Juma Liuzio ajitetea kiaina

Muktasari:
- Mkosi huo ulianza kumkumba Liuzio tangu alipokuwa Zesco ya Zambia kwani kwa mwaka mmoja na nusu aliokaa klabuni hakucheza kabisa katika mashindano hayo.
REKODI zinaonyesha straika wa Simba, Juma Liuzio hana bahati kabisa na mashindano ya kimataifa na tangu aanze kucheza soka hajawahi kucheza hata dakika moja katika mashindano hayo kwa ngazi ya klabu.
Mkosi huo ulianza kumkumba Liuzio tangu alipokuwa Zesco ya Zambia kwani kwa mwaka mmoja na nusu aliokaa klabuni hakucheza kabisa katika mashindano hayo.
Sasa habari mbaya zaidi ni, Simba ilipocheza mechi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Gendarmerie ya Djibouti, Luizio hakuwepo kutokana na kuwa na matatizo ya kifamilia. Kwenye mechi ya ugenini kule Djibouti hakucheza, pia kwenye mchezo wa Jumatano iliyopita dhidi ya Al Masry hakucheza.
“Kipindi Zesco inashiriki michuano hiyo nilikuwa majeruhi kwa hiyo nisingeweza kucheza. Kwa Simba wakati wanaanza kucheza mechi ya kwanza nilikuwa na matatizo ya kifamilia, ila kwa sasa nipo kwenye orodha ya majina ya wachezaji ambao wanaenda kucheza mechi ya marudiano dhidi ya Al Masry, nitacheza tu hakuna kinachonizuia juu ya hilo,” alisema.