiliwa katika timu ya vijana na Azam wakati huo ikiwa na kipa Metacha Mnata.

“Nakumbuka niliishi katika kikosi cha vijana Azam mwaka mmoja na nusu - tena ndani ya vyumba vyetu vya kulala sikuwa na kitanda nilikuwa nalala chini. “Unajua wakati nafika Azam wachezaji wa timu ya vijana walitimia kila mmoja alikuwa na kitanda chake tayari, kwa hiyo nilipewa godoro nililokuwa natandika chini natumia kulala na asubuhi naliweka pembeni tunaenda mazoezi.

“Baada ya mwaka huo mmoja na nusu nilipata kitanda nilipewa kile cha Metacha aliyekuwa amepandishwa kucheza timu ya wakubwa wakati huo.”


MWINGEREZA AMKATAA

Kabwili anasema 2015 ilibidi afanye uamuzi mgumu kutokana wakati huo kocha wa Azam alikuwa Mwingereza Stewart Hall aliyemwambia hawezi kupandishwa timu ya wakubwa kutokana na umbo lake dogo na kimo chake si kifupi.

“Sifa alizokuwa akizihitaji alizipata kwa Metacha na kumpandisha timu ya wakubwa kama kipa chaguo la tatu. Kiukweli jambo hilo sikulipenda kutokana na sababu alizonieleza,” anasema Kabwili.

“Kilichokuwa kinaniumiza si kunikataa bali sababu alizonipa zilikuwa tofauti na zile nilizokuwa naambiwa kwenye timu ya taifa ya vijana wakati ule Serengeti Boys nilikuwa kipa chaguo la kwanza.

“Ilikuwa haina jinsi nilifanya uamuzi kwenda Yanga iliyokuwa inanihitaji nikasaini mkataba wa muda mrefu ambao mwisho wa msimu huu ndio unakwenda kumalizika.

“Kiuweli Azam wamenilea na kunipa mafunzo na misingi ya soka ila ilikuwa haina jinsi kuondoka kutokana na changamoto hiyo niliyokuwa nimekutana nayo wakati huo.”


MAISHA YA YANGA

Kabwili anasema 2017 ndipo aliunganishia dili la kutua Yanga na kukutana na makipa wawili wakubwa Youthe Rostand ambaye ulikuwa msimu wake wa kwanza na Benno Kakolanya aliyekuwa mwenyeji wao kwani alikuwa anacheza msimu wa pili.

“Kuna vitu walinifundisha na kunielekeza cha kufanya tukiwa mazoezi na kwenye baadhi ya mechi na nikaendelea kuimarika kiwango changu tofauti na wakati sijaingia hapo,” anasema Kabwili.

“Ndani ya Yanga nimekutana na watu tofauti wenye asili ya maeneo mbalimbali wamenifundisha jinsi ya kuishi, kutafuta kipato nje ya mpira, kuwekeza pamoja na kutumia vizuri kile nachopata katika maisha ya mpira kwani kuna kustaafu.

“Nimebadilisha maisha yangu pengine kupiga hatua tofauti na nilivyokuwa awali na hata ikitokea leo nimeenda kutafuta maisha sehemu nyingine nina vitu vya kujivunia. Kuna changamoto nimepitia Yanga kama kuna wakati niliamini nastahili kucheza ila nikawa nawekwa nje, lakini mambo mengi niliyopita yalikuwa ya raha na yenye kujifunza.”



SKENDO SASA

Uongozi wa Yanga Desemba 19, 2021, ulimsimamisha Kabwili na kuondolewa kwenye kikosi cha timu hiyo kilichokuwa kambini Kigamboni kutokana na masuala ambayo alihusishwa nayo ambayo ni kinyume na tamaduni za Kiafrika. Matatizo yaliyotokea kabla ya kusimamishwa kwa Kabwili na Yanga yamemfanya kupoteza wafuasi waliokuwa wakiamini kuwa anaweza kuwa mmoja wa makipa bora nchini miaka ijayo.

“Nimejisikia vibaya, lakini kwa bahati nzuri wapo ambao wameanza kurejesha imani kwangu. (Hata hivyo) siwezi kurudishwa nyuma na mapito,” anasema Kabwili.

“Mitihani tumeumbiwa wanadamu hakuna jambo gumu ambalo nimekumbana nalo kwenye maisha yangu ya mpira kama hilo. Kila mtu anasema lake, mimi ndiye ninayeujua ukweli. Nashukuru Mungu kwa sasa natazama mbele.”


YANGA BINGWA

Msimu huu wa Ligi Kuu unaonekana kuwa mgumu kwa timu nyingi, lakini Kabwili anaipa Yanga nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa, huku watani zao wa jadi, Simba akiwapa asilimia 30 tu za kupata taji hilo.

“Kwa sasa nitagawa asilimia 70 kwa 30. Hizo 70 ni za Yanga kuchukua ubingwa na zilizobaki nawapa Simba lakini kiuhalisia Yanga inakuwa bingwa msimu huu,” anasema.

