JUU YA KILELE: Ujerumani, Argentina ya 2014 kujirudia

Ni kama vile unatazama filamu ya kihindi. Sterling anamzaba tu mtu kibao halafu anakufa. Inatokea kwenye filamu za Kihindi tu.

Inaweza pia kutokea Sterling anakimbizwa na majambazi halafu katikati ya safari wakaanza kucheza muziki. Huwa inatokea tu kwenye filamu hizo za India. Unawezaje kucheza muziki wakati kuna watu wanakusaka wakuue? Ni ajabu na kweli.

Drama hizi za filamu za Kihindi nazo zimetokea kwenye soka. Ilianza kama utani. Ufaransa ikampiga chini staa wake, Antony Martial.

Wadau wa soka wakapigwa na butwaa hasa wakitazama kiwango cha winga huyo wa Manchester United kwenye msimu uliopita.

Baada ya hapo ikafuatia Ubelgiji. Ikampiga chini staa wake, Raja Naingolan. Nani alitarajia kiungo huyo wa shoka angeweza kuachwa kwenye michuano hiyo mikubwa duniani.

Naingolan ni mwanaume kweli kweli. Anakaba kama hakuna kesho. Anamiliki mpira, anachezesha timu, anapiga mashuti ya maana na kufunga. Siyo kiungo wa kawaida n ahata kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya alikinukisha kinoma akiiwezesha Roma kufika robo nusu fainali.

Kocha wa Ubelgiji, Roberto Martinez alisema amemuacha Naingolan kwa sababu za kiufundi. Kwake aliona ni vyema akaenda na Maroune Fellaini kuliko Naingolan. Utasema nini zaidi baada ya hapo.

Filamu hii ya kihindi ikaendelea tena na tena. Wachezaji wengi zaidi wakaachwa. Watu wakajiuliza maswali juu ya uwezo wa nyota hao waliotemwa kwenda Kombe la Dunia. Mwisho wa siku yalibaki kuwa maamuzi ya kocha.

Sasa utamu zaidi ulikuwepo kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Argentina. Changamoto kubwa ikawa kwenye safu ya ushambuliaji.

Argentina imejaaliwa vipaji usikwambie mtu. Kwenye safu ya ushambuliaji kulikuwa na Gonzalo Higuain, Paulo Dybala, Sergio Aguero, Manuel Lanzini na Leonel Messi.

Kocha wa Argentina, Jorge Sampaoli alikuwa na kitendawili kikubwa. Mastraika hao wote wamefanya vizuri na timu zao. Hakuna aliyehusika kwenye mabao chini ya 20 kwa msimu uliopita. Unamuacha nani? Hicho kilikuwa kitendawili kikubwa.

Mwisho wa yote, Sampoali aliamua kumchinja Mauro Icardi. Straika wa Inter Milan aliyefunga mabao 29 kwenye Seria A msimu uliopita.

Ilihitaji roho ngumu sana kufanya uamuzi kama huo.

Unamuachaje straika mwenye mabao hayo katika kikosi cha timu ya Taifa? Ni vigumu. Hata hivyo, Sampaoli hakuwa na la kufanya.

Aguero, Dybala, Higuain na Messi wote walikuwa moto.

Argentina ilihitaji kumpunguza straika mmoja mzuri ili kukidhi idadi ya wachezaji 23 wanaohitajika kwenye Kombe la Dunia. Hakukuwa na namna, ilibidi Icardi achinjwe tu. Japokuwa sasa anaweza kurudishwa baada ya Lanzini kuumia.

Filamu hii tamu ikahitimishwa pale Ujerumani. Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani, Joachim Low alihitaji kikosi cha wachezaji 23 wa kwenda Russia. Aliita wengi zaidi katika kikosi cha awali.

Akafanya nao mazoezi. Akacheza nao mechi kadhaa za kirafiki ili kuona ni nani yuko vizuri zaidi kwenda na nani abaki. Mwishowe panga likapita na kinda wa Manchester City, Leroy Sane.

Ni habari iliyosikitisha sana. Unawezaje kumuacha Sane kwenye kikosi chako? Ni ngumu sana. Hata hivyo, Ujerumani imemuacha kwenye kikosi kinachokwenda Russia.

Ujerumani imeamua kwenda na Julian Draxler na kumuacha Sane. Haikuwa habari njema hata kidogo.

Sane ni mchezaji bora chipukizi wa Ligi Kuu ya England msimu uliomalizika. Alihusika kwenye mabao 33 msimu uliopita.

Alifunga mara 14 na kutengeneza mengine 19 katika michuano yote. Unamuachaje mchezaji kama huyu kwenye kikosi kinachokwenda Urusi? Inahitaji robo mbaya kidogo.

Hata hivyo, Wajerumani wamemuacha. Wameamua kwenda na Draxler wakitumaini kuwa atakuwa na faida kubwa za kiufundi kuliko Sane. Utasema nini juu ya hili? Hakuna.

Mwisho wa yote, tofauti ya Ujerumani, Argentina na timu nyingine imeanza kuonekana mapema. Ni timu hizo mbili tu mpaka sasa zimelazimika kuacha wachezaji wao bora kuelekea kwenye michuano hiyo.

Timu nyingine zinazokwenda Kombe la Dunia zinatamani kuwa na straika kama Icardi, lakini hawana. Ila Argentina walilazimika kumkata. Wana mastraika wengi wenye uwezo mkubwa kuliko Icardi.

Ni timu gani inayokwenda Kombe la Dunia ina safu hatari ya ushambuliaji kama Argentina? Hakuna. Brazil ina Neymar, Philippe Coutinho na Roberto Firminho. Hawana nguvu kubwa kama Argentina.

Kwa Sane ndiyo machozi yanaweza kukutoka. Ni mchezaji wa daraja la juu. Ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira. Ana kasi na uwezo mkubwa pia wa kupiga krosi. Ana uwezo mkubwa pia wa kupunguza mabeki na kutoa pasi za mwisho.

Timu nyingi zinazokwenda Kombe la Dunia zinatamani kuwa na winga kama Sane, lakini hawana. Ila Ujerumani wala haikuwaza mara mbili kumkata. Ujerumani ina kina Sane wengi tu, kwao siyo ishu.

Hii ndiyo tofauti ya Argentina, Ujerumani na timu nyingine zinazokwenda Russia. Timu hizo mbili zimekamilika kila idara. Zinaweza kuchagua mtu wa kwenda na mtu wa kubaki. Hazina hofu wala kidogo.

Mwisho wa siku, natumai Argentina na Ujerumani zitafanya makubwa kwenye Kombe la Dunia. Vinginevyo zikutanishwe tu mapema ili mmoja atoke. Tofauti na hapo, huenda tukashuhudia fainali ya mwaka 2014 ikijirudia.