“Kuna vitu vingi vilikuwa vinaifanya Yanga isipate ubingwa kwa misimu kadhaa iliyopita lakini uwanjani tulifeli zaidi kwenye eneo la ushambuliaji. Karibu kila msimu tulibadili washambuliaji, lakini changamoto ya kufunga iliuendelea kuwepo.

“Ukiangalia msimu huu, licha ya timu kuimarika kila idara lakini eneo la ushambuliaji limekuwa bora zaidi. Ukimuangalia Fiston Mayele mshambuliaji wa kati

amefikisha mabao 10 na kwa jinsi anavyocheza unamuona akiendelea kufunga kwenye mechi zijazo sambamba na wengine ambao ni bora pia. Nawapongeza viongozi na kila mtu aliye ndani ya Yanga kwa jitihada wanazozifanya kuhakikisha timu inaishi vizuri na kutimiza kila kitu ndani ya muda.”


YUPO YANGA

Kabwili anasema haonekani katika mazoezi na mechi za Yanga kutokana na matatizo yaliyomkuta na kupeww muda wa kupumzika kujiweka sawa kiakili.

Anasema sio kazi rahisi kuweza kuyachukulia kama kawaida na kuishi katika jamii ya binadamu wengine kwani mtu mwingine anaweza kupoteza maisha.

“Naomba niweke wazi leo kupitia heshima ya Mwanaspoti ingawa nafanya jambo la nje ya makubaliano na viongozi wangu bado nipo Yanga, napokea mshahara wangu kwa wakati na posho kama ilivyo kwa wachezaji wengine,” anasema.

“Kiukweli nimeamua kuweka wazi kwa sababu sio jambo dogo viongozi wangu wanalifanya, sipo ndani ya timu kwa maana ya kufanya mazoezi ili nipo kumkataba lakini wananipatia kila kitu kwa wakati.” Mkataba wangu na Yanga umebaki wa miezi minne na mwisho wa msimu huu ndio utamalizika baada ya hapo nitawafuata na kuwauliza wapo tayari kuendelea na mimi au nitafute changamoto mpya sehemu nyingine.”


MSHERY DAMU DAMU

Licha ya kwamba kwa sasa yuko nje ya timu, Kabwili amefunguka kuwa mshikaji wa karibu na kipa mpya wa timu hiyo Aboutwalib Mshery aliyesajiliwa na vinara hao wa Ligi Kuu Bara akitokea Mtibwa Sugar tangu kitambo. “Mshery ni miongoni mwa rafiki zangu wa karibu sana na hata nje ya urafiki pia nimedaka naye kwenye timu za taifa tangu U-17, U-20 na U-23 hivyo tupo karibu sana na muda mwingi tunapiga stori na kushauriana,” anasema Kabwili.

Hata dili yake kujiunga na Yanga nilikuwa naijua tangu mwanzo na siku anakuja kusaini aliniambia nikamtakia heri, pia nikamkaribisha aje tufanye kazi.

“Tangu wadogo tulikuwa tunatamani siku moja tuje kuidakia klabu moja kwa wakati mmoja na hatimaye imetokea. Mshery ana nidhamu na kipaji kikubwa na Yanga ndio sehemu sahihi kwake kwa sasa.”


KAGERE NOMA

Ukimuuliza Kabwili ni mshambuliaji gani hawezi kumsahau Ligi Kuu Bara hasiti kumtaja Meddie Kagere wa Simba, huku akimtaja kuwa mshambuliaji hatari kwa muda wote ambao amecheza soka.

“Kagere ndiye mshambuliaji siwezi kumsahau hadi sasa. Yule jamaa ni mshambuliaji hatari na kila muda anawaza kufunga tu. Katika maisha yangu kama kipa sijawahi kucheza na straika mgumu kama yule,” anasema.

“Mfano kuna mechi tulicheza nao (Simba) 2019 nikiwa golini nilijitahidi kumdhibiti lakini mwisho wa siku alifunga bao pekee la ushindi kwao. Nakumbuka nilijitahidi kupambana naye, hakupata nafasi nyingi zilikuwa kama tatu nikacheza mbili na moja ndio akafunga na kunitibulia mipango kwani nilitamani kumaliza mechi bila kuruhusu bao.”


FAMILIA YAKE

Kabwili anasema kwa sasa anajitegemea. “Nimebaki na mama yangu mzazi anayeishi Kibaha, namshukuru Mungu maisha ndio nimeamuanzishia huko na kiukweli anajivunia mtoto wake kucheza Yanga.

“Nieleze tu licha ya magumu na changamoto ninazopitia, kupitia miguu na mikono yangu napambana kwa ajili yao kwani mimi ndio kama baba yaani kila kitu kwao,” anasema Kabwili anayeamini msimu ujao atakuwa katika milingoti miwili akicheza.

Imeandikwa na Ramadhan Elias, Eliya Solomon na Thobias Sebastian.